Habari za Punde

Zaidi ya familia 200 zaachwa bila ya makaazi kufuatia mvua kali za Masika

Baadhi ya wananchi wakitafuta maeneo ya hifadhi
Familia zisizopungua 200 zimeachwa bila makaazi baada ya makaazi yao kuharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoikumba manispaa ya mji wa Unguja na vitongoji vyake.
Akizungumza na Swahilivilla kwa njia ya simu, mkaazi wa Mwanakwerekwe Sokoni, mjini Unguja ndugu Mussa Makame alisema kuwa mvua hizo zilizoendelea kwa muda wa siku mbili mfululizo, zimepelekea maafa makubwa katika miundombinu mjini humo.
"Hali ya hewa ya Zanzibar kwa siku ya pili leo imekuwa na utata wa hali ya mvua na maafa mengi yametokea", alisema Ndugu Mussa, na kuongeza kuwa kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa za watu wawili kupoteza maisha kutokana na maafa hayo, na kwamba vyombo rasmi vinavyohusika vitatoa taarifa sahihi kuhusu tetesi hizo katika wakati muafaka.
Aliendelea kusema kuwa wananchi wamekuwa wakishirikiana katika juhudi za kusaidia waathikika wa janga hili, na kwamba serikali imetenga makaazi ya muda katika mashule na kujenga mahema kwa ajili ya kuzihifadhi familia zilizoathirika vibaya. 
Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni Mwanankwerekwe, Jang'ombe, Chumbuni na Tomondo. Aliutaja ujenzi holela na miundombinu duni kuwa ni miongoni mwa sababu zilizopelekea watu wengi kuathirika na mafuriko hayo.
Mbali na athari za kijamii, mvua hizo pia zimekuwa na athari za kiuchumi kwa vile barabara kuu inayounganisha mji wa Zanzibar na Mkoa wa Kusini Unguja zimekuwa hazipitiki. Hali hii imepelekea usumbufu kwa wafanyabiashara kutoka maeneo ya kisiwa cha Unguja kufika katika maeneo ya Mjini ambako ndiko kwenye harakati nyingi za kiuchumi.
Katika mahojiano hayo na Bwana Abou Shatry wa Swahilivilla, Ndugu Mussa amewataka Wazanzibari kuacha tofauti zao za kisiasa na kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na maafa hayo. "Mvua ni kudura ya Mwenyezi Mungu, hakuna wa kulaumiwa, na wale wanaoingiza siasa waache kufanya hivyo", alisema Ndugu Mussa, na kuongeza kwamba tayari kuna watu wameanza kuingiza maslahi binafsi ya kisiasa katika swala hili.
Mafuriko haya yanakuja wakati Zanzibar ikiwa bado inaendelea kuuguza jeraha la kimbunga kilicholikumba eneo la Kisiwapanza, kisiwani Pemba wiki chache zilizopita.
Ungana nasi kusikiliza Mahojiano yetu na Ndugu Mussa Makame

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.