Habari za Punde

Uholanzi yaipatia Z’bar 19.2b/- kusaidia huduma za mama wajazito, watoto


Na Madina Issa
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Uholanzi zimetiliana saini mkataba wa mradi wa kuimarisha afya ya mama wajawazito na  watoto katika hospitali kuu ya Mnazimmoja pamoja na hospitali za wilaya 21 Unguja na Pemba.

Utiaji saini msaada huo ulifanyika katika ofisi ya Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo ambapo kwa upande wa Zanzibar iliwakilishwa na  Katibu Mku wizara hiyo, Khamis Mussa Omar na Balozi wa Uholanzi nchini Dk. Ad Koekkoek aliiwakilisha nchi yake.

Katika mkataba huo, Uholanzi itaipatia Zanzibar shilingi bilioni 19.2 kutekeleza mradi huo.

Katibu Mkuu Mussa, alisema msaada huo unakwenda sambamba na kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA II) pamoja na malengo ya maendeleo ya milenia.


Alisema msaada huo unalenga kusaidia uimarishaji huduma za mama na watoto Zanzibar na inajumuisha utanuzi wa majengo ya hospitali kuu ya Mnazimmoja utakaohusisha jengo lililokusudiwa kuwa kiwanda cha dawa liliopo karibu na hospitalI hiyo.

Aidha alisema pia utashughulikia ujenzi wodi mpya ya wazazi, idara ya kupokelea wagonjwa wa kawaida na waliopata ajali pamoja na kutanua wodi ya wazazi na watoto zilizopo sasa.

Maeneo mengine yatakayonufaika ni kuimarisha, kutengeneza na kujenga hospitali za 21 za wilaya  na kuwekwa vifaa muhimu vitakavyowezesha kutoa huduma bora kwa mama na watoto.

Mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka minane.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.