Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akipokea maandamano ya wanafunzi hawapo pichani waliomaliza mafunzo yao katika ngazi ya msingi, cheti na Stashahada katika chuo cha Utawala Umma Zanzibar hapo tunguu.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa umma na Utawala Bora Mh. Haji Omar Kheri na kushoto yake ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Maalim Abdulla Suleiman.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimzawadia Mwanafunzi bora zaidi Iddi Muhsin Bakar kati ya wanafunzi 25 waliofanya vizuri katika mafunzo yao ya Stashahada katika chuo cha Utawala Bora Tunguu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpatia zawadi Maalum Mwafunzi Maryam Hassan Vuai ambae ni mlemavu kwa moyo wake wa kukamilisha ndoto yake ya kujipatia stashahada katika fani ya Rasilmali Watu kwenye mahafali ya tano ya chuo cha Utawala Bora Tunguu.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisisitiza utumishi bora katika mahafali ya tano kwa wahitimu waliomaliza mafunzo yao katika chuo cha Utawala Bora Tunguu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika picha ya pamoja na uongozi wa chuo cha Utawala Bora mara baada ya kukamilika kwa mahafali ya tano ya chuo hicho hapo Tunguu.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri anayesimamia Utumishi wa Umma na Utawala BoraMh. Haji Omar Kheir, Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala Bora Bibi Arusi Masheko na Mkuu wa Wilaya ya Kati ambae ndie mwenyeji Nd. Vuai Mwinyi.
Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara inayosimamia Utumishi na Utawala Bora Nd. Joseph Meza, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala Bora Maalim Abdulla Suleiman na Mjumbe wa Baraza hilo Nd. Mohd Fakih Mohd.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema usimamizi uliobora na utekelezaji wenye ufanisi wa mipango ya Serikali hupatikana kutokana na taaluma bora wanayopewa watumishi wa umma.
Alisema maendeleo ya nchi yanategemea watumishi wa umma waliopikwa vizuri kitaaluma ambayo inayokwenda sambamba na mabadiliko ya wakati hasa yale ya karne hii ya Sayansi na teknolojia.
Akizungumza katika Mahafali ya Tano ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar hapo katika Viwanja vya majengo yake Mapya yaliyopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema mtumishi wa umma ndie msimamizi na mtekelezaji wa mipango sahihi ya Serikali.
Balozi Seif alisemaipo haja kwa chuo cha Utawala wa Umma kutilia mkazo mafunzo mafupi ya kuwajengea uwezo watumishi na watendaji tofauti ili wafanye kazi zao za kutoa huduma kwa ufanisi unaokubalika na jamii.
“ Kwa vile chuo hichi kina dhima ya kuleta mabadiliko na mageuzi ya utumishi wa umma, si vibaya mkatumia uwezo wa vyuo vya nchi tofauti ili kuona jinsi wanavyoendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo na kukuza maadili ya watumishi”. Alisisitiza Balozi Seif.
“ Wenzetu hawa wa vyuo vya nje tayari wameshapiga hatua kubwa katika mageuzi ya utumishi , hivyo hatuna budi nasi kujifunza kutoka kwao”. Aliongeza kusisitiza zaidi Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikiomba chuo hicho kusaidia katika upandaji wa fikra mpya kwa umma jinsi ya kuwahudumia wananchi wanapohitaji huduma kutoka kwa watumishi wa Umma.
Alisema wananchi wanapohitaji huduma hizo ni vyema kwa watumishi hao wakaelewa kwamba wananchi hao ndio waliosababisha uwepo wao kutokana na kodi wanazolipa.
Akizungumzia suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema utendaji kazi katika sekta za umma hauko kwenye kiwango kinachokubalika.
Alisema tabia hiyo inayochangia kuzorotesha ufanisi wa kazi inakwenda sambamba na kuporomoka kwa maadili ya kazi pamoja na kukithiri kwa wizi katika taasisi kadhaa za umma.
Balozi Seif alishauri elimu ya sasa ya utumishi iweke mkazo wa kuendesha Taasisi na Idara za umma kama zinavyoendeshwa katika Taasisi Binafsi kwa kuheshimu uwajibikaji na udhibiti madhubuti wa matumizi ya fedha.
“ Moja kati ya sifa kubwa ya sekta binafsi ambayo wengi wetu tunaielewa ni udhibiti madhubuti wa matumizi ya fedha. Sasa sekta binafsi isipofanywa hivyo maana yake ni kufilisika kunakopelekea Taasisi kushindwa kutoa huduma. Kwa bahati mbaya mwamko kama huo haupo katika sekta za umma hapa Nchini”. Aliasa Balozi Seif.
Aliupongeza Uongozi pamoja na Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma kwa juhudi zao za maandalizi ya mahafali hayo ya tano ambayo ni ya kihistoria kwa vile kwa mara ya kwanza yamefanyika katika jengo lao jipya liliopo Tunguu.
Halkadhalika Balozi Seifalitoa pongezi maalum kwa mwanafunzi Maryam Hassan Vuai ambae ni mlemavu wa viungo kwa moyo wake wa kujiendeleza uliomuwezesha kukamilisha ndoto yake na kumaliza mafunzo ya Rasilimali watu katika ngazi ya Stashahada chuoni hapo.
Katika risala yao wahitimu hao wa chuo cha Utawala wa Umma wameelezea faraja yao kutokana na jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali kupitia wizara inayosimamia Utumishi wa Umma kwa kujenga jengo la kudumu la chuo hicho.
Walisema ujenzi huo umesaidia kuondosha kero na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wanafunzi hao kwa kipindi kirefu hali ambayo ilikuwa ikiwakosesha utulivu wa mafunzo kutokana na ukosefu wa sehemu ya uhakika ya kupata taaluma.
Walisema licha ya hatua nzuri ya upatikanaji wa jengo hilo na uhaba wa vifaa na changamoto nyengine zinazoendelea kukikabili chuo hicho, lakini wameiomba Serikali kupitia chuo hicho kufikiria uamuzi wa kuanzisha mafunzo ya shahada ya kwanza hapa Zanzibar kwa vile vijana wengi wenye sifa za kujiunga na kiwango cha elimu hiyo wapo wa kutosha.
Mapema Mkurugenzi wa chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar Bibi Arusi Masheko alisema jumla ya wahitimu elfu 1455 wa fani tofauti katika ngazi ya Msingi, Cheti na Stashahada wamekamilisha mafunzo yao na kufanikiwa kupata vyeti na stashahada.
Bibi Arusi Masheko alifahamisha kwamba kati ya wahitimu hao wanafunzi 424 ni wa ngazi ya Msingi, 1312 ambao ndio wengi walikuwa ngazi ya Cheti na 190 wa ngazi ya Stashahada.
No comments:
Post a Comment