Na Asya Hassan
WAKATI Waziri
Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda akiunda Tume kuchunguza sababu ya wanafunzi
kufeli katika mitihadi ya kidato cha nne, kwa upande wa Zanzibar wadau wa elimu
wametoa maoni tafauti kuhusu matokeo hayo.
Wakizungumza na
mwandishi wa habari hizi, walidai hao walitaja sababu nyingi zilizochangia
wanafunzi kufeli, ikiwemo wanafunzi kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi,
starehe, wazazi kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao na walimu
kutokuwajibika ipasavyo kutokana na madai ya kiwango kidogo cha mishahara
wanacholipwa, mbali ya Serikali kuwaongezea mishahara kwa kiwango kikubwa
karibu miaka miwili sasa.
Walisema
mahusiano ya kimapenzi yameliathiri kundi kubwa la wanafunzi hasa wanaosoma
katika skuli za mijini.
Walisema hali
hiyo imewafanya wanafunzi kuchanganya mapenzi na masomo kwa wakati mmoja.
Aidha walisema
kushushwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya kidato cha pili kunasababisha
wanafunzi wengi kufaulu kidato cha tatu, ingawa hawana uwezo wa kufaulu hali
inayowafanya pia kukosa uwezo wa kufanya mitihani ya kidato cha nne.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama
cha Walimu Zanzibar (ZATU) Salim Ali Salim, alisema mitihani ya kidato cha nne
inafanywa wakati wanafunzi wakiwa hawajawa tayari kufanya mitihani hiyo.
Lakini pia alisema wana
uwezo mdogo sana wa kuukabili mtihani huo kwa sababu wizara ya elimu haina
kiwango maalum cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha pili.
Kwa mfano alisema, wizara
imekuwa ikiwachukua wanafunzi ambao wamefaulu kwa kiwango cha chini sana cha
asilimia 29 kujiunga na kidato cha tatu, kiwango ambacho hakiwezi kumuwezesha
mwanafunzi huyo kufaulu katika mitihani ya kidato cha nne.
Alisema ili kuweza kuziba
mapango ya kufeli kwa wanafunzi hao ni vyema kwa serikali kuongeza bajeti ili
wizara ya elimu iweze kufanya utafiti wa kutosha juu ya elimu na kuweza kujua
kwa kina sababu halisi inayopelekea wanafunzi hao kufeli.
Aidha alisema pia
inawezekana walimu walichangia wanafunzi hao kufeli, lakini alidai sababu kubwa
ni mishahara midogo wanayolipwa walimu hao.
Nae Msaidizi wa Mwalimu mkuu
wa skuli ya Mwembeladu, Salma Nassor ambae wanafunzi 565 wa skuli yake wamepata
daraja sifuri, alisema matokeo hayo mabaya yamesababishwa na wanafunzi
kushindwa kuwasikiliza walimu wao wawapo madarasani na badala yake kukimbilia
kutafuta masomo ya ziada (tuition) ambazo walimu wake hawafahamu mbinu za kujibia
masuali ya mitihani ya kitaifa.
Nae mwalimu wa skuli hiyo
Ali Idd Hamad alisema, walimu wamekuwa wakifuata mtaala, lakini uwezo wa
wanafunzi ni mdogo mno na kama mabadiliko hayatafanywa hawezi kufaulu.
Aidha alisema walimu
wamekuwa na mzigo mkubwa wa vipindi na idadi kubwa ya wanafunzi ndani ya darasa
moja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh, alipotakiwa kueleza kuhusu matokeo
hayo alisema, wizara bado haijakaa kujadili suala hilo.
Miaka miwili iliyopita
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliongeza mishahara ya walimu kwa asilimia
kubwa ili kuwafanya walimu kubakia nchini na kuondokana na mtindo wa kukimbia
kufanya kazi nje kufuata malipo makubwa.
No comments:
Post a Comment