Habari za Punde

Tanzania yataka iachiwe fursa ya kupanga na kuchagua miradi ya maendeleo

Dr. Babatunde Osotimehin, Mkurugenzi  Mtendaji wa UNFPA akiwasilisha taarifa yake mbele ya wajumbe wa Bodi ya UNFP, anaonekana Balozi Tuvako Manongi akifuatilia kwa karibu taarifa ya  mtendaji huyo  aliyoitoa mwanzoni mwa mkutano kabla ya wajumbe wengine kupewa fursa ya kuchangia.Balozi Tuvako Manongi , Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  akizungumza wakati wa mkutano wa Bodi ya  Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi  ya Watu ( UNFPA) uliofanyika siku ya  jumatano ukiwa ni mwendelezo wa mikutano ya Bodi za UNDP. UNOPS, na  UNICEF. Katika mchango wake Balozi  ametoa wito kwa washirika wa  maendeleo kuwapa nafasi  watendaji wa serikali kupanga na kuchagua miradi ya maendeleo. Pamoja naye ni  Maafisa wa  Uwakilishi, Bw. Songaliel Shilla,  Bi. Lilian Mukasa na Bi. Ellen Maduhu.   Meza Kuu  akiwamo    Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dr. Babatunde Osotimehin wakimsikiliza  Balozi  Tuvako  Manoni,  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa wakati  ambapo pamoja na mambo  mengine amesisitiza dhana ya uwajibikaji wa pamoja  kati ya serikali na washirika wa maendeleo

 Sehemu wa Wajumbe wa mkutano wa  Bodi ya  UNFPA, mkutano ambao pia  umepitisha Taarifa za  Baadhi ya Nchi ( Country Report)Tanzania ikiwamoNa Mwandishi Maalum,   New York

Tanzania  imetoa wito  kwa washirika   wa maendeleo yakiwamo  Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuiachia nafasi  ya  kupanga na kuchagua miradi yake ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vyake.

Wito  huo  umetolewa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, katika  siku ya pili ya  Mkutano wa  Bodi za Mifuko na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambapo  katika siku hiyo ya Jumatano Mfuko wa Umoja wa Mataifa  wa Idadi ya Watu ( UNFPA) uliwasilisha  Taarifa yake  iliyobainisha mafanikio pamoja na changamoto  za utekelezai   mipango yake ya maendeleo.

Balozi Manongi, amewaeleza wajumbe wa Bodi hiyo,  ambayo Tanzania pia ni  miongoni wa wajumbe kwamba,  Tanzania inaamini kuwa  ushirikiano wa kweli ni ule ambao washirika   watazipatia mamlaka za serikali fursa ya kupanga na kung’amua vipa umbele vyake vya maendeleo.
 Katika mkutano huu pia iliwasilishwa  Taarifa  ya nane ya  Tanzania ( country progamu) ambayo inaainishia miradi itakayotekelezwa na UNFPA kwa kipindi cha   miaka mitano kuanzia 2016 hadi 2021.


Pamoja na kusisitiza  haja na umuhimu wa  mamlaka za kitaifa kuachiwa fursa ya kupanga na kuamua   miradi ya maendeleo,  Mwakilishi huyo wa Tanzania pia amebainisha  katika  mchango wake kwamba    suala la uwajibikaji  nalo linapashwa kuwa kwa pande zote.

Vile vile amesema ,  Tanzania ingependa  kusisitiza  juu ya  hoja ya  uwazi, uwajibikaji katika  ufadhili   na   uthibitisho wa  thamani  ( value for money) ya miradi  inayofadhiliwa na Mfuko huo.

Balozi Manongi amebainisha pia kwamba, tatizo la uendelevu wa miradi inayoazishwa na   washirika wa maendeleo ni moja ya changamoto  inayozikabili nchi nyingi. Na kuongeza kuwa  changamoto hiyo inakwenda mbali zaidi ya miradi inayofadhiliwa na UNFPA.

“Itakuwa jambo jema na la muhimu kama mafanikio tunayoyapata kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo si tu yanakuwa endelevu lakini pia  panakuwepo na  ushahidi wa mafanikio yake.”akasema Balozi

Kuhusu uwezeshwaji wa  taasisi mbalimbali za  kitaifa ikiwano zile zinazohusu  ukusanyaji na uchambuzi wa  takwimu, Tanzania imesema  haitoshi kwa Mashirika  ya  Kimataifa kutoa tu kasoro au mapungufu katika eneo hilo bila ya kuainisha namna gani ya  kusaidia kutatua kasoro hizo.

Na kwa sababu hiyo Tanzania  kwa kutambua umuhimu wa takwimu katika upangaji wa  miradi ya maendeleo na  mipango mingine,  ingepeza  kuona panakuwwepo na  ushirikiano wenye tija na wadhati  katika  eneo la  la uwezeshaji wa taasisi za kitaifa.

Akaongeza kwamba Serikali ya Tanzania  inashukuru  pale ambapo baadhi ya  wadau wa maendeleo wamekuwa wakisaidia katika eneo hili. Na kwamba mafanikio mengi ambayo  hata washirika wa maendeleo wanajivunia yamewezekana kutoka na  serikali kutoa ushirikiano wake.

Akizungumzia kuhusu  uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali  ya Tanzania na UNFPA, Balozi Manongi  pamoja na kueleza kwamba  tofauti na  huko nyuma hivi sasa   uhusiano huo sasa umeimarika licha ya kupitia changamoto  nyingi.

Akabainisha kuwa mazingira mazuri ya ushirikiano  kati ya pande hizo mbili yamesaidia katika utekelezaji na ufanikishaji wa miradi mbalimbali  ya maendeleo ikiwano  inayohusua masuala ya afya ya uzazi salama na  uzazi wa mpango,   udhibiti wa magonjwa kama vile ukimwi,     na  utoaji elimu mbalimbali kwa vijana iliwaweze kujitambua.


1 comment:

  1. Lazima wafadhili msimamie fedha hizi ziende kwa walengwa
    Miradi mingi hupelekwa kwenye wabunge wa CCM

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.