Habari za Punde

Balozi Seif: Tuwe utamaduni wa kupima afya zetu

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kukizindua rasmi Kituo cha Afya cha Kijiji cha Bwagamoyo Piki Wilaya ya Wete ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50 sawa na Nusu Karne.

Daktari dhamana wa Wilaya ya Wete Dr. Fatma Khazal akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kukizindua kituo cha Afya cha Kijiji cha Bwagamoyo Piki wilaya ya Wete Pemba.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vifo vya ghafla vitaendelea kuikumba jamii kwa vile watu wengi hawajajipangia utamaduni  wa kupima afya zao kila baada ya kipindi.
 
Alisema tabia ya watu ya kuogopa kupima kwa kusubiriwa maradhi yajichomoze yenyewe mwilini mwa watu ni njia moja wapo ya kukaribisha vifo ambavyo vinaweza kuepukika.
 
Balozi Seif alisema hayo wakati akikizindua rasmi kituo cha Afya cha Kijiji cha Bwagamoyo Piki Wilaya ya Wete ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50 sawa na nusu Karne.
 
Alisema wakati Serikali ikiendelea kuimarisha miundo mbinu ya sekta ya Afya wananchi hawana budi kuvitumia vituo vya afya na kuwepuka utaratibu wa baadhi ya watu wanapopata maradhi kuwamua kutumia dawa bila ya ushauri wa Madaktari  na wengine kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.
 
“ Ukweli ilo wazi unaonyesha kwamba vituo vya afya mara nyingi husaidia kupunguza  kasi ya  wananchi kukimbilia kwenye dawa za asili zisizo na vipimo vyovyote vile ambapo matokeao yake huleta athari kwa watumiaji “. Alisema Balozi Seif.
 
Akizungumza upungufu wa Madaktari hapa Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Zanzibar inatarajiwa kuwa na idadi kubwa ya Wataalamu wa Afya  kutokana na Madaktari 38  wanaochukuwa  taaluma ya fani hiyo kutarajiwa kukamilisha mafunzo yao katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali yas Cuba zilifikia makubaliano ya kuanzisha chuo Maalum cha Madaktari Bingwa hapa Zanzibar ili kukabiliana na upungufu huo.
 
Balozi Seif aliwaasa Madaktari  wote wanaosomeshwa na Serikali kuendelea kuwa na moyo wa kizalendo kwa kubakia nyumbani ili lile lengo lililokusudiwa na Serikali la kuwasomesha madaktari hao na baadaye  kuwahudumia Wananchi wenzao liweze kufanikiwa.
 
Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar alieleza kwamba si vyema kwa madaktari hao kuwasaliti wananchi wao kwa kingizio cha mshahara mdogo usiokidhi mahitaji yao ya kimaisha.
 
Balozi Seif pia aliwatahadharisha watendaji wa sekta hiyo ya afya kuacha tabia ya kukimbia Kisiwa cha Pemba wakati wanaopangiwa kutoa huduma za afya Kisiwani humo kwani tabia hiyo haiwatendei haki wananchi wa visiwa hivyo.
 
“ Tumeshuhudia tabia ya baadhi ya watendaji wa afya wanapopangiwa kufanya kazi Pemba hutoa visingizo kadhaa ikiwemo suala la ndoa “. Alieleza Balozi Seif.
 
Akitoa Taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho cha Kijiji cha Bwagamoyo Piki Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji hicho Nd. Mussa Mohd Abdulla alisema wananchi wa kijiji hicho walilazimika kuunda kamati yao ili kuibua maendeleo katika kuanzisha miradi tofauti ya ustawi wa jamii.
 
Nd. Mussa alisema malengo yaliyodhamiriwa na wana kijiji hicho ikiwemo ujenzi wa skuli, huduma za maji safi na salama pamoja na kituocha cha afya kilichozinduliwa tayari yameshafikia asilimia 90%.
 
Aidha Katibu huyo wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Bwagamoyo Piki alizitaja changamoto zinazokikabili Kijiji hicho ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nyumba ya Daktari pamoja na uhaba wa maji uliosababishwa na ujenzi wa Bara bara.
 
Akitoa salamu  na kuwapa matumaini ya maendeleo zaidi Wananchi hao Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi  alisema Serikali ya Mkoa huo itahakikisha kwamba inasimamia kuondoa changa  moto zinazowakabili wananchi hao.
 
 
Mh. Dadi alisema changa moto ya maji safi na salama kwenye kijiji hicho yaliyopunguwa kasi yake kutokana na kuharibika kwa mikundo mbinu iliyosababishwa na ujenzi wa Bara bara iliyopita Kijijini hapo iko ndani ya uwezo wa Serikali ya Mkoa.
 
Mapema katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi alisema ujenzi wa kituo hicho cha afya cha Kijiji cha Bwagamoyo Piki umeifanya Wilaya ya Wete kuwa na vituo vya afya  vipatavyo 19.
 
Dr. Jidawi alisema hatua hiyo ambayo Jimbo la Mtambwe lina vituo vya afya Vinne imelifanya eneo hilo kuvuka lengo la Milenia la Shirika la Afya Ulimwenguni la kuagiza ujenzi wa vituo vya afya kila baada ya kilomita Tano.
 
Akizungumzia uhaba wa watendaji wa afya unaovikumba  vituo mbali mbali Nchini Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya alisema Wizara hiyo iko katika jitihada za kuwasomesha wataalamu wake ili kuondosha upungufu huo.
 
Kituo cha Afya cha Bwagamoyo Piki kinachotarajiwa kuwa na wafanyakazi 12 ambapo hadi hivi sasa wapo watatu kinatarajiwa kuwahudumia wananachi wapatao 3,317 wa Kijiji hicho pamoja na Vijiji jirani.
 
Takriban huduma zote za msingi za afya ikiwemo chanjo,,uzazi , elimu ya afya, ushauri nasaha zitatolewa katika kituo hicho kipya kilichogharimu ujenzi wake jumla ya shilingi Milioni 53,302,000/-.

1 comment:

  1. hakuna matata makau wa rais , tupatie hizo chenji za kwenda nje na sisi tukafanye kupimwa afya zetu kame vile nyie mnavyoenda kwa pesa zetu , kama kweli mnajivunia hivi vituo kwa nini nyinyi hampimwi hapa nchini mpaka mwende nje , jee huu ndio usawa wa binadamu ambao nyinyi wazalendo wa nchii huu huwa mnauhimiza? aaah wazalendo wetu hawa ......

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.