BAADA ya kupotea kwa miaka mingi, hatimaye ligi ya mpira
wa miguu kwa timu za wachezaji wanawake Zanzibar inatarajiwa kurudi viwanjani
leo.
Katiba wa soka la wanawake Zanzibar Laila Said,
amewaambia waandishi wa habari kuwa pazia la ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya
timu sita, litafunguliwa katika uwanja wa Amaan mnamo saa 10:00 jioni.
Alisema timu zinazotarajiwa kufungua dimba ni New
Generation Queens ya mtaa wa Kwahani, itakayorushana roho na Mwenge Sisters
kutoka Makunduchi.
Timu nyengine zinazoshiriki ligi hiyo ni Women Fighters,
Bungi Sisters, Kidimni Sisters pamoja na Mkoani Stars kutoka kisiwani Pemba,
ambayo hata hivyo haitakuwepo kwenye sherehe za ufunguzi kwa kuwa itachelewa
kufika Unguja.
Hata hivyo, Laila alisema mechi nyengine zote zitakuwa
zikichezwa uwanja wa Mao Tse Tung wakati wa saa 8:00 na saa 10:00 jioni.
Katika ligi hiyo iliyopangwa kumalizika Januari 26, mwaka
huu, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Asha Suleiman
Iddi.
No comments:
Post a Comment