HOTUBA
YA MAONI YA KAMATI YA KUSIMAMIA AFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA YA BARAZA LA
WAWAKILISHI KUHUSU BAJETI YA OFISI YA MAKAMO WA PILI WA RAIS KWA MWAKA
2015/2016.
Mhe.
Spika,
Kwanza naomba kwa sote
tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na Afya njema na kuweza kukutana
hapa kuweza kutekeleza majukumu tuliyopewa na wananchi wetu waliotuchagua.
Mhe.
Spika,
Pili nikushukuru kwa
kunipa nafasi ya mwanzo kwa niaba ya Kamati yangu kuweza kuchangia hotuba hii
iliyowasilishwa na Mhe Waziri, wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, kwa
utulivu na umahiri mkubwa.
Mhe
Spika, Pia nimshukuru Mhe Waziri pamoja na watendaji wake
kwa kuweza kushirikiana vizuri na Kamati kwa kipindi chote cha miaka mitano,
mashirikiano hayo tunaamini yameleta ufanisi mkubwa kwa Wizara. Pia katika
Serikali na ndio maana leo hii Waziri ameweza kusimama hapa mbele ya Baraza
lako tukufu akijinasibu kwa mafanikio makubwa ya Serikali katika kipindi chao
cha Awamu ya saba yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa ambapo hata sisi wananchi tumeridhika
na hatua ya maendeleo inayopigwa na Serikali yetu huku Nchi yetu ikishuhudia
utulivu,
Amani na mashirikiano makubwa kwa viongozi wetu wakuu na hata sisi
tunaofuata jambo ambalo limeleta hali ya amani kwa wananchi wetu wa kawaida,
tunaomba wananchi wote vwa Zanzibar waendelee na utulivu huo hasa katika
kipindi hiki kigumu kisiasa kwatika Nchi yetu kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa
2015, kwa sote basi tumuombe Mwenyeenzi Mungu atujaalie na Amani yetu hadi
kumaliza uchaguzi wetu mkuu kwa salama na Amani. AMIN.
Mhe
Spika, tatu kwa niaba ya Kamati yangu niungani na wewe
kwa Kumshukuru na kumpongeza Mhe Rais wetu D.k Ali Mohd Shein kwa uongozi wake
bora na wenye busara kubwa kwa kuiongoza nchi yetu hii kwa salama na Amani
katika vkipindi chake chote cha miaka mitano cha Serikali yake ya awamu ya Saba
iliyopata mafanikio makubwa katika maendeleo ,ustawi wa jamii, na Amani na
utulivu kwa muda wote wa miaka mitano, na pale ilipotokea dalili za vurugu
hakuyumba ila alisimamia Katiba na Sheria za Nchi yetu katika kukabiliana na
Changamoto hizo na leo hii tunajivunia Amani tuliyonayo na iko haja ya kuilinda
kwa hali zote.
Mhe
Spika, kwa kua hii ni Bajeti ya mwisho ya Serikali hii ya
Awamu ya Saba basi naomba utuvumilie kwa kuchukua muda wako mwingi wa
kuwapongeza viongozi wetu wa Nchi yetu, kwa hiyo nachukua fursa hii adhim kwa
kutoa pongezi zetu maalum kwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ,Mhe Balozi
Seif Ali Iddi kwa uwezo wake mkubwa aliounyesha kwa kumsaidia Mhe Rais kuongoza
Nchi yetu kwa umahiri wake, ustahamilivu na uvumilivu mkubwa wakati wote huo wa
uongozi wake kwani amekua ni kiungo kikubwa baina ya Serikali na Baraza lako la
Wawakilishi na pia amekua Balozi mkubwa wa Serikali kwa matakwa ya Serikali kwa
wajumbe wa Baraza lako hili na hata pale tulipokua wagumu basi alitumia uzoefu
wake wa Kidiplomasia kutulainisha na kweli tuliweza kulainika na mambo yao kama
Serikali yalipita bila ya kupingwa, hii inatuonyesha kua kweli Zanzibar ni
chimbuko la viongozi ,mahiri na wenye busara na wanaweza kuivusha Nchi yetu kwa
salama na Amani katika mawimbi na misukosuko ya aina yeyote bila ya msaada
kutoka nje, nadhani somo hili la Zanzibar iko haja na Nchi nyingine za kiafrika
waje Zanzibar ili kujifunza namna ya kuweza kusuluhisha tofauti zao bila ya
kumwaga damu na kuweza kuendesha Nchi zao kwa upendo na mashirikiano
makubwa.
Mhe
Spika, pia naomba kutoa shukrani zetu za Kamati kwa Makamo wa kwanza wa Rais kwa ,kuweza kumsaidia Mhe Rais wa
Zanzibar, katika kutekeleza majukumu yake kwa nchi yetu, pamoja na tofauti zao
za kisiasa na wakati mwingine wananchi walipata wakati mgumu kuhisi labda kauli
zinatofautiana lakini kimsingi bado kiujumla mambo mengi wamekua wakishirikiana
na kwa kua tumeukubali mfumo wa vyama vingi wa kisiasa na pia tukaongezea mfumo
mpya Duniani wa Serikali ya umoja wa Kitaifa inabidi tuwe wastahamilivu kwani
ndio kipindi cha mwanzo cha mfumo huo kwa hiyo inabidi tuvumiliane, hapa kubwa
kwa wananchi wetu tushukuru kuwa tumeweza kuvuka salama katika mfumo mpya wa
kuongoza Nchi kama nilivyosema hapo awali basi wenzetu Nchi jirani na hata wa
mbali basi wanaweza kuja kujifunza miujiza hii ilyotokea hapa Zanzibar, kwa
hiyo naomba naomba wananchi wote tuige mfano ulioonyeshwa na viongozi wetu hawa
wa kutoautiana bila ya kugombana.
Mhe
Spika, nitakua mwizi wa fadhila bila ya kukushukuru wewe
mwenyewe binafsi kwa kuendelea kutuongoza kwa kipindi chote cha miaka mitano ya
uhai wa Baraza hili la nane kwa umahiri mkubwa na busara zisizo na kifani
katika kipindi cha hali ya utulivu Barazani na pale ambapo kunapotokea dalili
za misukosuko umekua ukiirejesha hali ya utulivu Barazani bila ya kuonekanwa
unapendelea upande wowote kati ya pande mbili zilizopo hapa Barazani hii
inatuonyesha ni jinsi gani ulikomaa kwenye utendaji na uadilifu katika
kusimamia haki, kwa kusaidiana na wasaidizi wako akiwemo, Naibu Spika, na
Wenyeviti wa Baraza. Kwa hiyo mimi na Kamati yangu tumeridhika kabisa na
uongozi wako.
Mhe.
Spika,
Kama Waheshimiwa
Wajumbe wako wanavyoelewa kuwa, Serikali imeanzisha rasmi utaratibu wa
kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Serikali kwa mfumo wa
kuzingatia program (PBB), mfumo ambao kwa Waheshimiwa Wajumbe wameshakuwa
waelewa kutokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na Baraza letu, lakini
wanaowawakilisha bado ulelewa wao upo kama zamani, wa bajeti ya mfumo wa
vifungu vya matumizi (Line Budget)
Mhe.
Spika,
Pamoja na juhudi
zilizochukuliwa na Serikali, sote tunakubaliana na ukweli kwamba, kumfahamisha
mtu aliyetumwa ni lazima kuende sambamba na kumuelewesha yule aliyemtuma, kwani
kumuelemisha aliyetumwa bila aliyetuma, ni sawa na kuufanya utumishi
usiohitajika kwa wakati huo.
Mhe.
Spika,
Nakusudia kusema kuwa,
pamoja na juhudi za elimu ya bajeti ya mfumo wa PBB kutolewa kwa Waheshimiwa
Wajumbe, elimu hiyo pia inapaswa kutolewa kwa watendaji katika ngazi za chini
za Serikali, taasisi, mashirika, pamoja na wananchi ambao ndio waliowachagua na
kuwateua Wajumbe wa Baraza hili, kwani mipango yote hiyo inamalizia kwao kwani
ndio watakaopata huduma zilizokusudiwa.
Mhe
Spika, kama alivyoelezea Mhe Waziri kuhusu hali ya
kisiasa hapa Zanzibar kwa hivi sasa ni nzuri kwani kama tulivyoelezea hapo
awali kuwa viongozi na wananchi wanaendelea kushirikiana katika shughuli mbali
mbali za kiuchumi na kijamii, kwa hiyo tunamshukuru sana Rais wetu kwa kuweza
kuisimamia kwa kikamilifu hali hiyo na kwa sote tumuombe Mwenyeenzi Mungu hali
hiyo iendelee hivyo hivyo milele ili kuijenga nchi yetu kiuchumi kwani huko
nyuma tumeshajifunza mambo mengi ya vurugu hayakutusaidia chochote ila kututia
hasara kwa kujenga chuki baina yetu.
Mhe
Spika, kamati yangu tunaendelea kumuunga mkono Mhe Waziri
kwa kuwaomba wananchi wote wa Zanzibar kwa kua huko mbele Nchi yetu inategemea
kuingia katika maamuzi magumu ya kinchi ya kupiga kura ya maoni ya Katiba
inayopendekezwa kwa kupiga kura ya kuiamulia hatma ya baadae nchi yetu basi ni
vyema wananchi wakaendelea kuzitafuta nakala za Katiba hiyo ili kuzisoma na
kuzielewa vizuri ili siku ikifika kuweza kuipigia kura Katiba inayopendekezwa,
kwa hiyo kamati yangu tunawaomba wananchi wote kuweza kuitumia haki yao hiyo ya
msingi ya kidemokrasia ya kuamua wanachokitaka bila ya kubughudhiwa na mtu
yeyote, kwani sisi wazanzibari kwa muda mrefu ndio tuliokua tukilalamika kua
Katiba ilyopo hivi sasa inamapungufu mengi na wakati umefika kutokana na
mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi katika Nchi yetu basi iko haja ya
kuweza kuirekebisha ili na sisi Zanzibar tuweze kutononoka kiuchumi.
Mhe
Spika, sambamba na hilo pia si muda mrefu Nchi yetu
inategemea kuingia katika mtihani mwingine wa wananchi kupiga kura ya kuweza
kuwachagua tene viongozi wao ili kuweza kuwaongoza na kuwawakilisha katika
kipindi kingine cha miaka mitano na kuiweka Serikali itakayowaongoza kwa kipindi
kingine cha miaka mitano, hapa kamati yangu inawaomba tena viongozi na wananchi
kuweza kuilinda Amani tuliyonayo na wala tusikaribishe viashiria vyovyote vya
vurugu kwani huu utakua ndio mtihani wa mwanzo baada ya ya kuanzisha Serikali
ya Umoja wa Kitaifa hapa Zanzibar, kwani tukifeli mtihani huu basi Zanzibar
haitokuweko njia nyingine ya sulhu ya Amani kwani itakua vurugu ndio maumbile
yetu, lakini sisi kama ndio viongozi tuliopewa dhamana na wananchi wetu
kutuongoza basi ni vyema kuweza kua mstari wa mbele katika kuisimamia na
kuilinda kwa maslahi ya wananchi wetu wanyonge.
Mhe
Spika, Kamati yangu inaipongeza Serikali kupitia hotuba ya Mhe Waziri kua tume ya
Uchaguzi imeshajiandaa na kusimamia kura ya Maoni na uchaguzi Mkuu katika hali
ya Amani na utulivu na kupitia kauli mbali mbali za viongozi akiwemo Mhe Rais,
na leo Makamo wa pili wa Rais kuwa uchaguzi utakua wa huru na wa Haki kwa hiyo
tunaiomba Tume ya Uchaguzi kuwa waadilifu katika kulisimamia hilo ili wananchi
wote wa Zanzibar wenye haki ya kupiga kura basi waweze kuitumia haki yao hiyo
ya msingi ya kuwachagua viongozi wao wanaowataka.kwa uhuru mkubwa bila ya
bughudha yeyote, kwa hiyo kamati yangu inawataka wananchi wote waliotimiza
masharti ya kupiga kura wakajiandikishe ili kuweza kuja kuitumia haki yao hiyo
ya kikatiba ya kupiga kura.
Mhe
Spika, kamati yangu pia inaungana na hotuba ya Mhe Waziri
kwa kuipongeza Serikali yetu kwa kuendelea kuwaonyesha moyo wananchi wetu kwa
kuwapunguzia mzigo wa maisha wananchi wetu kwa kufuta ada zote za kiingilio cha
Skuli pamoja na kufuta ada ya mitihani yote kuanzia Skuli za msingi hadi form
six ,hili ni jambo kubwa sana hasa kwa wananchi wetu wanyonge ambao hata mlo
mmoja kwao ni shida, kwa mtu wa kawaida hili jambo jama kwani utakuta katika
familia moja kwa wakati mmoja familia inao wanafunzi kiasi watano au sita kwa
wakati mmoja na wote wanahitaji ada ya kiingilio cha Skuli na wengine ada ya
mitihani jambo ambalo linampelekea mzazi kuchanganyikiwa kwani uwezo hana na
wakati mwingine kushindwa kupata pesa na watoto kukosa haki yao ya msingi ya
kupata Elimu.kwa hiyo tunawaomba vijana wetu kuunga mkono jitihada za Serikali
yetu ili kuweza kuwapatia Elimu bora kwa hiyo wajitahidi katika kujisomea ili
waweze kufaulu masomo yao, ili kuja kuijenga nchi yetu hapo baadae.
Mhe
Spika, sambamba na hilo tunaipongeza Serikali kwa kuweka
mazingira mazuri ya kuwawezesha vijana wetu waliofaulu masomo yao kuweza kupata
mikopo kupitia Mfuko wa Elimu ya juu kwa masomo yao ya ndani na nje ya Nchi
,kwa hapa kamati yangu tunaiomba Serikali kwa mwaka huu pamoja na pesa
zitakazotolewa kwa mfuko wa Elimu ya juu basi ikiwa wanafunzi wengi
watajitokeza watakaohitaji pesa za mkopo basi kuangalia uwezekano kuongezewa
fedha hizo kupitia pesa za kodi ya miundombinu tuliyoipitisha jana tu ili
kuweza kuusapoti mfuko huu ili kuhakikisha kila kijana wetu anaehitaji mkopo wa
Elimu ya juu basi aweze kupata fursa hiyo, lakini pia kamati yangu inaiomba
Afisi ya Makamo wa pili wa Rais ambayo ndiyo inayoratibu na kusimamia shughuli
zote za Serikali kufuatilia wanafunzi wote waliopata mikopo ya Elimu ya juu
siku za nyuma ili kuweza kuanza kurejesha pesa hizo ili ziweze kuzunguka na
wenzao waweze kuzitumia kwa ajili ya kujiendeleza kielimu.
Mhe
Spika, kama alivyoeleza Mhe Waziri katika kitabu chake
ukurasa wa 8 kif. (19.0) katika sekta ya Afya Serikali imeendelea kuboresha huduma
za Afya na hapa tunaipongeza Serikali kwa kutekeleza ahadi yake kupitia Waziri
wa Fedha pale kwenye Bajet ya mwaka uliopita tulipozuia Bajeti ya Wizara ya
Afya kwa kushindwa kukitengeneza chumba cha ICU ambapo hali yake ilikua mbaya
au hata kusema tulikua hatuna kabisa huduma ya ICU na kupelekea Waziri wa Affya
kwa wakati ule Mhe Juma Duni Haji kutaka kujiuzulu lakini aliposimama Waziri wa
Fedha na kumuokoa kwa kusema kua Serikali itahakikisha ICU kwa Hospitali kuu ya
Mnazi mmoja itajengwa, leo tunafuraha kusema zile kelele zetu za wajumbe Wa
Baraza clako hili tukufu kuitaka Serikali kujenga ICU tunathubutu kusema
tumeridhika kabisa na tunaimani kwa hivi sasa huduma hiyo inatumika vizuri na
wananchi wetu.
Mhe
Spika, sambamba na hilo pia tunaipongeza Serikali kwa
kusikia kilio chetu cha muda mrefu cha ukosefu wa madaktari bingwa na wauguzi
kuwa kilio hicho sasa kimeanza kupungua kwa kuongeza idadi kubwa wa madaktari
na wauguzi katika Hospitali yetu kuu ya Mnazi mmoja na zile kilizoko katika vijiji vyetu, kwa
kweli hivi sasa tunashuhudia tumeletewa madaktari na wahudumu kwatika Hospitali
zetu ikiwemo na ile ya Jimbo langu la Kwamtipura kwakweli tunawashukuru sana.
Mhe
Spika, sambamba na hilo tunaipongeza Serikali kwa
kuandaa Shiria ya Condominium pamoja na kuanzisha Sheria ya kuunda Shirika la
nyumba ili kuweza kuwawezesha wananchi wanaoishi katika nyumba za maendeleo
pamoja na nyingine za Serikali kuweza kumiliki sehemu ya nyumba hizo kwa
kushirikiana na Serikali lakini pia kuanzisha ujenzi wa makaazi ya wananchi kwa
bei nafuu ili kuweza kuleta maisha bora na yenye faraja wananchi wetu. Kwa hiyo
tunaiomba Serikali kuinazisha Mamlaka hiyo ya nyumba na wakabidhiwe watu wenye
ubunifu na uwezo wa kuweza kuandaa mbinu za kupata fedha na kuweza nyumba hizo
kwa haraka ili lile lengo la Serikali liweze kufikiwa kwa haraka.
