Na Majid Omar Najim
Waziri
wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Mhe. Amina Salum Ali amevitaka vyombo
vinavyosimamia Sheria kuhakikisha Sheria ya Maendeleo ya Karafuu inatumika
ipasavyo ili uwepo wake uweze kuleta tija kwa wakulima na Taifa.
Alisema
Baraza la Wawakilishi limekamilisha wajibu wake wa kutunga sheria hiyo hivyo
sio sahihi kuwa sheria hiyo isitumika ipasavyo. Alisema vitendo vya makusudi
vya hujuma dhidi ya Sekta ya Karafuu haviwezi kufumbiwa macho na lazima Sheria itumike
ili kutoa haki inayostahiki.
Aliyasema
hayo wakati akifunga semina ya mafunzo ya siku moja ya kuwafahamisha wasimamizi
wa Sheria- Jeshi la Polisi, Wapelelezi na Mahakimu kuhusu Sheria No. 2 ya
Maendeleo ya Karafuu ya mwaka 2014 iliyofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Ocean
View, Kilimani Zanzibar.
Alitolea
mfano tukio la uchomaji moto wa mashamba ya mikarafuu uliotokea katika Shehia ya Mzambarauni Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini
Pemba, ambapo mikarafuu 151 iliteketea kwa moto na kusema vitendo kama hivyo
vinatokana na usimamizi duni wa Sheria hiyo.
Alisema kuwa iwapo wadau wa sekta hiyo hasa
wasimamizi wa Sheria likiwemo Jeshi la Polisi, Wapelelezi wa Makosa, Mahakimu
na Wanasheria wataitendea haki Sheria hiyo basi Sekta ya Karafuu itakuwa ni
faraja kubwa kwa wakulima wa zao hilo.
“Nimeisoma vizuri Sheria hii, nimeiona imeweka misingi
imara ya haki, kama itafanyiwa kazi kwa vitendo basi hakuna shaka zao la karafuu
litabadilisha hali ya uchumi wa Zanzibar”. Alifahamisha Mhe. Amina.
Akifungua Mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu
Zanzibar Rabia Husein Mohamed alisema Sheria ya Maendeleo ya Karafuu imetungwa
kwa ajili ya kulinda maslahi ya wakulima na wananchi wanaojishughulisha na zao
la karafuu pamoja na wadau wengine wote.
“Sheria hii ni msingi imara wa kuijenga na kuiimarisha
Sekta hii ya karafuu katika mazingira yote, maendeleo ya Zanzibar na ustawi wa
wakulima wa zao la karafuu, wananchi wanaojishughulisha na biashara ya karafuu na
wadau wote wenye maslahi ya moja kwa moja au kupitia kwa njia nyengine za
kujenga uchumi wa nchi wanamatumaini makubwa na Sheria hii”. Alifahamisha Mhe,
Rabia.
Aliwasisitiza wasimamizi wa Sheria kutekeleza
wajibu wao kwa kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa pande zote na hakuna
anaedhulumiwa katika utekeleji wa Sheria hiyo, na pale penye utata suluhisho lifanyike
mara moja ili isije kuleta athari ya kutotendeka haki kwa wahusika.
Akiwasilisha Sheria hiyo No. 2 ya Maendeleo ya
Karafuu Katibu wa Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) Ali Hilali
Vuai aliainisha makosa yaliyoanzishwa na Sheria hiyo na kanunui zake kuwa ni
kuhujumu mkarafuu kwa aina yoyote, kuchafua karafuu kwa makusudi na kuanika
karafuu isivyotakiwa.
Akiwasilisha tathmini ya Zao la Karafuu Zanzibar mtaalamu
wa Kilimo kutoka Wizara ya Misitu na Maliasili Badru Kombo Mwamvura alisema
Sekta ya Kilimo cha Karafuu inakabiliwa na changamoto nyingi hivyo Sheria hiyo inahitaji
ifanyiwe kazi ipasavyo ili kukabiliana na changamoto hizo.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uharibifu
wa Mikarafuu kwa makusudi, ukatajaji wa mikarafuu, wizi wa karafuu, ujenzi na
uchimbaji mchanga ndani ya mashamba ya mikarafuu.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki kutoka vyombo
vya kusimamia Sheria walisema ili Sheria hiyo iweze kutimiza lengo la kuundwa
kwake lazima kuwepo kwa ushirikiano mkubwa baina ya Polisi, Mahakama na Waendesha mashtaka.
Mwanasheria Mfawidhi kutoka Afisi ya Mwendesha
Mashtaka (DPP) Zanzibar, Suleiman Haji Hassan alisema kesi nyingi zinazotokana
na karafuu zimekuwa hazifiki katika mamlaka husika kutokana kutowajibika
ipasavyo kwa baadhi ya taasisi za Kisheria.
“Nina kumbukumbu ya kesi moja tu iliyotufikia, hii
inaonesha ni jinsi gani hakuna ufuatiliaji wa kesi hizi, na hata pale
zinapofuatiliwa basi huwa zinaishia kuamuliwa kienyeji ”.Alibainisha.
No comments:
Post a Comment