Habari za Punde

Balozi Seif azindua mradi wa maji safi na salama Tumbatu

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasili katika Bandari ya Kisiwa cha Tumbatu na kupokewa na Katibu Tawala wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu Nd. Khatib Habib Ali kwa ajili ya uzinduzi wa Mradi wa Maji Safi na salama Kisiwani humo.
 Balozi Seif Ali Iddi akizindua Mradi wa Maji safi na salama katika kisiwa cha Tumbatu ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

 Balozi Seif akimtwisha ndoo ya Maji Bibi Miza Ali Haji mara baada ya kuuzindua mradi wa maji safi na salama katika kisiwa cha Tumbatu kiliopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu waliohudhuria uzinduzi wa maji safi na salama hapo katika eneo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo pembezoni mwa Bandari ya Tumbatu.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar daima itaendelea kutekeleza kazi zote zilizoahidiwa na chama cha zamani cha Afro Shirazy Party { ASP } katika kuwajengea  ustawi bora Wananchi wake.

Amesema  huduma za maji safi na salama ilikuwa ni miongoni mwa ahadi kubwa Nne zilizotolewa na ASP wakati ikiomba ridhaa ya kutaka kuviongoza Visiwa vya Zanzibar wakati ikipigania  kuwakomboa Wananchi wake.

Akizindua mradi wa maji safi na salama uliopo Wilaya ndogo ya Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Balozi Seif Ali Iddi alisema SMZ inatambua  umuhimu wa maji kwa uhai na maendeleo ya Wananchi na ndio maana ikaamua kwa makusudi kutekeleza ahadi hizo.


Alisema hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya Zanzibar hasa Vijijini inatia moyo kutokana na jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Wadau wa Maendeleo ndani na nje ya Nchi kwa kushirikiana katika kukabiliana na upungufu wa maji.

Balozi Seif alifahamisha kwamba ukosefu wa maji safi na salama umekuwa tishio kubwa linaloikumba Dunia na kuonyesha baadhi ya Miji Jamii zake  hupata huduma za maji safi mara moja kwa kipindi cha siku Nne.

Alieleza kwamba karibu Watu Milioni Mbili hufariki Duniani kote kutokana na maradhi yenye uhusiano na ukosefu wa maji safi na salama kama vile maradhi ya kuharisha damu pamoja na Kipindupindu.

“ Watoto wapatao elfu 5,000 hupoteza maisha kila siku Duniani kote kutokana na ukosefu wa maji safi na salama. Halkadhalika Mtu Mmoja kati ya Watu 10 Duniani kote hawapati maji safi na salama “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi  lazima wajenge tabia ya kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa vianzio vya maji kwa lengo la kulinda mazingira.

Alisema ugomvi mkubwa unaibuka na kuendelea katika maeneo tofauti nchini kati ya Serikali na baadhi ya Wananchi kutokana na ile tabia ya watu wachache kuamua kujenga nyumba za makaazi katika vianzio vya maji.

Aliwapongeza Wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu kwa ustahamilivu wao wa muda mrefu ambao ulipelekea kukosa huduma za maji na kulazimika kutumia muda wao mrefu uliopaswa kuuelekeza katika kazi za maendeleo na kutafuta maji ambao mengine sio salama.

Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya mradi wa maji safi na salama katika Kisiwa cha Tumbatu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Mkaazi, Maji na Nishati Zanzibar Nd. Ali Khalil Mirza alisema mradi huo utatoa fursa ya kuhudumia Wananchi wa Kisiwa hicho wapatao elfu 8,252.

Nd. Mirza alisema mradi huo utakaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni moja katika awamu zote mbili uliolenga kuwakomboa Wananchi hao uligharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali za Marekani na Iran.

Alieleza kwamba ujenzi wa mradi huo ulioanzia kwa hatua ya uchimbaji  wa visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha Maji Lita Laki 250,000  katika Vijiji vya Tingatinga na Pale ulienda sambamba  na ulazaji wa Mabomba  yenye  urefu wa Kilomita 8.25.

Katibu Mkuu huyo wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati alifahamisha kwamba awamu ya kwanza ya mradi huo tayari imeshatumia zaidi ya shilingi Mia 636.7 Milioni wakati ile iliyobakia inatarajiwa kutumia shilingi Milioni 400.

Mapema  akisoma  Risala ya Wananchi wa Kisiwa hicho Katibu Tawala wa Wilaya ndogo ya Tumbatu Ndugu Khatib Habib Ali alisema kukamilika kwa mradi huo wa maji safi na salama kutawapunguzia usumbufu wa kupata huduma hiyo hasa akina Mama.

Nd. Khatib alisema Wananchi wa Shehia zote nne zilizomo ndani ya Kisiwa cha Tumbatu wanathamini juhudi kubwa za Viongozi wao ambazo ni kichocheo cha kasi katika kuelekea kwenye  Maendeleo.

Katibu Tawala huyo wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu aliuomba Uongozi pamoja na wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kuhakikisha kwamba awamu ya Pili iliyobakia ya mradi huo inakamilika kwa wakati uliopangwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.