Mhe
Spika, kama alivyoeleza Mhe Waziri kuwa Serikali imeguswa
sana na suala la udhalilishaji na ukatili wanaofanyiwa wananchi wetu hasa
wakiwemo wanawake na Watoto, kwa kweli suala hili ni kubwa na linakera sana na
linauma sana na linakera, kwakweli hivi sasa Zanzibar imekua ni aibu kubwa hasa
unapowaona watu wazima wenye akili zao wanawabaka watoto wafdogo wengine hata
hawajafiikia umri wa miaka kumi hii ni aibu kubwa kwa hiyo tunaungana na jitihada
za Mhe Rais kwa kuunda kamati ya Mawaziri ili kushughulikia suala hilo, lakini
tunaiomba kamati hiyo bado hatujaona makali yake kwani kila siku ikisikiliza
habari za mawio utasikia kesi mpya za watoto kubakwa na wala hatusikii hukumu
za watu waliobaka, tunaitaka Serikali kuhakikisha suala hili linakoma hapa
Zanzibar.
Mhe
Spika, suala la Rushwa limekua ni suala la kusikitisha
sana na tunapongeza jitihada za Serikali kwa kuanzisha Sheria ya kupambana na
Rushwa pamoja na Sheria ya Maadili ya
Viongozi, ingawa kuunda Sheria ni suala moja lakini tatizo linakuja katika
kutekeleza Sheria hizo kwani tumeona kuna vitando vingi vya rushwa bado
vinaendelea na nyingine ni za wazi wazi, lakini pia kuna ukiukwaji mkubwa
taratibu za kisheria katika shughuli nyingi Serikalini nadhani wakati umefika
tupunguze kuoneana muhali hasa katika mambo mazito ya shughuli za Serikali, ili
kujenga jamii inayoheshimu Sheria na kufuata taratibu tunazojiwekea vinginevyo
kila siku tutakua tunapiga kele kua Sheria hazifuatwi lakini wakosaji ndio
sisi, kwa hiyo tunaomba kwanza tuanze sisi viongozi kufuata Sheria ili na walio
chini yetu kuweza kutuiga vinginevyo na wao wataiga mifano yetu.
Mhe.
Spika,
Kwa ujumla Ofisi ya
Makamo wa Pili wa Rais, inahitaji kuidhinishiwa Tsh. 23,333,300,000 kwa matumizi ya kawaida na matumizi ya shughuli za
maendeleo, fedha ambazo zinahitajika kwa Ofisi yenyewe ya Makamo wa Pili wa
Rais, Baraza la Wawakilishi na Tume ya Uchaguzi. Aidha, kati ya Taasisi hizi
tatu kuu, ni Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais pekee ndiyo yenye makadirio ya
makusanyo kupitia Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na
Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, huku Taasisi zenye makadirio ya
fedha za Maendeleo kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa kwa Kamati, ni Ofisi
ya Makamo wa Pili wa Rais pekee.
OFISI
YA MAKAMO WA PILI WA RAIS
Mhe.
Spika,
Kama alivyoeleza
Waziri afisi hii inatarajia kukusanya Tsh. 612,360,000 kwa mwaka 2015/2016,
fedha ambazo zitapatikana kutokana na huduma wanazozitoa Idara ya Upigaji Chapa
na Mpiga chapa Mkuu wa Serikali, fedha ambazo ni Tsh. 600,000,000 kutokana na
mauzo ya uchapishaji na Tsh. 12,360,000 zinatarajiwa kupatikana kutoka katika
Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, ambapo Tsh. 3,000,000 zitatokana na
malipo ya Ukodishaji wa Vifaa na Tsh. 9,360,000 zitatokana na malipo ya kazi za
biashara.
Mhe.
Spika,
Kamati yangu inafahamu
kuwa, Serikali inajaribu kujitahidi kuwa na njia za uhakika za kufanya makadirio ya makusanyo ya fedha mbali mbali kwa
kipindi cha mwaka wa bajeti, hasa kupitia katika Wizara na Taasisi zake mbali
mbali. Bado hufanya makisio ya uzoefu wa mwaka ama miaka iliyopita katika
kuamua na kuzielekeza taasisi zake kutafuta mapato kwa kupitia vyanzo mbali
mbali vya makusanyo hayo. Kwa mfano, Mauzo ya Uchapishaji ambayo mwaka huu
yamekisiwa kuwa Tsh. 600,000,000 ndio hizo hizo zilizokadiriwa mwaka uliopita.
Aidha, fedha zilizokadiriwa kwa mwaka 2013/2014 kwa Idara ya Upigaji Chapa na
Mpiga chapa Mkuu wa Serikali, zilikuwa Tsh. 500,000,000 kupitia Mauzo ya
Uchapishaji, lakini fedha halisi zilizokusanywa zilikuwa Tsh. 42,776,200 kukiwa
na tofauti ama upungufu mkubwa wa Tsh. 457,223,800, na mapato halisi
yaliyopatikana ni sawa na asilimia 8.5 tu ya makadirio. Ambapo hali hii kama
tunavyoelewa hali iliyokua nayo Idara hii ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali
hatushangai kua kweli walishindwa kutimiza malengo yao, kutokana na uchakavu wa
mitambo pamoja eneo walilokua wakifanyia kazi lilikua katika hali mbaya sana,
lakini kwa sasa kamati yangu inajinasibu kuwa zile kelele za Serikali kihamishia
Idara ile katika katika eneo lililo salama ili waweze kufanya kazi zao kwa
utulivu mkubwa kama tulivyoanza kuona hivi sasa.
Mhe.
