STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.05.2016

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi,Mhe. Issa Haji Ussi Gavu, amemtumia salamu za rambi rambi Waziri
anayeshughulikia Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Yusuf bin Alawi bin Abdullah kufutia
kifo cha Balozi mdogo wa Oman aliyopo Zanzibar Mhe. Ali Abdallah Al-Rashid.
Katika salamu hizo za
rambi rambi, Waziri Gavu alisema kuwa amepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa ya kifo
cha Balozi Ali Abdallah Al-Rashid kilichotokea
hivi karibuni hapa Zanzibar.
Kwa niaba ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wote wa Zanzibar, alitoa salamu za
rambirambi kwa ndugu, jamaa na wananchi wote wa Oman kufuatia msiba huo mkubwa.
Aidha, salamu hizo za
rambirambi zilieleza kuwa Wazanzibari watamkumbuka sana Balozi Ali Abdalla
Al-Rashid kwa juhudi zake za kuuendeleza na kuuimarisha uhusiano wa kihistoria
uliopo kati ya Zanzibar na Oman.
“Nakuhakikishia Mhe.
Waziri kwamba sote tupo pamoja na wanafamilia pamoja na wananchi wote wa Oman
katika kipindi hiki kigumu cha msiba”, zilieleza salamu hizo.
Pamoja na hayo, salamu
hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Balozi Ali Abdalla Al-Rashid
mahali pema peponi. Amin.
Balozi Ali Abdallah
Al-Rashid alifariki dunia katika hospitali ya Global hapa Zanzibar baada ya kukabiliwa na
shindikizo la damu na baada ya kifo chake mwili wake ulisafirishwa kuelekea
nchini Oman kwa ajili ya mazishi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment