Na Khamis Mohammed
MTAKWIMU Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Mohammed Hafidh, amesema Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine za ukanda wa Afrika Mashariki, bado inakabiliwa na changamoto ya utoaji wa takwimu za kijinsia.
Hayo aliyaeleza wakati wa maadhimisho ya siku ya takwimu Afrika, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazimmoja mjini hapa.
Hafidh, alisema, takwimu nyingi zinazotolewa zikiwemo tafiti za kitaifa mfano, utafiti wa mapato na matumizi, utafiti wa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi, sensa ya kilimo na nyenginezo bado, zinaonesha tofauti ya mgawanyo wa kijinsi badala ya uchambuzi wa kina kuonesha tofauti ya kijinsia.
Alisema, ili kukabiliana na changamoto hiyo, jitihada za makusudi zinahitajika, ikiwemo kuingiza masuali katika utayarishaji wa miongozo ya kukusanyia takwimu itayotoa uchambuzi wa kina kuhusu jinsia.
Aidha, alisema, changamoto nyengine ni matumizi madogo ya takwimu zinazotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ambapo ripoti nyingi zinazotolewa na taasisi husika hazitumii taarifa za kitakwimu kama uthibitisho kutokana na uelewa mdogo wa matumizi ya takwimu.
Mtakwimu huyo, alisema, matatizo ya kufikisha uwasilishaji wa matokeo ya tafiti zinazofanywa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali hadi katika ngazi za chini kunatokana na ufinyu wa bajeti na hiyo inasababisha matumizi ya takwimu kubakia katika ngazi za juu tu.
Hivyo, alisema, ukusanyaji wa takwimu za kijinsia, ni muhimu kwa matokeo mazuri ya maendeleo ya nchi katika kuhusisha tofauti ya usawa kati ya mwanamke na mwanamme na musuala ya kumuwezesha mwanamke katika nyanja zote za mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema, kauli mbiu hiyo inatoa fursa kwa watunga sera kutambua vyema musuala ya kijinsia na kusimamia utengenezaji wa mfumo wa takwimu za kijinsia kitaifa, ufuatiliaji na ukusanyaji wa takwimu kwa uchambuzi na usambazaji wa taarifa.
Mtakwimu huyo wa Serikali, alisema, umuhimu wa jinsia umekubalika na kutumika katika shughuli mbalimbali za kitakwimu na programu za maendeleo ya taifa ikiwemo Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).
Alisema, makisio ya idadi ya watu kwa Zanzibar kwa mwaka 2011 ni milioni 1.2 ambapo kati ya hao asilimia 51 ni wanawake.
Hafidh, alisema,taarifa hiyo ni muhimu katika utayarishaji wa sera na mipango ambayo itanufaisha mwanamke na mwanamme kwa kuzingatia jinsia zao.
Alisema, kuna haja ya kuchukua juhudi maalum za kuingiza masuala ya kijnsia katika mfumo maalum wa ukusanyaji wa takwimu zinazotokana na taarifa za uhakika zilizopatikana kwa malengo yanayowezekana kuwa na uzito na umuhimu kwa jinsi moja na nyengine, na kupata taarifa sahihi ambazo sera na mipango inaweza kuwa na matokeo tofauti kati ya wanawake na wanaume, hivyo ni lazima taarifa za kijinsia ziangaliwe kwa mwanamke na mwanamme tofauti.
Alisema, mgawanyo wa idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi zinapishana katika nchi za Afrika zikiwemo nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki ambapo takwimu zinaonesha kuwa Kenya ina wabunge asilimia 10, Tanzania asilimia 30, Uganda asilimia 35, Burundi asilimia 36 na Rwanda asilimia 56.
Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la Wawakilishi lina takriban ya asilimia 30 ya wawakilishi wanawake, kati yao ni wale wa viti maalum na wagombea wa majimbo.
Alisema, nchi nyingi za Afrika zikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepiga hatua kimaendeleo katika ukusanyaji wa takwimu za kijinsia katika nyanja za elimu na afya, bado masuala mengi ya kijinsia yanahitajika kufanyiwa kazi ikiwemo muda unaotumika , udhalilishaji dhidi ya wanawake na mengine kama hayo,hiyo inaonesha pengo kubwa lililopo katika mfumo wa kitakwimu na changamoto kubwa ya muongozo au mpango usio na usawa wa mgawanyo wa rasilimali zilizopo.
Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika hufanyika kila ifikapo Novemba 18 ya kila mwaka ambapo kwa Tanzania maadhimisho hayo kitaifa yalifanyika jana.
No comments:
Post a Comment