Na Salim Said Salim
WATU wengi wa Zanzibar walifuatilia kwa karibu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa
Kenya.
Kutokana na mazungumzo yao inaonekana wamejifunza mengi. Lakini sijui kama
wale ambao hawataki kujifunza wamekuwa tayari kubadilika.
Yapo mambo mengi yaliyowasababishia watu wa Visiwani kufanya hivyo, mojawapo
ni ujirani na uhusiano wa karibu walionao na watu wa Mombasa, eneo ambalo zamani
lilikuwa sehemu ya Zanzibar, lakini chini ya himaya ya Serikali ya Ungereza.
Kubwa zaidi ni kwa sababu Kenya, kama Zanzibar, ilipata mtihani mkubwa tokea
kuachana na siasa za chama kimoja na kuja mfumo wa vyama vingi vya siasa miongo
miwili sasa.
Wakati chaguzi Zanzibar ziligharimu maisha na hasa katika mwaka 2001, Kenya
nayo ilikuwa na vurugu ulipofanyika uchaguzi wa mwaka 2007 na mamia ya watu
kuuawa na kupata hasara kubwa za mali.
Wakati vurugu za Zanzibar zilisababisha mamia ya watu kuwa wakimbizi Mombasa,
Kenya na nchi nyingine, ikiwemo Somalia, zaidi ya Wakenya 600,000 walihama
sehemu walizozaliwa au kuishi kwa miaka mingi na kwenda kwengine kuanza maisha
mapya.
Hivi sasa baadhi ya viongozi wa Kenya wamefunguliwa mashitaka ya kuchochea
mauaji yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambayo baada ya
mvutano yalisababisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Tuombe Mungu na viongozi wetu na waandishi wa habari wasijisahau hata
kulazimika jumuiya ya kimataifa kuwawajibisha kisheria.
Nayo Zanzibar, labda kwa kujifunza kutokana na balaa za uchaguzi
walizokumbana nazo na yaliyotokea Kenya, nayo ilipata mwafaka uliosababisha
kufanyika uchaguzi wa amani mwaka 2010 na baadaye kuundwa serikali ya umoja wa
kitaifa.
Kwa bahati mbaya inaonekana wapo ambao hawakufurahia hili na tayari
panasikika na kuonekana chokochoko za kuleta balaa.
Badala yake ni viongozi wa Uamsho tu ndio unaosikia wanachunguzwa na polisi,
lakini hatuelezwi kinachoendelea juu ya vikaratasi vya uchochezi na matusi
yaliyoporomoshwa kwa marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume.
Sijui viongozi waliopo madarkani hivi sasa (Bara na Visiwani) watahisi vipi na
wao wakija kukashifiwa katika vikaratasi watakapoachia ngazi za uongozi.
Sasa Kenya baada ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa imefanya uchaguzi
ambao nao umekuwa na shaka kutokana na kuwepo kwa madai ya mizengwe wakati wa
kuhesabu kura.
Hata hivyo, watu wake wamekataa uchaguzi kuwarudisha kwenye vurugu za kutoana
roho. Badala yake malalamiko ya uchaguzi yamepelekwa mahakamani kwa sababu
sheria ya uchaguzi inatoa fursa hiyo, tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo uamuzi
wa tume ni wa mwisho na hauwezi kupelekwa mahakamani.
Hili ni eneo ambalo Tanzania na hasa Zanzibar inafaa kuliona kama somo kwa
vile kutotoa nafasi kwa uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kuhojiwa si demokrasi bali ni
udikteta.
Lakini zuri zaidi ni kuwa kesi za uchaguzi, hasa ya kupinga matokeo ya
uchaguzi wa rais zitasikilizwa katika kipindi cha sio zaidi ya wiki mbili tokea
matokeo kutolewa.
Vilevile kesi zote zinazohusu uchaguzi zitasikilizwa hata siku za mapumziko
na hadi usiku.
Hapa kwetu na hasa Zanzibar kesi za uchaguzi hupigwa tarehe kutoka uchaguzi
mmoja hadi ufikie mwengine.
Hii si demokrasia wala utawala bora. Ni vizuri tukajifunza kutoka Kenya.
Uchaguzi uliopita wa Kenya ulikumbana na matatizo ya kiufundi ya teknolojia,
lakini palikuwepo uwazi wa kiasi fulani na wananchi kuelewa kilichokuwa
kikiendelea, tofauti na Zanzibar ambapo ukimya hutanda na kusababisha kuwepo
kila aina ya uvumi.
Ukweli ni kwamba Kenya imefanya marekebisho makubwa katika kuendesha
uchaguzi, ijapokuwa bado inayo safari ndefu.
Hapakuwa na malalamiko ya watu wengi kunyimwa haki ya kupiga kura kama
inavyoendelea kuonekana Zanzibar na wala hazikusikika habari za wapiga kura
mamluki kupelekwa vituoni.
Kenya ilikwenda hatua moja mbele zaidi ya hata kuwa na Jimbo la Uchaguzi wa
Rais kwa raia zake wanaoishi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hii ni tofauti na Zanzibar ambapo watu zaidi ya 40,000 walinyimwa haki hiyo
licha ya sio tu kuzaliwa Zanzibar, bali wengine wakiwa hawajawahi hata kusafiri
nje ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika uchaguzi wa Kenya maofisa wa uchaguzi ndio waliokuwa wakifanya uamuzi
katika vituo vya kupiga kura, tofauti na Zanzibar ambapo masheha ndio wenye
uamuzi wa nani awe na haki ya kupiga kura.
Hawa masheha wamelaumiwa sana, hata na wachunguzi wa uchaguzi wa ndani na
nje, kuwa ndio waliokuwa tatizo na kuwa chanzo cha vurugu.
Baadhi yao bila ya aibu wamekuwa wakidai hawawajui watu wanaoishi mitaani
kwao na hata vijana waliowaozesha binti zao. Ni watu wanafiki kwa kiwango
ambacho hakielezeki.
Kinachosikitisha ni kwamba hakuna hata sheha mmoja aliyechukuliwa hatua za
kisheria kwa kusema uongo na hapakuwepo taarifa ya kufanyika uchunguzi juu ya
madai kuwa baadhi ya masheha walitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa
uchaguzi.
Badala yake tuliona mamia ya watu wakifunguliwa mashitaka bandia, ikiwa hata
vizee kudaiwa kuwanyang’anya silaha polisi.
Askari wa Jeshi la Polisi Kenya walionekana kila pembe, lakini walikuwa
hawaingilii shughuli za uchaguzi au kutisha wananchi.
Katika chaguzi za Zanzibar, askari wa SMZ walikuwa ndani ya vyumba vya
kupigia kura kama vile wao ni makarani wa Tume ya Uchaguzi.
Nimeyaona hayo Unguja na Pemba na nilipowauliza maofisa wa Tume ya Uchaguzi
walinieleza ati wanalinda usalama.
Wagombea nao walionesha uungwana wa hali ya juu kwa kila mmoja kuweka
uzalendo mbele na sio utashi wa kisiasa licha ya kutoridhika na baadhi ya
matokeo, kama madai kuwa baadhi ya vituo vilipokea wapiga kura masaa kadha baada
ya muda unaoruhusiwa kwa mpiga kura kufika kituoni.
Kwa upande mwingine, vyombo vya habari vya Kenya, hata vile vya umma,
havikuonyesha utashi mkubwa wa kisiasa kama unavyoonekana katika chaguzi za
Zanzibar.
Jingine ambalo Zanzibar inapaswa kujifunza ni kwamba uchaguzi ulikuwa wa watu
wazima, wale waliofikia umri wa miaka 18 na kuendelea, wakati Zanzibar watoto
ambao umri wao hauwaruhusu kuwa wapiga kura walishiriki.
Moja ya kambi maarufu iliyotumika kufanya mizengwe ni katika jengo lililokuwa
kiwanda cha viatu hapo Mtoni, mjini Unguja.
Nani aliwakusanya watoto hao na walitoka wapi wanajuwa hao waliofanya hayo,
lakini ukweli ni kwamba walikuwepo hapo na walipoulizwa na waandishi wa habari
walikuwepo hapo kufanya nini jawabu yao ilikuwa waliwekwa hapo ili wapige
kura.
Nilipowauliza walitokea wapi waliniambia wengi wao walitoka Kunduchi, Kawe na
maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Wapo watu ambao huwa wanachukia haya yakielezwa eti kwa madai anayefanya
hivyo anatonesha vidonda, lakini ukweli ni kwamba uchafu huu umefanyika na kama
walikuwa hawataki yazungumzwe basi wasingefanya madhambi haya.
Ukweli lazima usemwe na kurudiwa ili wasitoke tena vidudu mtu vya kutufanyia
manyago yatakayosababisha Zanzibar kurejea katika mizengwe ya uchaguzi.
Wakati tunaelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ni vizuri kujifunza kwa
yaliyotokea siku za nyuma na mamia ya watu kuuawa, na hatua zilizochukuliwa na
Kenya katika uchaguzi wake ili kuinusuru Zanzibar na kuwapa watu wake nafasi ya
kusonga mbele.
Viongozi wa Zanzibar wanapaswa kuelewa kama wanakataa kujifunza na kushikilia
kwamba ushindi lazima, hata ikiwa kwa kufanya mizengwe, basi dunia itawafunza
baadhi ya wakati kwa njia ambazo zitawadhalilisha.
Tusisahau wazee walivyotuasa kwa hekima na busara kwa kutuambia: “Asiyefunzwa
na mamaye hufunzwa na ulimwengu.”
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment