Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na Balozi wa
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Tanzania,Mallallah Mubarak Alameri na
kueleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kihistoria
kati yake na Umoja huo.
Katika mazungumzo hayo
yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Dk. Shein alisema Zanzibar na UAE zimekuwa
na mahusiano na mashirikiano ya muda mrefu ambayo yameweza kuimarika siku hadi
siku katika nyanja mbali mbali za maendeleo.
Dk. Shein, alimueleza Balozi
huyo ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kuaga, kuwa kutokana na uhusiano na
mashirikiano hayo kukua ipo haja ya kukuza mashirikiano katika sekta za
maendeleo na hatimae kupata mafanikio kwa pande zote mbili.
Dk. Shein alisema juhudi za
makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuimarisha sekta za
maendeleo ikiwemo sekta ya uwekezaji ambapo nchi za umoja huo zimeweza kuonesha mwelekeo mkubwa wa kuwekeza katika
sekta ya utalii.
Kwa upande wa sekta ya afya, Dk. Shein
alieleza hatua kadhaa zinazochukuliwa na nchi za Umoja huo katika kuiunga mkono
Zanzibar kuimarisha sekta ya afya, juhudi ambazo zimeweza kusaidia kwa kiasi
kikubwa sekta hiyo.
Akieleza kuhusu sekta ya
biashara, Dk. Shein alieleza pamekuwa na uhusiano mwema kati ya Zanzibar na UAE
katika kuendeleza sekta hiyo ambayo ni muhimu katika kuimarisha uchumi ambpo
pia, aliushukuru mfuko wa Abudhabi kwa kusaidia upatikanaji wa maji safi na
salama katika baadhi ya maeneo nchini.
Alitoa pongezi za pekee kwa
viongozi wa Umoja huo kwa juhudi zao za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na
kuzidisha uhusiano na ushirikiano uliopo zikiwemo baadhi ya nchi za umoja huo
ambazo alifanya ziara hapo Novemba mwaka 2011.
Dk. Shein alimueleza Balozi
huyo kuwepo kwa Kamati ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Zanzibar na
Ras-Al-Khaiman kwa ajili ya kuendeleza mashirikiano katika nyanja hizo pamoja
na miradi na shughuli mbali mbali zilizokubalika kutokana na utiaji saini
waraka wa makubaliano kati ya pande mbili hizo.
Nae Balozi Mallallah, alitoa
shukurani kwa viongozi na wananchi wa Zanzibar kwa mashirikiano makubwa
waliyompa wakati akiwa nchini.
Alisema wananchi wa UAE na
wale wa Zanzibar ni ndugu na wana uhusiano wa muda mrefu na mashirikiano katika
nyanja mbali mbali za kimaendeleo ambazo aliahidi kuendelea kuimarishwa na
umoja huo kwa manufaa ya wote.
Pamoja na hayo, Balozi
Mallallah alimuahidi Dk. Shein kuwa umoja huo utaendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuimarisha sekta zake za maendeleo huku akisisitiza kuwa sekta ya
uwekezaji hasa katika sekta ya utalii litapewa kipaumbele na Umoja huo.
Alisema UAE inathamini
uhusiano na ushirikiano uliopo na kueleza kuwa miradi mbali mbali ambayo
iliahidiwa kuanza ukiwemo kuanza safari kwa ndege za Shrika la Emirate, suala
hilo linafanyiwa kazi.
Wakati huo huo, Dk. Shein
alifanya mazungumzo na Balozi wa Msumbuji nchini Tanzania,Dk. Vicente Mebunia
Veloso na kumueleza haja kwa nchi mbili hizo kuimarisha mashirikiano katika
sekta ya kilimo, biashara, usafiri na usafirishaji.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alimueleza Balozi Veloso kuwa ipo haja kwa Zanzibar na Msumbiji
zikaimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuendeleza sekta ya kilimo kwani ni kata muhimu katika maendeleo ya nchini.
Kwa upande wa biashara, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo kuwa umefika wakati kwa wafanyabiasahara wa
Msumbiji kushirikiana na wafanyabiashara wa Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
biashara kwa pande zote mbili.
Alisisitiza haja ya kuwepo
kwa mashirikiano katika usafiri wa angani na kueleza haja kwa Shirika la ndege
la nchi hiyo kufanya safari zake moja kwa moja Zanzibar hatua ambayo
itaimarisha sekta utalii.
Kuhusu
usafiri wa majini, Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuwepo mashirikiano
katika sekta hiyo hali ambayo itasaidia kusafirisha bidhaa mbali mbali pamoja
na wananchi katika nchi mbili hizo hatua ambayo inahitaji zaidi kuwepo kwa meli
kubwa za usafiri.
Nae Balozi huyo mpya wa
Msumbiji alimueleza Dk. Shein kuwa nchi
yake inathamini uhusiano na mashirikiano ya muda mrefu yaliopo kati ya nchi
mbili hizo ikiwa ni pamoja na kutambua juhudi za ukombozi zilizochukuliwa na Tanzania.
No comments:
Post a Comment