Na Salum Vuai, Maelezo
KATIKA mikakati yake kujiandaa kwa ajili ya ligi kuu ya soka Tanzania Bara, timu ya Coastal Union ya kutoka Tanga, imeamua kupiga kambi hapa Zanzibar itakayodumu kwa muda wa wiki moja.
Ligi kuu ya Tanzania Bara inayodhaminiwa na kampuni ya simu Vodacom, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 15, mwaka huu.
Timu hiyo iliwasili kisiwani hapa tangu juzi, ikitokea Dar es salaam, ikiwa chini ya makocha wake Juma Mgunda na Habib Kondo, na jana asubuhi ilianza mazoezi katika uwanja wa timu ya Shangani ulioko Mnazi mmoja.
Kocha msaidizi wa timu hiyo Habib Kondo, alisema kuwa wameamua kuweka kambi mjini Unguja ili kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea ligi kuu.
Kondo alisema, wakiwa mjini hapa, wanatarajia kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu ikiwemo dhidi ya mabingwa wa soka wa Zanzibar, Super Falcon, ambayo imepangwa kuchezwa leo katika uwanja wa Ngome Fuoni.
Aidha Chama cha Soka Zanzibar kimeipangia timu hiyo kuvaana na Zimamoto keshokutwa Ijumaa katika uwanja huohuo, na huenda Septemba 11, ikapambana na Mafunzo
No comments:
Post a Comment