Habari za Punde

Mwanafunzi ajiripua kwa kugombwa na wazazi. Ni mtahiniwa kidatu cha pili

Na Masanja Mabula, Pemba
MTOTO wa kike, mkaazi wa kijiji cha Tondooni Makangale Pemba amelazwa katika hospitali ya Chake Chake kisiwani Pemba kwa matibabu baada ya kujiripua kwa moto.

Habari zilizopatikana kutoka kijijini kwao zinasema mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidatu cha pili (jina tunamuhifadhi) alipatwa na mkasa huo baada ya kugombwa na mama yake mzazi.

Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa manane kuamkia jana Jumapili Novemba 25.
Mwanafunzi huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Chake Chake Pemba, akipatiwa matibabu na hali yake inasemekana kuwa bado mbaya kutokana na kuungua vibaya maeneo takriban yote ya mwili wake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Saleh Mohammed, alisema kuwa chanzo cha tukio hilo, ni mtoto huyo kukutwa akiwa na mtoto wa kiume.

Kaimu Kamanda huyo aliwataka Wazazi kutumia lugha nzuri wanapozungumza na watoto wao ili kuwaepusha kuchukua ghadhabu za ghafla ambazo hatimae hazitomuathiri yeye peke yake bali na familia nzima.

Alifahamisha kuwa mtoto huyo baada ya kugombwa na mama yake ndipo alipoamua kuchukua uamuzi huo mbaya ambapo majirani ndio waliofanikiwa kuokoa maisha yake kwa kumwagia maji.

Habari zaidi za tukio hilo zinatarajiwa kutolewa na madaktari ambao kwa sasa wanahangaikia hali yake inayotajwa kuwa ni mbaya.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.