Na Shomari Hamad, Mafunzo
WANAMICHEZO wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar, wametakiwa kuzingatia nidhamu na haja ya kukuza udugu na timu za Magereza kutoka Tanzania Bara, wakati wote wa sherehe za Pasaka.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Khalifa Hassan Choum, katika kikao cha kuratibu mapokezi ya wageni wao na mashindano yatakayozikutanisha timu za pande mbili hizo wakati wa maadhimisho ya Pasaka.
Kamishna huyo amesema lengo la ziara hizo za kimichezo ni kuendeleza umoja, ushirikiano na mshikamano kati ya wananchi na wanamichezo wa Zanzibar na Tanzania Bara, hivyo ni vyema wakazingatia jambo hilo kwa kuonesha mchezo wa kiungwana.
Jumla ya wanamichezo 135 wa Jeshi la Magereza, ambao ni wageni wa Vyuo vya Mafunzo, wanatarajiwa kuwasili asubuhi ya Machi 29, mwaka huu ikiwemo timu ya soka, mpira wa wavu, mchezo wa bao na mingine mbalimbali ya ufukweni.
Ufunguzi wa mashindano kati ya timu hizo marafiki, unatarajiwa kuanzia saa 8:00 mchana katika viwanja vya Mafunzo Kilimani, ukitanguliwa na gwaride maalum, kabla ya mechi ya mpira wa wavu itakayochezwa saa 10:00 jioni.
Kwa mujibu wa ratiba, saa 2:30 usiku, kutakuwa na burudani ya ngoma za utamaduni zitakazoporomoshwa na wasanii wa Mafunzo katika ukumbi wao maarufu ‘Wajelajela’.
No comments:
Post a Comment