Habari za Punde

Kichocho Kinaweza Kusababisha Saratani ya Machango.

Na Abdulla Ali - Maelezo 
Kichocho cha tumbo kinaweza kusababisha Saratani ya machango endapo mgonjwa hatotibiwa kwa wakati.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo wakati akijibu swali la mwakili wa Jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor Juma katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja, aliyetaka kujua ni lini Serikali itachukua hatua thabiti kwa ajili ya kutoa taaluma vijijini juu ya wananchi kujikinga na Kichocho kama ilivyofanyika kwa upande wa kudhibiti Malaria nchini.

Amesema Kichocho hicho huambukizwa kutoka kwa mtu mwenye ugonjwa huo kujisaidia haja ndogo kwenye maji safi iwe ya Mto, Bwawa au Ziwa, ambapo baadae vimeleya hulelewa na Konokono maalum wajulikanao kwa jina la kitaalamu kama (Bullinus Globosus).


Amefahamisha kuwa ugonjwa wa Kichocho wa Kibofu cha Mkojo pia kinaweza kusababisha Saratani ya Kibofu hicho endapo kitakosa dawa muafaka kwa muda mrefu hivyo amewataka wananchi kufika vituo vya afya mara tu watakapoona dalili za ugonjwa huo.


Amesema Serikali kupitia Wizara ya afya  inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na Kichocho tangu miaka ya 1970 na huduma zimekuwa zikitolewa zaidi kwa watoto wa shule katika kupunguza kasi ya maambukizi kama ijulikanavyo kuwa watoto ndio waathirika wakuu wa ugonjwa huo.

Ameeleleza kuwa kuanzia Mwaka 2012 Wizara ya Afya imeongeza mikakati katika kudhibiti na hatimae kutokomeza kabisa ugonjwa huo visiwani Zanzibar ikiwemo kulisha dawa za Kichocho na Minyoo katika jamii ya Wazanzibari mara 2 kwa Mwaka, kunyunyiza dawa za kuangamiza Makonokono kwenye Mito na Mabwawa katika Shehia mbalimbali za Unguja na Pemba, unyunyizaji wa dawa hufanyika kila mwisho wa msimu wa mvua, pamoja na kutoa elimu ya Kichocho kwa jamii na mashuleni kwa lengo la kuwaelimisha wanafunzi juu ya athari za ugonjwa huo.

Amesema jumla ya Mito 98 kwa upande wa Unguja na 120 kwa upande wa Pemba inanyunyiziwa dawa kila Mwaka na Serikali ya Zanzibar inashirikiana na Serikali ya Watu wa China, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) pamoja na  Wadau wengine wa maendeleo katika kutoa huduma kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa maradhi ya Kichocho yanabaki kuwa historia visiwani Zanzibar.


            IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.