Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi wote kuitumia fursa ya kupata vitambulisho vya Taifa kwani ni haki yao ya kikatiba na kuwasihi waachane na propaganda za baadhi ya watu za kuhusishwa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa na utashi wa kisiasa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi, viliopo Chukwani Mjini wa Zanzibar. Katika Sherehe za utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alirejea kauli yake ya kuwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vitaendelea kuwepo na kutumika kwa madhumuni yaliokusudiwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema kuwa uzoefu wa makosa yaliyotokea wakati wa usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi utumike ili kuondoa kasoro na matokeo yatakayoathiri kupatikana ufanisi katika kuendesha zoezi hilo la Vitambulisho vya Taifa.
Alieleza kuwa kuwepo kwa vitambulisho vya Taifa, kutaisaidia Serikali katika kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yake na hivyo kuweza kuziimarisha huduma za kijamii, kama vile elimu, afya na upatikanaji wa maji safi na salama.
Aidha, alisisitiza kuwa mapato hayo yatasaidia kuimarisha miundombinu ya barabaram huduma za umeme na pia, kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao kadhalika itakuwa ni rahisi katika kukabiliana na tatizo la wafanyakazi hewa jambo ambalo hupelekea serikali kupoteza fedha nyingi.
Dk. Shein aliwakumbusha watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuendeleza umakini na uadilifu walio nao, kwa kutambua dhamana kubwa waliyonayo kwa niaba ya Watanzania.
“Kazi yenu inahitaji uzalendo, ustahamilivu na kuweka mbele maslahi ya nchi badala ya maslahi binafsi, jambo ambalo sina shaka mnalielewa vyema na mtalitekeleza, lakini ni wajibu kukumbushana kwani, tunaambiwa kuwa ukumbusho huwafaa walioamini”alisema Dk. Shein.
Aidha, kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa wananchi wake hawana budi kuzingatia kuwa kutokana na nchi yenyewe ni ya visiwa haiwezi kuhimili ongezeko lkubwa la watu kutokana na rasilimali zilizopo hasa rasilimali ya ardhi.
Hivyo, alisisitiza kuwa NIDA haina budi kuhakikisha kuwa vitambulisho vinavyotolewa ni kwa ajili ya wale wenye haki ya kupatiwa vitambulisho hivyo ambao ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, Dk. Shein aliwahimiza viongozi wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini pamoja na vyombo vya habari kuunga mkono jitihada za Serikali katika zoezi hili kwa kuhakikisha kuwa wanawapa wananchi elimu ya kutosha juu ya zoezi hilo pamoja na umuhimu wake.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kulifanikisha jambo hilo la kihistoria, Mkurugenzi wa NIDA na wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo kwa jitihada zao na ushirikiano wao hadi yakapatikana mafanikio hayo.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima alieleza kuwa umuhimu wa kuwa na vitambulisho vya Taifa ni jambo la msingi ambalo litaweza kuwa na manufaa makubwa kwa kuunganisha mifumo mikubwa ya Usajili ya Kitaifa.
Alisema kuwa pamoja na kufanikiwa kufikia hatua ya kuanza kuwa na vitambulisho vya Taifa, mradi huo unakabiliwa na changamoto kubwa ambayo ni upatikanaji wa fedha za kuendeshea mradi, ikitiliwa maanani kuwa zoezi hilolinatakiwa kuhusushwa pia na Daftari la kudumu la wapiga kura, kwa madhumuni ya vitambulisho kutumika katika kura ya maoni ya katiba mwaka 2014, pamoja na kusaidia katika uchaguzi mkuu 2015.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Taifa, Bwana Dickson Maimu alisema kuwa NIDA itaendelea na utoaji wa vitambulisho kwa watu wote waliosajiliwa na kuchukuliwa alama za vidole, picha na saini kulingana na ratiba ya utekelezaji wa zoezi la usajili na utambuzi wa watu kitaifa itatolewa kwa umma hapo baadae.
Katika sherehe hizo, Rais Dk. Shein alikabidhiwa kitambulisho chake na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais, nae alikabidhiwa chake na Dk. Shein. Baada ya hapo Dk. Shein aliwakabidhi vitambulisho vyao watu mbali mbali katika makundi tofauti kutoka Bara na Zanzibar akiwemo Mama Maria Nyerere, Mkuu wa Majenshi ya Ulinzi na Usalama Davis Mwamunyange, Wawakilishi, viongozi wa dini, wastaafu, wenye ulemavu, wake wa viongozi na wengineo.
Utoaji wa vitambulisho vya Taifa awamu ya kwanza ni tukio ambalo lilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete mnamo Februari 7 mwaka huu huko katika viwanja vya Karimjee mjini Dar-es Salam.
No comments:
Post a Comment