Habari za Punde

Bilioni moja zatumika kuendesha miradi ZAPHA+

Na Mwanajuma Mmanga
SHILINGI bilioni 1,024.916.646 zimetumiwa na jumuiya ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar ( ZAPHA+) katika utekelezaji wa miradi na majukumu yake mbali mbali kwa kipindi cha Januari 2011 hadi Oktoba 2012.

Fedha hizo ni sehemu ya msaada kutoka kwa wafadhili mbali mbali kwa mashirika tofauti kwa lengo la kuwasaidia walioathirika na maambukizi pamoja na uendeshaji wa shughuli mbali mbali za miradi ikiwemo ushonaji, upishi wa sabuni, pamoja na uandaaji wa programu za watoto.

Chini ya mpango huo wa kuboresha maisha ya waathirika unaohusisha kuwapelekea wananchi maendeleo katika maeneo ya shehia zao za mjini na vijijini, fedha hizo pia ziweze kuwasaidia na kuwainua wenye kipato cha chini.

Hayo yalielezwa na Mshika fedha wa jumuiya ya wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar, Rehema Magundo alipowasilisha ripoti fupi ya mapato na matumizi ya fedha ya miezi 18 katika Mkutano Mkuu wa nane wa wadau wa Jumuiya ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar ZAPHA+ uliofanyika ukumbi wa umoja wa watu wenye ulemavu Kikwajuni mjini Zanzibar.

Alisema fedha hizo zilitumika kwa kutengenezea programu na kuelimisha zikiwa ni msaada kutoka mashirika tofauti kwa lengo la kuondosha kabisa maambukizi ya virusi vya ukimwi na kufikia 0.3 kwa wananchi wa Zanzibar.

Nae Mkuu wa kitengo cha elimu na uhamasishaji wa tume ya ukimwi Zanzibar (ZAC), Nuru Ramsa Mbarouk wakati akifungua mkutano aliitaka jamii kuachana na tabia ya unyanyapaa hususan kwa wale watu wanaoishi na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi ili kupata muongozo imara utakaosaidia kupunguza kasi ya maambukizi nchini.

Alisema vitendo vya unyanyapaa vinatakiwa kudhibitiwa ipasavyo katika jamii kwani inaweza kusababisha athari kubwa zaidi kwa watu wanaoishi na maambukizo ya virusi hivyo ikiwemo kupata matatizo ya kiakili, kiafya na kiutendaji jambo ambalo linaweza kurejesha nyuma harakati mbali mbali za kimaendeleo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa jumuiya hiyo, Seif Juma Abdalla amewataka wafanyakazi wa jumuiya hiyo kufanya kazi kwa pamoja na kusaidiana katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoikabili ili waweze kutoa mchango wao kwani wataweza kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi Zanzibar.

Hata hivyo, ameiomba serikali kusaidia huduma za afya na kuhakikisha zinapatikana kwa ukamilifu hasa kwa wanaoishi na virusi vya ukimwi ili kuwasaidia maisha yao.

Aidha alifahamisha kua jumuiya hiyo ina wanachama wanoishi na virusi vya ukimwi waliojitokeza na kusajiliwa. watoto na wanawake wapatao 106 kwa Zanzibar, unguja 159 na Pemba 47.

Alisema takwimu inaonesha idadi kubwa ya wanawake na watoto wanaoongoza kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi na kufikia 0.6 na asilimia 70 ya watoto walio na ukimwi ambao waliachwa na wazee wao na pia hawakupata elimu ya kutosha katika kituo cha afya na baadhi yao kufariki.

Ameziomba taasisi husika na mashirika mengine kuwasaidia fedha za kuweza kujiendeshea jumuiya hiyo ya watoto wenye maisha magumu na walioathirika na virusi vya ukimwi ili wa waweze kuondokana na usumbufu wa kulipia kodi ya ofisi zake.

Mkutano huo umewashirikisha wajumbe kutoka taasisi mbali mbali za serikali na taasisi binafsi ikiwemo Save the children Fund, ZAC, UNICEF na Mashirika mbali mbali


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.