Spika,
Kamati yangu inakubali
ni kweli Serikali kuwa, iliipa Idara dhima kubwa zaidi ya makusanyo kwa mwaka
2014/2015, ikizingatiwa kuwa mwaka 2013/2014, Idara hii na Ofisi ya Makamo wa
Pili wa Rais kwa ujumla haikuweza kufikia malengo hata kwa asilimia 10 ya
makadirio ya makusanyo. Na ndipo mwaka 2014/2015 kama ilivyo pia kwa mwaka
2015/2016, Idara hii kwa kupitia chanzo hicho hicho cha Mauzo ya Uchapishaji,
kimekadiriwa kukusanya Tsh. 600,000,000. Kiwango ambacho ni kikubwa
ukilinganisha na makadirio ya mwaka 2013/2014 na 2014/2015.
Mhe.
Spika,
Kamati yangu kwa mwaka
huu wa fedha kupitia vyanzo vya mapato vya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais,
imeshuhudia tena kuondoshwa kwa vyanzo vya mapato ambavyo vilikuwa vinatumika
kwa miaka iliyopita. Kwa mfano, mwaka 2014/2015, Idara ya Uendeshaji na
Utumishi ilikadiriwa kukusanya Tsh. 5,000,000 kupitia Ukodishaji wa Ukumbi wa
Mikutano (Hire of Conference Seminar), chanzo ambacho kilianza kukisiwa na
kuingizwa katika vyanzo vya mapato vya Idara hii mwaka 2013/2014 . kamati yangu
imeridhika kwa mwaka huu kukiondoa chanzo hicho kwani hali ya ukumbi ule
uliotegemea kukusanya mapato hauko katika hali nzuri, kwa hiyo tunaitaka
Serikali kuweza kufanya maamuzi katika umilikaji wa Ukumbi huo wakati ambapo
hata Baraza la wawakilishi waliomba uwe chini yao.
Mhe.
Spika,.
Halikadhalika kwa
Idara ya Sherehe na Maazimisho ya Kitaifa, mwaka 2013/2014 ilikadiriwa
kukusanya Tsh. 3,000,000 lakini fedha hizo hazikukadiriwa hata shilingi moja
kwa mwaka 2014/2015 na mwaka 2015/2016 chanzo hicho cha fedha hakionekani
kabisa katika bajeti ya Idara hii, sawa ilivyo katika Ofisi hii ya Makamo wa
Pili wa Rais.
Mhe.
Spika,
Kwa upande wa matumizi
ya kazi za kawaida, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais inakadiriwa kutumia Tsh.
5,066,700,000 kwa ajili ya Mishahara ambazo fedha zitakazotumika kwa matumizi
haya ni Tsh. 1,967,950,000, Maposho yatatumia Tsh. 703,179,000 na fedha za
kuendesha Ofisi ni Tsh. 2,395,571,000. Aidha, kwa matumizi ya maendeleo, fedha
zinazohitajika kwa mwaka huu wa fedha ni Tsh. 100,000,000, kwa kuzingatiwa kuwa
Tsh. 24,550,000 zitatumika kwa matumizi ya uendeshaji wa mradi na Tsh.
75,450,000 zitatumika kwa matumizi ya utekelezaji wa mradi.
Mhe.
Spika,
Fedha hizo
zinatarajiwa kutumika kupitia program kuu nne ambazo ni Uratibu awa Shughuli za
Makamu wa Pili wa Rais, yenye program ndogo hiyo hiyo. Program Kuu ya Pili ni
Uratibu wa Shughuli za Serikali yenye program ndogo tatu ambazo ni Kukabiliana
na Maafa, Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na kuwaenzi viongozi wa
Kitaifa na Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, Program Kuu ya
Tatu ni Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa ambayo program yake ndogo ni
hiyo hiyo na Program Kuu ya Nne ni Mipango na Utawala yenye program ndogo tatu
ambazo ni Uongozi na Utawala, Mpingango, Sera na Utafiti na Ofisi Kuu Pemba.
Mhe.
Spika,
Ofisi inahitaji
kupatiwa Tsh. 625,569,000 kwa Program Ndogo ya Uratibu wa shughuli za Makamu wa
Pili wa Rais, ambayo pia ni Program Kuu fedha ambazo zitatumika zaidi kwa
kuwapatia maslahi bora wafanyakazi, kulipia gharama za uendeshaji wa Ofisi,
kuimarisha huduma za usafiri za Idara kwa kazi za kila siku, kununua vifaa vya
kuandikia, vya usafishaji, samani pamoja na vifaa vyengine kwa matumizi ya
Ofisi na kwa ajili ya mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu.
Mhe.
Spika,
Program Kuu ya Uratibu
wa Shughuli za Serikali inahitaji Tsh. 2,239,727,000 ili iweze kutekelezeka na
kwa upande wa Idara ya Maafa ambayo kwa kuzingatia mfumo wa Bajeti ya PBB,
tunaweza kusema kuwa, shughuli zote za Idara hii zimo katika program ndogo ya
Kukabiliana na Maafa chini ya Program Kuu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali,
kwa mwaka 2014/2015 ilikadiriwa kutumia Tsh. 298,447,800 kwa kazi za kawaida,
na kwa mwaka huu wa fedha, Programu ndogo hii inahitaji Tsh. 405,775,000, ikiwa
ni ongezeko la Tsh. 107,327,200.
Mhe.
Spika,
Tunaipongeza Wizara na
Serikali kwa ujumla kwa ongezeko hilo, lakini tufahamu kuwa, fedha hizo pamoja
na kuongezwa kwake na ikizingatiwa maafa
yanayoikabili nchi yetu, ni fedha kidogo ambazo zinapaswa ziongezwe mara dufu.
Kwa mfano tu ukizingatia maafa ya mvua zinazoendelea kunyesha, namna ya
kukabiliana na maafa haya, kuwasaidia walioathiriwa na mvua, kunahitaji
matumizi makubwa ya fedha, pamoja na ukweli wa kutarajiwa kutumika kwa fedha za
mradi zinazohusiana na maafa kama tutakavyoeleza baadae. Hapa tunaiomba
Serikali sasa kuanzisha rasmin ule mfuko wa maafa ili uweze kusaidia kutoa
huduma kwa haraka pale maafa yanapotokea kwani maafa siku zote hayapigi hodi
pale yanapotaka kutokea.
Mhe.
Spika,
Program Ndogo ya
Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa ambayo
shughuli hii mwanzo ilisimamiwa na Idara ya Sherehe na Maazimisho ya Kitaifa,
kwa mwaka uliopita ilikadiriwa kutumia Tsh. 871,615,500 lakini kwa mwaka huu
kwa kuzingatia program ndogo niliyoitaja kabla, fedha zinazohitajika kwa
matumizi hayo ni Tsh. 987,260,000, ikiwa kuna ongezeko la Tsh. 115,644,500 sawa
na ongezeko la asilimia 113.2 ya makadirio ya mwaka jana. Aidha, Kwa program
ndogo ya Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, fedha zinazohitajika
kukamilisha fedha za Program Kuu ni Tsh. 846,692,000.
Mhe.
Spika,
Program Kuu ya
Usimamizi wa Shughuli za Upigaji Chapa ambayo program yake ndogo ni hiyo hiyo,
imekadiriwa kutumia Tsh. 714,050,000 kwa mwaka 2015/2016, ambazo ni nyongeza ya
Tsh. 231,983,400.
Fedha za program ndogo
hii zinatarajiwa kutumika kwa kuwapatia stahiki na maslahi bora wafanyakazi
ikiwa ni pamoja na maposho, mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu (kwa
wafanyakazi 7 wa Idara), kuimarisha huduma za uchapaji, ikiwa ni pamoja na
ununuzi wa mafuta na vilainisho, kulipia gharama za umeme, kununua vifaa vya
usafishaji, vespa, matengenezo ya mitambo na kununua zana na vifaa bora vya
uchapishaji, kulipia gharama za matangazo na kuandaa mpango wa biashara, sheria
na miongozo.
Mhe.
Spika,
Program Kuu ya
Mipango, Sera na Utawala inakadiriwa kutumia Tsh. 1,587,354,000 kwa mwaka
2015/2016 huku fedha hizo zikielekezwa kwa matumizi ya program ndogo ya Uongozi
na Utawala (Tsh. 780,741,000), Mipango, Sera na Utafiti (Tsh. 271,792,000) na
Ofisi Kuu Pemba (Tsh. 534,821,000).
Mhe.
Spika,
Ofisi Kuu Pemba, mwaka
2013/2014 ilikadiriwa kutumia Tsh. 452,817,000 na fedha halisi zilizoingizwa
hadi kufikia March 2014 zilikuwa Tsh. 254,014,050 sawa na asilimia 56 ya
makadirio. Kwa mwaka 2014/2015, fedha zilizokadiriwa zilikuwa Tsh. 388,964,000 na
fedha halisi zilizoingizwa hadi March 2015, zilikuwa ni Tsh. 85,815,350, kukiwa
na upungufu wa Tsh. 303,148,650 ya makadirio. Hali hii bado inaonesha kuwepo
kwa tatizo la uingizwaji wa fedha, bila ya kujali tuna mfumo gani wa bajeti.
Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ambayo sasa ni program ndogo ya Mipango, Sera
na Utafiti kwa mwaka 2014/2015, kwa kipindi cha July hadi March, iliingiziwa
Tsh. 55,621,903 na makadirio yalikuwa Tsh. 83,289,000 sawa na asilimia 88 ya
makadirio.
Mhe.
Spika,
Tsh. 100,000,000
zinazohitajika kwa matumizi ya miradi ya maendeleo, miradi ambayo imo katika
Program Kuu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali katika program ndogo ya
kukabiliana na maafa, ambapo mradi wa Kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa
unahusika, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga kwa fedha za ndani
Tsh. 15,000,000 kwa ajili ya kuandaa michoro na kusimamia Kituo cha huduma za
dharura cha kukabiliana na maafa na Tsh. 35,000,000 kwa ajili ya kufanya
matengenezo ya vituo vya kukabiliana na maafa.
Mhe.
Spika,
Kamati imetaka
kupatiwa fedha halisi za wafadhili zinazotarajiwa kuchangiwa na washirika mbali
mbali wa maendeleo na kuelezwa kuwa ni Tsh. 204,950,000 kwa mwaka 2015/2016. Aidha,
kwa mwaka 2014/2015, Serikali ilikadiriwa kuchangia Tsh. 40,000,000 na
wafadhili kuchangia Tsh. 1,282,880,000 na hivyo, jumla ya Tsh. 1,322,880,000
zilikadiriwa kwa ajili ya kujenga uwezo na kukabiliana na maafa.
Mhe.
Spika,
Kwa kuzingatia kuwa
mwaka huu Serikali itachangia Tsh. 50,000,000 na wafadhili wa maendeleo
kuchangia 204,950,000 kunaifanya bajeti inayokadiriwa kwa matumizi ya miradi ya
program ndogo hii ya kukabiliana na Maafa kuwa Tsh. 254,950,000 wakati mwaka
uliopita fedha zilizokadiriwa zilikuwa Tsh. 1,322,880,000 kwa upungufu wa
1,067,930,000, huku sote tukijua kuwa, kwa suala zima la kukabiliana na maafa,
siku zote fedha huwa hazitoshi jambo linaloipekelea Serikali kuwa na uwezo
mdogo sana wa kukabiliana na maafa hayo.
Mhe.
Spika,
Kwa ajili ya
utekelezaji bora wa progam ndogo ya shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iliyo chini ya program kuu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali,
inahitaji Tsh. 50,000,000 ambazo zitatumika kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF III) kwa kuzingatia uchambuzi ufuatao:
·
Tsh. 7,000,000 kwa ajili ya kusimamia
miradi midogo 40 Unguja na Pemba.
·
Tsh. 2,900,000 kwa ajili ya kuratibu
shughuli za miradi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
·
Tsh. 5,300,000 kwa ajili ya kufanya
vikao 8 vya Kamati ya Uongozi.
·
Tsh. 13,520,000 kwa ajili kusimamia
shughuli za uendeshaji.
·
Tsh. 13,160,000 kwa ajili ya kufanya
ziara za kikazi, mafunzo na kuandaa kikao cha ujumbe wa Benki ya Dunia.
·
Tsh. 3,500,000 kwa kutoa elimu kwa njia
ya vipindi vya TV na Redio.
·
Tsh. 1,830,000 kwa kusimamia na
kufuatilia miradi midogo midogo, na
·
Tsh. 2,790,000 kwa kuandaa vikao vinane
vya Kamati ya Uongozi.
BARAZA
LA WAWAKILISHI
Mhe.
Spika,
Baraza la Wawakilishi
nalo limekadiriwa kutumia Tsh. 16,762,600,000 kwa matumizi ya kazi kawaida,
fedha ambazo zitatumika kwa mishahara (Tsh. 1,383,160,000), maposho (Tsh.
12,802,363,000) na matumizi ya uendeshaji wa Ofisi (Tsh. 2,577,077,000) ikiwa
ni tofatuti na mwaka 2014/2015 ambapo Baraza lilikadiriwa kutumia Tsh.
14,564,000,000 kwa matumizi haya ya kawaida, ambapo kwa mwaka huu kuna nyongeza
ya Tsh. 2,198,600,000 .
Mhe.
Spika,
Fedha hizo zinazoombwa
mwaka huu wa fedha zinatarajiwa kutumika chini ya program kuu mbili. Ya kwanza
ni Kutunga Sheria, Kupitisha bajeti na Kusimamia Taasisi za Serikali ambapo
program yake ndogo ni hiyo hiyo na program kuu ya pili ni Uongozi na Utawala wa
Baraza la Wawakilishi yenye program ndogo hiyo hiyo.
Mhe.
Spika,
Program kuu ya kwanza
ambayo bila ya shaka program hiyo hiyo ni ndogo, inahitaji kupatiwa Tsh.
6,539,295,000, fedha ambazo zinahitajika kwa kujadili, kurekebisha na kupitisha
miswada ya sheria; Kusimamia utendaji wa Taasisi za Serikali na kupitisha
bajeti ya Serikali. Katika kutumiwa kwa fedha hizo hadi kufikia tarehe 30 Juni
ya mwaka 2016, Baraza linaahidi mambo yafuatayo:
·
Kufikia asilimia 100 ya uwiyano wa
miswada iliyopelekwa na kupitishwa katika Baraza la Wawakilishi.
·
Kupitisha miswada 14.
·
Wajumbe watakaokuwa wamechangia miswada
ya sheria kufikia asilimia 40.
·
Kamati za Kudumu za Baraza zitakuwa
zimeweza kutekeleza majukumu yake mara nne kwa mwaka na pia zimeweza
kuwasilisha ripoti zao katika Mkutano wa March, 2016.
·
Baraza litaweza kupitisha bajeti ya
Serikali katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mhe.
Spika,
Fedha zinazohitajika
kwa program kuu ya pili ya Uongozi na Utawala wa Baraza la Wawakilishi ambayo
pia ndiyo program ndogo ni Tsh. 10,223,305,000, fedha ambazo zitatumika kwa
kuwapatia Wajumbe na Wafanyakazi wa Baraza lako huduma na stahiki zao na
kuimarisha uwezo wao; kuimarisha mazingira ya kazi ya Afisi ya Baraza pamoja na
kuratibu shughuli za Afisi ya Baraza Pemba.
Mhe.
Spika,
Wajumbe wako wana haki
ya kulihoji Baraza lako na kumhoji Waziri wa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais na
kuchukua hatua wanazoona zinafaa kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Baraza
iwapo viashiria vifuatavyo vitashindwa kufikiwa hadi tarehe 30 Juni 2016:
·
Iwapo asilimia ya Wajumbe na
Wafanyakazi wa Baraza hawatopatiwa stahiki zao kwa asilimia 100.
·
Iwapo Wajumbe wote na Wafanyakazi 24 wa
Baraza hawatopatiwa mafunzo.
·
Iwapo asilimia ya utekelezaji wa Mpango
Kazi hautofikia asilimia 90 na huduma pamoja na matengenezo yanayohusiana na
mazingira ya kazi yatafikia asilimia 100.
·
Iwapo wafanyakazi watapata huduma kwa
asilimia 100 na Wafanyakazi watano watapatiwa mafunzo. Hayo yote yanategemea
upatikanaji na uingizwaji wa fedha kwa wakati kama Program inavyotaka.
Mhe.
Spika,
Mradi wa Maendeleo wa
Kuwezesha Mabunge (Legislative Support Programme (LSP)) ambao mwaka jana
ulikadiriwa kutumia Tsh. 710,615,000 kutoka kwa UNDP bila ya kuwa na mchango
wowote wa Serikali, haukuwasilishwa maendeleo yake mbele ya Kamati na wala
hauonekani katika bajeti ya Baraza la Wawakilishi. Bila ya shaka inaweza kuwa
kunatokana na ule mkakati wa Serikali wa kupanga zile fedha za ndani ama za
Wahisani wa Maendeleo wenye muelekeo mkubwa wa kusaidia, lakini kwa taarifa
tulizonazo, wenzetu UNDP bado wanaendelea na nia ya kutusaidia. Kwa kua kuna
tetesi kuwa wanategemea kuendelea kutusaidi basi ni vyema kukaandaliwa taratibu
za kuuingiza kwenye Bajet yetu katika siku zijazo.
TUME
YA UCHAGUZI
Mhe.
Spika,
Katika mwaka huu wa
fedha wa 2015/2016, Zanzibar tunaingia katika uchaguzi Mkuu na Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar ndie yenye jukumu la kuratibu na kukamilisha uchaguzi huo. Hali hii
inaifanya Tume kutumia fedha nyingi katika maandalizi ya Uchaguzi.
Mhe.
Spika,
Fungu laC.03 la Tume
ya Uchaguzi linahitaji Tsh. 1,404,000,000 kwa ajili ya matumizi ya kazi zake za
kawaida, ambapo Tsh. 501,758,000 zitatumika kwa malipo ya mishahara, Tsh.
630,982,000 zitatumika kwa maposho na matumizi ya uendeshaji wa Ofisi yatakuwa
Tsh. 271,260,000. Kiwango hiki kilichokadiriwa mwaka huu na fedha iliyokadiriwa
kwa matumizi ya kazi za kawaida mwaka jana ambayo ni Tsh. 1,314,100,000 kuna
ongezeko la Tsh. 89,900,000 .
Mhe.
Spika,
Tume ya Uchaguzi ina
porgramu kuu mbili. Programu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Shughuli za Uchaguzi
ambayo program ndogo yake ni hiyo hiyo, na Program Kuu ya pili ni Usimamizi wa
Kazi za Utawala na Uendeshaji wa Shughuli za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar yenye
program ndogo mbili, ya Usimamizi wa kazi za Utawala na Uendeshaji wa Tume ya
Uchaguzi, pamoja na Uratibu wa Shughuli za Uchaguzi Pemba.
Mhe.
Spika,
Program Ndogo ya
Usimamizi wa Kazi za Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Uchaguzi inahitaji
kupatiwa Tsh. 1,214,021,000 na Program ndogo ya Uratibu wa Shughuli za Uchaguzi
Pemba upatiwe Tsh. 189,979,000 fedha ambazo kwa ujumla wake zitatumika kwa
kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kuimarisha mazingira bora ya kufanyia
kazi, kuwajengea uwezo uwezo wafanyakazi
na kufanya ukaguzi na upimaji uwajibikaji.
Mhe.
Spika,
Fedha za Maendeleo
hazikuonekana katika bajeti iliyowasilishwa kwa Kamati, wakati Kamati yangu
inafahamu kuwa mwaka jana, Tume ilikadiriwa kutumia fedha za maendeleo katika
mradi wa kuimarisha demokrasia, uliowadhiliwa na UNDP kwa makadirio ya Tsh.
1,750,000,000. Ni vyema Kamati pamoja na Wajumbe wakafahamu mradi wa maendeleo
unaotarajiwa kuwa Tume ya Uchaguzi kwa mwaka huu wa fedha.
Mhe.
Spika,
Sasa naomba
kukushukuru wewe na Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa usikivu wenu wa
kunisikiliza tokea mwanzo wa hotuba yangu hadi hivi sasa. Napenda pia kwa niaba
ya Kamati, kumshukuru Makamo wa Pili wa Rais, Mhe. Waziri Mohamed Aboud
Mohamed, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, kwa
juhudi zao na ujasiri na moyo wa uzalendo katika kuiongoza Ofisi hii ya Makamo
wa Pili katika kipindi chote cha miaka mitano sasa.
Mhe.
Spika,
Nikushukuru wewe
pamoja na Katibu wa Baraza la Wawakilishi pamoja na watendaji wote wa Afisi ya
Baraza kwa huduma wanazozitoa kwetu Wajumbe na tunaendelea kuwanasihi wasichoke
kutoa huduma bora kwa Wajumbe wote wa Baraza kwa kufuata ipasavyo Sheria na
Kanuni za Utumishi na kwa mazingira pekee ya huduma inavyotolewa Barazani. Mhe.
Spika, Tunamshukuru pia Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi na watendaji wake wote
kwa mashirikiano waliyoyatoa kwa Kamati katika kipindi chote cha uhai wa
Kamati.
Mhe.
Spika,
Shukurani za pekee
ziwaendelee Wajumbe wa Kamati kwa mashirikiano ya pamoja na kuaminiana katika
kazi zetu. Naendelea kuwaombea Wajumbe hawa kurejea tena katika Baraza
linalokuja ili kwa uzoefu walioupata katika kazi zao mbali mbali ikiwa ni
pamoja na kazi za Kamati, na elimu waliyofunzwa na Afisi ya Baraza na Taasisi
nyengine mbali mbali zinazohusika pamoja na wataalamu binafsi, waweze kuzitumia
katika kuwafunza na kuwajenga uwezo wajumbe wenzao hasa wala ambao mara ya
kwanza wamefika katika Baraza hili na kuzisaidia Kamati za Baraza kutekeleza kazi
zao kwa ufanisi mkubwa.
Mhe. Spika,
Naomba uniruhusu sasa
niwatambue Wajumbe wote wa Kamati kama ifuatavyo:-
1. Mhe Hamza Hassan Juma Mwenyekiti
2. Mhe. Saleh Nassor Juma Makamo Mwenyekiti
3. Mhe. Ali Mzee Ali Mjumbe
4. Mhe. Ashura Sharif Ali Mjumbe
5. Mhe.Shadya Mohammed Suleiman Mjumbe
6. Mhe. Makame Mshimba Mbarouk Mjumbe
7. Mhe. Subeit Khamis Faki Mjumbe
8. Ndg.Rahma Kombo Mgeni Katibu
9. Ndg.Othman
Ali Haji Katibu
Mhe. Spika,
Nimalizie shukurani
zangu kwa Makatibu Kamati yetu, ambao ndio macho na masikio ya Kamati. kutoona
kwao, ni sehemu kubwa ya upofu wa Kamati na kutosikia kwao yenye maslahi na
maendeleo ya Zanzibar kupitia utekelezaji wa majukumu yao, kuna mchango mkubwa
wa Kamati zetu kutofanikiwa katika utekelezaji mzima wa majukumu yake.
Mhe.
Spika,
Naomba kuwasilisha.
Hamza
Hassan Juma
Mwenyekiti,
Kamati
ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa
Baraza
la Wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment