Habari za Punde

Spika wa Baraza la Wawakilishi Awaapisha Wajumbe Walioteuliwa na Rais leo.

Ali Issa Maelezo, Zanzibar.
Mwakilishi mteule wa Chama cha Alliance for Development Change (ADC) Hamad Rashid Mohammed, amemuomba Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, atakapounda serikali achague watendaji wenye utaalamu wanaoweza kuisaidia serikali kuinua uchumi wake.

Akichangia hotuba ya Rais baada ya kuapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Rashid amesema kupewa nafasi kwa wataalamu kutaisaidia serikali kufikia malengo inayojipangia kwa kuwaletea maendeleo wananchi.

Mwakilishi huyo aliyegombea urais wa Zanzibar kupitia ADC katika uchaguzi mkuu uliopita, amesema katika kipindi cha pili cha awamu ya saba, Dk. Shein anahitaji wataalamu wachumi na watakaotumikia nchi kwa uadilifu.

Aidha, alisisitiza vyombo vya sheria vitumie nafasi yao dhidi ya watendaji na viongozi watakaokiuka sheria na kujaribu kuikwamisha serikali kutimiza malengo yake.

Aliiomba serikali iache muhali kwa kulea watendaji wasiotimiza majukunmu yao ipasavyo, akisema ni lazima watu kama hao wachukuliwe hatua madhubuti vyenginvyo nchi itarudi nyuma kimaendeleo.

Rashid alieleza kuwa, kinachokwamisha nchi kupata maendeleo ni watendaji na viongozi wengi kutojali wakati na kupoteza muda mwingi kwa mambo yasiyokuwa ya msingi badala ya kufanya kazi.

“Tumeshuhudia watu wengi wakkinyimwa au kucheleweshewa huduma wakiwemo wawekezaji wanaoomba miongozo. Hili ni tatizo na lazima tufike wakati likomeshwe,” alisisitiza.

Aliitaka serikali kuiga mfano wa Tanzania Bara, ambapo amesema mtu anayeomba huduma hupangiwa mtendaji maalumu wa kumsaidia, na pia hujulishwa mapema tarehe atakayomaliziwa mchakato wake na kupewa majibu au kutumiwa kokote aliko.

Kwa upande mwengine, aliitaka serikali iwe makini katika kusimamia ukusanyaji wa mapato kwani kodi ndio msukumo wa kuharakisha maendeleo.

Mhe.Rashid aliwataka wananchi waondokane na fikra za kutegemea misaada kutoka nchi za nje, na badala yake wakaze buti katika kufanya kazi za uzalishaji na huduma kwa kutumia rasilimali zilizomo nchini.

Kwa upande wake,Mhe.Mohammed Aboud Mohammed ambaye pia ni mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, amewaomba wajumbe wenzake waache siasa kwani  uchaguzi umekwisha na kilichobaki sasa ni kujenga nchi.

Amefahamisha kuwa katika suala la maendeleo, si vyema kuingiza itikadi za kisiasa, dini, ukabila au maeneo watu wanakotoka kwani Zanzibar ni nchi ya Wazanzibari wote.

Aidha aliwataka wananchi wawe watulivu, wavumilie na kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.