Habari za Punde

Watoto Zanzibar wapewa chanjo


Na Asia Hassan
WAZIRI wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji ameelezea haja ya kulinda ukuaji wa watoto ambao ni tegemeo la maendeleo ya Taifa la baadae.

Alisema iwapo hakutakuwa na juhudi za kuwakinga watoto na maradhi hasa yanayowakumba katika umri mdogo maisha yao yako hatarini.

Alieleza hayo wakati akizindua chanjo mpya ya ugonjwa wa kuharisha, nemonia na uti wa mgongo inayotolewa kwa watoto kuanzia wiki sita katika hospitali ya Mnazimmoja.

“Taifa letu linategemea watoto kwa ajili ya kuliendeleza hapo baadae hivyo ni vyema tukaweka msisitizo katika kulinda afya zao na ukuaji wao,” alisema Duni.

Chanjo hiyo iliyoanza kutolewa katika vituo vya afya kwa wiki tatu sasa itasaidia kupunguza maradhi hayo ambayo yanachagia kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto nchini.

Aliwasisitiza wazazi kushirikiana na watendaji wa sekta ya afya ili kuhakikisha wanawalinda watoto na maradhi yanayohatarisha ukuaji wao.

Aidha aliwashukuru wafadhili mbalimbali wakiwemo UNICEF, Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Chanjo kwa ushirikiano wao katika kufanikisha utaoji wa chanjo hiyo kwa watoto.

Mratibu wa chanjo za mama na watoto Zanzibar, Yussuf Haji Makame alisema chanjo hizo zitatolewa kwa awamu mbili kwa watoto wenye umri kuanzia wiki sita hadi wiki kumi.

Alifahamisha kuwa maradhi hayo yalikuwa yanaongoza kuchangia vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano hivyo chanjo hiyo itasaidia kuvipunguza.

Alisema kwa sasa hakuna wananchi wanaohusisha chanjo zinazotolewa kwa watoto na imani za kishirikiana na badala yake wamekuwa na mwamko wa kuwapatia kinga watoto.

Kwa upande wake Mwakilishi mkaazi wa UNICEF Zanzibabr, Ruth Leano alisema shirika hilo limeunga mkono Zanzibar katika kufanikisha ustawi wa watoto nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.