Habari za Punde

Dk Shein: Tujenge na kuuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Wanamichezo wa Vikundi vya Mazoezi ya Viungo katika Bonanza la 5,Vikundi vya mazoezi ya Viungo,lililofanyika katika Uwanja wa Amaan,Wilaya ya Mjini Unguja,katika shamra shamra za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]



STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                     01 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kujenga na kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao pamoja na kujikinga na maradhi yanayoweza kuepukika.

Dk. Shein ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa klabu za mazoezi na vyama vya michezo katika Bonanza Maalum la Mazoezi ya Viungo lililofanyika katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Kabla ya kuzungumza na wanamichezo hao Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi akiwa amefuatana na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na viongozi wengine walishiriki matembezi ikiwa ni sehemu ya Bonanza hilo yaliyoanzia Michenzani mjini Unguja hadi Uwanjani hapo.

Dk. Shein aliwaeleza washiriki kuwa ni jambo lililo dhahiri kuwa kufanya mazoezi ni jambo la msingi sana katika kuimarisha afya ya mwili na kuchangamsha akili hivyo Serikali ina kila sababu ya kuziunga mkono jitihada walizozianzisha za kuunda vikundi vya mazoezi.

Alifafanua kuwa hivi sasa kumekuwepo na maradhi mengi ambayo hapa kwetu yanaelezwa kusababishwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha na kuyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari na kuongezeka unene ambayo yanaweza kupunguza kwa kufanya mazoezi.


Hata hivyo pamoja na ukweli huo alibainisha kuwa kuimarika kwa huduma za afya na huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi kumerahisisha wananchi kugundua maradhi mengi kuliko iliyokuwa huko nyuma.  

Dk. Shein aliwahakikishia wanamichezo nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Saba itaendelea jitihada zilizoanzishwa na Serikali za awamu zilizopita kuimarisha michezo ikiwemo kuweka mazingira na miundombinu bora ya michezo.

Kwa hiyo aliwapongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kutekeleza maagizo yake kikamilifu ya kubadili haiba ya uwanja wa michezo vya Amaan Unguja kwa wakati pamoja na kualika timu za nje katika mashindano ya kikombe cha Mapinduzi mwaka huu.

Aliongeza katika kuimarisha michezo Serikali imeuwekea pia nyasi bandia uwanja wa Michezo wa Gombani Pemba na huduma nyingine ili kukidhi viwango vya kimataifa. Kuhusu uwanja wa Mao Dk. Shein alisema tayari Serikali imeshatiliana saini makubaliano na Serikali ya China kuujenga upya uwanja huo.

Sambamba na pongezi hizo alieleza kufurahishwa na Wizara hiyo kuhamasisha michezo mijini na vijijini huku akitolea mfano ushiriki wa vikundi kutoka sehemu zote za Zanzibar pamoja na Tanzania Bara katika Bonanza la mwaka huu.

Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameunga mkono tamko la Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo la kuifanya siku ya tarehe 01 Januari kila mwaka kuwa siku ya mazoezi kitaifa na ametaka maandalizi ya Bonanza hilo ambalo litakuwa la Sita yafanyike kwa umakini mkubwa.  

Akizungumza kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema Bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la kuitaka Wizara hiyo kurejesha hamasa ya wananchi kupenda nchini.

Kufuatia agizo hilo alibainisha Waziri huyo wa Michezo kuwa Serikali imeamua siku ya tarehe 01 Januari ya kila mwaka iwe siku ya mazoezi kitaifa ambapo kila mwananchi popote alipo nchini atashiriki mazoezi.

Aliongeza kuwa Bonanza hilo la Tano la Mazoezi ambalo limejumuisha vikundi vya mazoezi 65 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara badala ya 50 vilivyapangwa awali ni ishara ya wananchi kuitikia wito wa kufanya mazoezi pamoja na kuimarika uongozi wa ZABESA.

Kwa hiyo aliahidi kushirikisha vikundi kutoka sehemu nyingi zaidi ya nchi katika bonanza lijalo kuongeza hamasa na pia kuimarisha vikundi vya mazoezi.  
  
Kwa uapande wake Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar Sharifa Khamis alieleza kuwa Bonanza hilo ni uzinduzi wa Vuguvugu la Miaka 50 ya Mapinduzi kwa wanamichezo ambalo litaendelea hadi tarehe 13 Januari mashindano hayo yatakapofikia fainali.  

Amewashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha Bonanza hilo pamoja na michezo itakayofanyika wakati wa maadhimisho hayo. Amezitaja nchi za nje zilizoleta timu kuwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Zambia, Sudan Kusini na Ghana.

Katika  risala yao iliyosomwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Wafanya Mazoezi ya Viungo Zanzibar- ZABESA bibi Hawa Abdalla Mandred wanamazoezi hao waliiomba Serikali ifanye tathmini ya kiafya kwa wanamazoezi hao na Serikali kufanyia kazi matokeo ya tathmini yake kwa faida ya wanamazoezi na kwa Taifa kwa jumla.

Risala hiyo ilizidi kueleza kuwa wanamazoezi hivi sasa wanazidi kuhamasisha wananchi wengine zaidi kujiunga na vyama vya mazoezi na takwimu za kila mwaka zimekuwa zikionesha kuwa idadi ya vikundi na wanachama wa vyama vya hivyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka.

Sambamba na ongezeko hilo jambo muhimu la kutia moyo alisema Bi Hawa ni kuona kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanamazoezi wanawake tofauti na miaka mitano iliyopita lilipoanzishwa bonanza hilo.

Alisema ZABESA inaamini kuwa kazi hiyo ya kuhamasisha mazoezi inalisaidia Taifa kwa kuwa mazoezi hayo yanasaidia kuepusha maradhi yasiyo ya lazima na pia hata kutibu baadhi ya mardhi bila ya mwananchi kupaswa kweda hospitali hivyo kulipunguzia Taifa gharama za matibabu.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.