Habari za Punde

Waziri afanya mabadiliko vitengo vya Idara ya Uhamiaji

Waziri Charles Kitwanga (kushoto meza kuu), Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni (kulia meza kuu) na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji (kushoto) na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), wakati wa kikao katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wa kwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na wa kwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga ameagiza yafanywe mabadiliko makubwa katika Vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika Vitengo hivyo.


Mheshimiwa Kitwanga ametoa maagizo hayo leo wakati alipofanya kikao na Viongozi wa Idara ya Uhamiaji ambapo pia kilihudhuriwa na Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara. Kikao hicho kilifanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.



Katika kikao hicho, Mheshimiwa Kitwanga ameagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji walioko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.



Wengine watakaohamishwa ni kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.



Aidha ameagiza pia kuwa Wakuu wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, na pia wale wa Vituo vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine, na pia watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika Vituo hivyo.


Amesema hatua hii inayochukuliwa sasa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali.



Amesema katika kuisafisha Idara hii, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lakini lengo kubwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wale wasiowajibika.



Amesema kufuatana na utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka. Asilimia 15 inahusisha vitendea kazi wa mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia 5 ukabila na upendeleo.


Amewataka Viongozi na watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na waepuke vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji haramu na wauza madawa ya kulevya.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
23 Februari, 2016


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) akizungumza na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji nchini (kushoto) pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wakwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya akizungumza jambo katika kikao kazi alichokiitisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) kuzungumza na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji nchini pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara yake, kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli.

Kaimu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Victoria Lembeli (wapili upande wa kushoto) akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) kuhusu masuala mbalimbali ya kikazi ndani ya Idara yake katika Kikao kazi cha Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kilichoitishwa na Waziri Kitwanga na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wakwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, balozi Simba Yahya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.