Habari za Punde

Balozi Seif Awaambia Wananchi wa Jimbo Lake Changamoto zao Zinapata Ufumbuzi wa Kudumu Hatua kwa Hatua.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi vifaa vya ujenzi Mwenyekiti  wa CCM Tawi la Kitope Kichungwani Nd. Suleiman Fadhil kukamilisha ujenzi wa Tawi hilo.
Balozi Seif na Timu yake walikuwa katika ziara ya kushukuru wapiga kura wa Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo la Mahonda baada ya kupewa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Balozi Seif akiusisitiza Uongozi wa Tawi la CCM Kitope Kichungwani kumaliza haraka ujenzi wa Tawi lao ili liendane na hadhi ya chama chao.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif akikagua harakati za Ukamilishaji wa rangi katika  Ofisi ya CCM Tawi la Kitope “B” alipofanya ziara ya Timu yake katika kuwashukuru wapiga kura wao.
Balozi Seif  akibadilishana mawazo na wanachama wa chama cha Mapinduzi wa Tawi la CCM Kitope “B” baada ya kukagua harakati za ukamilishaji wa rangi wa Tawi hilo.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis OMPR.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema nia ya Viongozi wa Jimbo hilo wakati wakiomba ridhaa ya kutaka kuitumikia jamii ni kuona changamoto zinazowakabili wananchi katika mitaa ya Jimbo hilo zinapata ufumbuzi wa kudumu hatua kwa hatua.

Akiiongoza Timu ya Viongozi wenzake waliochaguliwa kuliongoza Jimbo la Mahonda katika kipindi cha miaka Mitano ijayo Balozi 
Seif alisema  hayo wakati wakiendelea na ziara zao za kutoa shukrani kwa Wananchi na wanachama wa CCM wa Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo hilo kwenye mikutano tofauti.

Balozi Seif Ali Iddi alisema Awamu ya kwanza katika utekelezaji wa ahadi waliyoitoa wakati wa kuomba kura na ilani ya CCM ndani ya Jimbo hilo itazingatia kipaumbele cha kusimamia huduma za upatikanaji wa maji safi na salama.  

Alisema kipaumbele hicho ambacho ni muhimu katika ustawi wa jamii kitasaidia kuwaondoshea usumbufu wananchi wanaoendelea kukosa huduma hiyo hasa akina mama ili wapate muda zaidi wa kuelekeza nguvu zao katika shughuli za miradi ya maendeleo.

Akigusia huduma za umeme zinazoongeza kasi ya kuchumi na kuwakomboa Wananchi walio wengi Balozi Seif alisema sekta hiyo bado ina gharama kubwa katika upatikanaji wake kiasi kwamba wananchi walio wengi hasa Vijijini wanashindwa kuigharamia.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliwaeleza Wananchi na wana CCM hao kwamba Uongozi wa  Jimbo hilo tayari umeshafanya mazungumzo na Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo.

Balozi Seif  na Timu yake aliridhika na hatua iliyofikiwa ya uimarishaji wa Ofisi za CCM katika Matawi ya Kitope Kichungwani, Kinduni pamoja na Kitope “B” iliyofanywa na Wana CCM hao kazi iliyomfanya kuhamasiska na kuamua kusaidia vifaa vya ujenzi ili kukamilisha ujenzi wa matawi hayo.

Akikabidhi Vifaa hivyo pamoja na matengenezo  ya jumla yenye gharama ya shilingi Milioni 11,700.000/-  vikiwa  ni pamoja na saruji, mchanga, Kokoto, Nondo, Rangi pamoja na fedha za mafundi alisema Ofisi hizo lazima zilingane na hadhi ya Chama chao.

Naye Mke wa Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi  aliwakumbusha wana CCM kuendelea na sera yao ya kuiheshimu amani iliyopo Nchini ambayo ndio dira inayotowa fursa kwao na wananchi wote kuendelea na harakati zao za kimaisha.

Mama Asha alifarajika na kusema kwamba hakuna mwana chama wa chama cha Mapinduzi anayeweza kufanya hujuma ambazo ana uhakika matokeo yake zinaweza kuleta maafa katika jamii inayowazunguuka.

Mapema Diwani wa  Wadi ya Mahonda Nd. Haji Fadhil Mkadam na Bibi Hadia Juma Chum wa Wadi ya Fujoni, Wadi zinazounda Jimbo la Mahonda walisema lengo la ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni kazi zake zimeanza rasmi.

Madiwani hao kwa pamoja wamewaeleza  Wananchi  na Wana CCM hao kwamba kinachohitajika kwa wakati huu ni kuimarishwa kwa ushirikiano wa pande zote husika kati ya viongozi na wananchi  wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.