Habari za Punde

Dk Shein ataka kasi iongezwe wakati wa kuwajibika

Na Rajab  Mkasaba
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka viongozi na watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wao wa kazi na kushirikiana pamoja katika kutekeleza Mpango wa miaka mitano wa utekelezaji wa MKUZA II.
Hayo aliyasema katika hotuba fupi ya ufungaji wa semina ya siku tatu iliyowashirikisha viongozi na watendaji wakuun wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliyofanyika huko katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Semina hiyo ambayo ilibeba maudhui ya kuimarisha uhusiano baina ya viongozi wa kisiasa na kiutendaji katika Serikali ya Mapinduzi ikiwa na kauli mbiu ya ‘Viongozi lazima tubadilike’ilijadili mada kuu tisa na kuweza kuchangiwa na washiriki hao na hatimae kuja na maazimio kadhaa.
Katika maelezo yake, Dk. Shein aliwataka viongozi hao na watendaji wakuu wa serikali kuongeza kasi katika utendaji wao wa kazi kwa kutambua kuwa wao ndio kigezo kikuu cha wale wanaowaongoza katika maeneo yao ya kazi.
Akieleza juu ya Mpango wa miaka mitano wa Utekelezaji wa MKUZA II, Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao kuchukua juhudi za makusudi katika kuipitian na kuisoma vizuri mpango kazi huo wa miaka mitano ili iwe irahisishe utekelezaji wake.
Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa kikao hicho hakitakuwa cha mwisho na wataendelea kukutana katika vikao mbali mbali vikiwemo vile vya Bango Kitita ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa katika kuimarisha na kuleta maendeleo nchini.
Aliwaeleza kuwa kukaa kwao kwa muda wa siku tatu ni kwa ajili ya manufaa ya nchi na kutoa pongezi kwa watoa mada pamoja na washiriki wote kwa michango yao mbali mbali waliyoitoa katika mada hizo zote zilizowasilishwa katika semina hiyo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi na watendaji hao kubadilika na kufanya kazi kwa mashirikiano na kuwa kitu kimoja kwani serikali ni ya watu wote na ndani ya serikali hamna upinzani. “Tukidhamiria tunaweza”,alisisitriza Dk. Shein.
Kufuatia kukamilika kwa uandaaji wa MKUZA II na kuanza utekelezaji wake katika bajeti ya 2010/2011 na kwa kutambua umuhimu wake, Serikali imetayarisha Mpango wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa MKUZA II ambao utatoa mwongozo wa utekelezaji ili kufikia malengo na shabaha zilizowekwa kwa ufanisi zaidi.
Mpango huo unaelezea zaidi maeneo makuu ya vipaumbele na kuweka mtiririko maalum wa program na miradi kwa ajili ya utekelezaji kulingana na rasilimali zinazohitajika ambapo vipaumbele hivyo vimepangwa kwa mwaka ikiwa ni miaka mitano.kuzingatia mahitaji ya kiuchumi, kijamii, kiutawala na mahitaji ya rasilimali fedha.
Mada mbali mbali ziliwasilishwa zikiwemo tathmini ya utekelezaji kazi katika serikali na taasisi zake tangu kufanyika semina za uongozi Mei hadi Juni mwaka jana, Mafanikio yaliopatikana katika ziara za viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nchini China, Uzoefu wa Malaysia katika kutoa huduma kwa wananchi kupitia mfumo wa kufuatilia na kupima utendaji wa shughuli za serikali “Pemandu”.
Mada nyengine ni Mapitio ya Dira ya Maendeleo ya 2020 Zanzibar, Mpango wa miaka mitano wa utekelezaji wa MKUZA II sehemu ya pili, Mpango wa Ufuatiliaji na utekelezaji wa MKUZA II, Ripoti ya Idadi ya watu Zanzibar 2011, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 2011/2012 na mada iliyohusu e. Governmet.
Miongoni mwa maazimio yalitolewa katika semina hiyo kutokana na mada hizo ni pamoja na viongozi wa Serikali kusimamia dhamana za kazi zao na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanawajibika kikamilifu.
Aidha, Wabunge, Wawakilishi, Masheha na Madiwani washirikishwe kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo. Pia Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananachi Kiuchumi na Ushirika iandae mkakati wa kuendeleza mpango wa ajira na kuwaandaa vijana wa Zanzibar kuondokana na tabia ya kuchagua kazi.
Aidha taaluma ya matumizi ya mtandao kwa viongozi na watendaji wa Serikali ili kuweza kutmia vizuri teknolojia ya e- Government pamoja na kuwataka watumishi wa serikali kujiandaa kimafunzo kwa ujio wa teknolojia hiyo.
Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walishiriki kikamilifu semina hiyo akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, Spika, Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu, Wakurugenzi, Maafisa Tawala, Mahasibu wakuu wote wa Wizara, Wenyeviti wa Halmashauri za Mikoa na Wilaya pamoja na viongozi wengine wa SMZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.