Habari za Punde

Huduma za afya zaimarika kutokana na juhudi za Serikali

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiufungua Mkutano wa Kumi wa Tathmini ya mapitio ya Sekta ya Afya kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein unaofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beacha Resort Mbweni.
  Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi akitoa maelezo ya ufafanuzi kwenye Mkutano wa Tathmini ya mapitio ya Sekta ya Afya hapo Zanzibar Beach Resort Mbweni.

 Mwakilishi wa Taasisi na Mashirika Hisani ya Kimataifa yanayotoa huduma za afya Nchini Tanzania Dr. Christin Harmel akitoa salamu kwenye Mkutano wa Tathmini ya mapitio ya Sekta ya Afya.

Naibu Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo akijiandaa kumkaribisha Mgeni rasmi kuufungua Mkutano wa Tathmini ya mapitio ya Sekta ya Afya.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kumi wa Tathmini ya mapitio ya Sekta ya Afya wakifuatilia Hotuba na ufunguzi wa Mkutano huo iliyotolewa na Balozi Seif  akimuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Shein.

 Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kumi wa Tathmini ya mapitio ya Sekta ya Afya wakifuatilia Hotuba na ufunguzi wa Mkutano huo iliyotolewa na Balozi Seif  akimuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Shein.
  Balozi Seif akisalimiana na Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Dunia unaoratibu maradhi ya ukimwi, malaria na kifua kikuu Zanzibar  { Zanzibar Global Fund Country Coodinating Mechanism – ZGFCCM } Bibi Benedict Maganga.
Kati kati yao ni Naibu Waziri wa Afya  Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo na kulia ya Balozi  Seif ni Katibu Mkuu Wizara hiyo Dr. Saleh Mohammed Jidawi.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa mashirika na taasisi za Kimataifa na zile za kitaifa zinazotoa huduma ya Afya Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema kwamba  juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali na Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha  miundombinu ya sekta ya Afya zimepelekea kuboreka zaidi kwa huduma za afya katika maeneo mbali mbali Mijini na Vijijini.

Alisema ujenzi wa Hospitali kubwa za Rufaa katika Miji Mikuu ya Visiwa vya Unguja na Pemba  pamoja na kuimarika  kwa zile Hospitali za Wilaya ni hatua nzuri itakayotoa fursa nzuri kwa Wananchi kupata huduma  za uhakika  za afya bila ya usumbufu.

Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akiufungua Mkutano wa Kumi wa Siku Mbili unaozungumzia tathmini ya mapitio ya pamoja  ya Sekta ya Afya katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi unaofanyika  katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya Mjini Zanzibar.


Alisema hatua zimeanza kuchukuliwa pia katika kuimarisha huduma za  msingi za afya  kupitia mradi maalum uliobuniwa na Serikali Kuu na kuungwa mkono na mashirika ya maendeleo ya Orio la Nchini Uholanzi la lile la Danida kutoka Nchini Denmark.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifahamisha kuwa hatua hii ina lengo la kuona huduma za Afya zinapatikana kwa wananchi si zaidi ya Kilomita Tano karibu na maeneo wanayoishi hasa Vijijini.

Hata hivyo Dr. Shein alieleza kwamba ujenzi wa majengo mapya  ya afya na uwepo wa vifaa bora vya matibabu hautatimia iwapo mipango ya muda mfupi na mrefu haitawekwa katika kuwapatia taaluma ya kisasa watendaji wa sekta hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Alisema Ndani ya kipindi cha tathmini ya Sekta ya Afya Serikali Kuu tayari imeshaajiri wafanyakazi katika sekta hiyo wapatao 2,000 sambamba na ongezeko na madaktari wazalendo waliopata taaluma yao kupitia ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chuo Kikuu cha Mantazas cha Nchini Cuba.

Akigusia upatikanaji wa dawa mbali mbali Rais wa Zanzibar Dr. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuongeza bajeti kutoka shilingi Bilioni 1.0 mwaka 2012/2014 hadi shilingi Bilioni 4.3 mwaka 2015/2016 ili kukabiliana na upungufu wa huduma hiyo.

Dr. Sein aliishauri Wizara ya Afya kuendelea kusimamia vyema mipango mizuri iliyokwishaiweka ikiwemo ile inayopata ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo ambayo itawawezesha watendaji wa sekta hiyo kutoka huduma kitaalamu zaidi.

Rais wa Zanzibar Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na kujali misaada yote inayotolewa na Mataifa mbali mbali Duniani  kupitia washirika wa Maendeleo pamoja na Taasisi Binafsi kwa kuunga mkono jitihada za Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya afya.

Dr. Shein alisema alisema mbali ya misaada hiyo lakini nguvu za uungaji mkono inayoendelea kutolewa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa kubwa na chachu ya kufanikiwa vyema kwa sekta hiyo Nchini.

Aliwataka washiriki wa Mkutano huo  wa Kumi wa mapitio ya pamoja  ya Sekta ya Afya wakiwemo Madaktari waliobobea, wataalamu wa masuala ya mazingira wa ndani na nje ya nchi kutumia nafasi yao kitaalamu katika kupitia tathmini ya mapitio hayo ya sekta ya afya na kutoa ushauri pamoja na muongozo katika sekta hiyo.

Alisema Serikali Kuu kupitia Wizara inayosimami sekta ya Afya itahakikisha kwamba ushauri na muongozo huo unapewa kipaumbele  katika kuona huduma za afya nchini zinaimarika nakufikia kiwango kinachokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Mapema Mwakilishi wa Taasisi na Mashirika Hisani ya Kimataifa yanayotoa huduma za afya Nchini Tanzania Dr. Christin Harmel alisema Taasisi hizo zimeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika jitihada zake za uimarishaji wa huduma za Afya.

Dr. Christin alisema hudujma za afya ya msingi lazima ziendelee kuimarishwa ili kuwa na jamii yenye afya na uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji mali utakaosaidia uchumi wa Taifa.

Alisisitiza watendaji wa Afya kuhakikisha kwamba kila motto anayezaliwa mikononi mwao ni lazima alindwe, ahifadhiwe na kutunzwa katika mazingira bora yatakayomuwezesha kukua kwa amani na upendo.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuufungua Mkutano huo Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo aliyashukuru Mashirika na Taasisi za Kimataifa na zile za Kitaifa kutokana na mchango wo mkubwa ulioiwezesha Wizara ya Afya kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Mh. Mahmoud alisema  hatua hii ya ushirikiano wa pamoja katika kujenga miundombinu ya Sekta ya Afya imesaidia kujenga Jamii yenye afya inayoweza kujenga uchumi imara wa Taifa na kunufaisha wananchi walio wengi.

Alieleza kwamba upo uhusiano mpana  kati ya Sekta ya Afya na Taasisi zinazosimamia uchumi wa Nchi kupitia sera  maalum inayoonyesha muelekeo wa ufanisi katika kuelekea  kwenye maendeleo yanayotokana na pande hizo mbili shirika.

Alisema zipo nchi nyingi Duniani hasa zile za Bara la Asia zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo baada ya kuamua kuimarisha kwamba miundombinu ya Sekta ya Afya  na kuwafanya wananchi wake kuwa na afya bora ya kufanya kazi.

Mkutano huo wa Kumi wa siku mbili unaozungumzia tathmini ya mapitio ya pamoja  ya Sekta ya Afya Zanzibar  ulioshirikisha Wataalamu na Washirika wa Maendeleo kutoka Taasisi za Kimataifa na Kitaifa umefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu { UNFPA } kwa kushirikiana na Seriali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.