Habari za Punde

Dk Shein : Sekta ya uvuvi kuimarishwa

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Pemba                                                                                                           5.1.2015

UJENZI  wa masoko mapya ya  kisasa ya samaki ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha sekta ya uvuvi na kuongeza tija sambamba na kuongeza soko la ajira kwa wananchi wake.
 
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kulizindua soko jipya la kisasa huko Tumbe, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
 
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema  kuwa ujenzi wa soko hilo utawanufaisha zaidi wavuvi wa Tumbe pamoja na maeneo mengine pamoja na kupanua soko la ajira kwa wakaazi wa Tumbe na vitongoji vyake ambapo hatua hiyo ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
 
Dk. Shein alisema kuwa kabla ya mwaka 1963 Zanzibar ilikuwa haijatawaliwa na ilikuwa na viongozi wake wa asli na ndipo baadae ukaja utawalakutoka Ureno na kufuatia Sultani kutoka Oman na kusisitiza kuwa hivi sasa Zanzibar iko huru na hakuna mtu yoyote wa kuja kuitawala tena Zanzibar.
 

Alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalileta uhuru na kuwafanya Wazanzibari waweze kujitawala wenyewe .
 
Dk. Shein alisema kuwa kila mvuvi ana haki ya kulitumia soko hilo na kuwataka wavuvi kuwa na subira na hamasa huku akiwataka kuwa na mashirikiano ya pamoja katika shughuli zao.
 
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alishangazwa na baadhi ya wavuvi wa eneo hilo la Tumbe ambao wameeleza nia yao ya kutolitumia soko hilo na kusisitiza kuwa hatua hiyo hawaikomoi Serikali na wanawakomoa ndugu zao wa Tumbe kwani wao ni wenyewe kwa wenyewe.
 
Alisema kuwa tayari serikali imeshafanya wajibu wake wa kuwapelekea wananchi wake huduama  muhimu ya kuwajengea soko la kisasa ambalo ni soko kubwa la samaki kuliko masoko yote ya Zanzibar.
 
" Wengi wape, kwani wengi wametaka kujengewa soko na serikali imefanya hivyo... leo Tumbe kuna soko kubwa kuliko masoko yote ya Zanzibar, hivyo ni vyema wazee mkazungumza na wavuvi hao  kwani mtihani wa kitendawili hicho ni lazima kiteguliwe na nyinyi wazee wa Tumbe.... kwani eneo hili lina wavuvi wengi wapatao 2000",alisema Dk. Shein.
 
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa soko hilo limejengwa ili kukidhi shughuli zote za kijamii zinazofanywa sokoni hapo ikiwa ni pamoja na sehemu za kuhifadhi samaki, sehemu ya mnada wa samaki, eneo la ukaaji wa dago, sehemu maalum ya mama lishe na sehemu ya kusalia.
 
Alieleza kuwa ujenzi wa soko hilo lililofunguliwa leo utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi ambapo mbali ya juhudi hizo serikali tayari imeshapeleka kijijini hapo umeme, maji safi na salama, skuli pamoja na  huduma nyengine muhimu za kimaendeleo.
 
Sambamba na hayo Dk. Shein alitoa pongezi kwa kijiji hicho kwa kuuunda Kamati ya kusimamia uendeshaji wa soko hilo na kusisitiza kuwa mbali ya shughuli hizo pia Kamati hiyo pia ishughulikie kazi za kiundendaji.
 
Pia, Dk. Shein alisisitiza azma ya Serikali ya kuwajengea uwezo wananchi kwa kutoa mafunzo ya ufugaji wa samaki pamoja na azma ya kuimarisha uvuvi wa bahari kuu huku akiahidi ombi la wanakijiji la kutaka barabara yao itiwe lami, umeme wa uhakika pamoja na kupatiwa boti na vifaa vyake.
 
Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mohammed Said Mohammed (Dimwa) alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kutambua umuhimu wake mkubwa katika maendeleo ya nchi na wananachi wake.
 
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Kassim Gharib Juma alisema kuwa sekta ya uvuvi imekuwa kwa asilimi 4.4 mwaka 2013 kutoka asilimia 2.3 mwaka 2012 na kueleza kuwa sekta hiyo imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
 
Alisema kuwa katika mwaka 2013 sekta hiyo ilichangia asilimia 7.2 ya pato la Taifa na kutoa ajira kwa wananchi wapatao 40,000 ambao wanajishughulisha moja kwa moja na shughuli za uvuvi.
 
Aidha, Dk. Gharib alisema kuwa sekta ya uvuvi hapa Zanzibar bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kutokana na fursa mbali mbali zilizopo ikiwa ni pamoja na uwezo wa kupanua uzalishaji wa samaki na mazao mengine ya bahari pamoja na kuwa na  maeneo ya uvuvi ambayo bado hayajafikiwa na shughuli za uvuvi.
 
Kwa maelezo ya Dk. Garib ujenzi wa soko hilo umegharimu shilingi milini 712,500,00 kupitia Mradi wa MACEMP ikiwa ni mkopo kwa Serikali kutoka Benki ya Dunia.
 
Nao wananchi katika risala yao walitoa pongezi zao kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein  kwa kuwajengea soko hilo na kueleza kuwa ujenzi wa soko hilo umekuja baada ya kuonekana umuhimy wa kuwepo kwake hasa kutokana na idadi kubwa ya wavuvi wenyeji na wageni katika vipindi tofauti vya msimu wa uvuvi.
 
Pamoja na hayo wananchi hao walieleza kuwa soko hilo ni kiunganaishi kikubwa kwa wananchi wa maaeneo ya karibu na hata wale wanaotoka maeneo ya mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba ambapo pia walieleza changamoto zinazowakabili.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.