Habari za Punde

Shirika la Milele Foundation kushirikiana na Serikali ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wanananchi

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Viongozi wa Shirika la Milele Zanzibar Foundation {MZF} na Jumuiya ya misada ya Kijamii Zanzibar { ZAHCO } Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Milele Zanzibar Foundation Bwana Yousuf Luiz Caires aliyepo kati kati akimueleza Balozi Seif Mikakati ya Taasisi yake katika kusaidia miradi ya maendeleo ya Jamii Nchini.

Wa kwanza kutoka kushoto ni Bibi Khadija Ahmed Sharif Mtendaji wa Milele Tawi la Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi cheti Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Milele Zanzibar Foundation Bwana Yousuf Luiz Caires kwa kazi nzuri iliyofanywa na Taasisi hiyo katika kusaidia miradi ya Jamii nchini.

Wa kwanza kutoka kushoto ni Bibi Khadija Ahmed Sharif Mtendaji wa Milele Tawi la Zanzibar.

 Wa kwanza kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya inayopjishughuilisha na Misaada ya Jamii Zanzibar { ZAHCO } Bwana Said Mohammed Mayugwa, Bwana Kassim Mbarouk Juma wa Milele Zanzibar na Bwana Salum wa Jumuiya ya Misaada ya Jamii Zanzibar.

Balozi Seif akiagana na Katibu Mkuu wa Jumuiya inayojishughuilisha na Misaada ya Jamii Zanzibar { ZAHCO } Bwana Said Mohammed Mayugwa baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Shirika lisilo la Kiserikali la Milele Zanzibar Foundation          { MZF } limeahidi kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Taasisi nyengine nchini katika kuona changamoto zinazowakabili wananchi hasa huduma za Elimu, Afya na Maji zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo lenye Makao Makuu yake Mjini Dubai katika Nchi za Falme za Kiarabu { UAE } Bwana Yousuf Luiz Caires alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.


Bwana Yousuf  Luiz Caires akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Shirika la Milele wa Tawi la Zanzibar alisema Taasisi hiyo iliyoanzishwa Mwezi Januari mwaka 2014 imejikita kuwa karibu zaidi na wadau wa sekta zinazowagusa moja kwa moja wananchi katika kusaidia nguvu kiuwezeshaji na Taaluma.

Alisema watendaji wa Milele Zanzibar Foundation wapatao 16 wamejipanga kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuzingatia mahitaji halisi ya sehemu husika.

“ Tumejipanga kuwa karibu zaidi na watendaji wa sekta za Elimu, Afya na Huduma za Maji salama ili kuona maeneo ya wananchi yatakayohitaji kupata msukumo wa msaada kwenye miradi yao ”.
 Alisema Mkurugenzi huyo Mkuu wa Milele Zanzibar Foundation.

Bwana Yousuf alieleza kwamba mipango mengine pia imeshandaliwa katika kuwawezesha wananchi hasa wakulima wa kilimo cha Mwani na mazao mengine ya biashara ili watekeleze miradi yao kitaalamu ili ilete tija kwa kupunguza umaskini na kuongeza kipato.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya inayojishughulisha na misaada ya Jamii Zanzibar { ZAHCO } Bwana Said Mohammed Mayugwa alisema Taasisi yake iko tayari kushirikiana na Shirika la Milele katika kutoa huduma za pamoja kwa Wananchi.

Bwana Said alisema tasisi hizo mbili zina malengo yanayofanana jambo ambalo watendaji wake wanapaswa kuwa karibu katika kubadilishana taaluma, uzoefu pamoja na wataalamu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema amevutiwa na kazi kubwa inayofanywa na Shirika la Milele Zanzibar Foundation pamoja na Jumuiya ya Misaada ya Jamii Zanzibar katika kutoa huduma za Kijamii hapa Nchini.

Balozi Seif alisema uamuzi wa Taasisi hizo mbili wa kusaidia miradi ya maendeleo ya Wananchi ni wa msingi kutokana na changamoto nyingi zinazowakumba Wananchi wanaofikia maamuzi ya kujitatilia matatizo yao kwa kuanzisha miradi tofauti.

Alisema licha ya uhaba wa Vikalio vya Wananfunzi katika Sekta ya Elimu kwenye maskuli mbali mbali nchini lakini Karne ya 21 ya Sayansi na Teknolojia haistahiki wanafunzi wake kuendelea kukaa chini.

Hatua za msingi zinapaswa kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi na mashirika hisani ya Maendeleo ndani na nje ya nchi katika kukabiliana na changamoto zinazowakumba Wananchi kwenye maeneo tofauti Nchini.

Akigusia Sekta ya Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe wa Watendaji hao wa Milele Zanzibar Foundation na ule wa Jumuiya ya Misaada ya Jamii kwamba Serikali inaendelea na mikakati ya kuimarisha miundo mbinu ya Sekta hiyo ili kuwawezesha Wananchi kupata huduma bora za Afya.

Balozi Seif alisema uamuzi wa Taasisi hizo kusaidia Sekta hiyo unakwenda sambamba na ile azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Vituo vya Afya katika umbali usiozidi Kilomita Tano.

Shirika la Milele Zanzibar Foundation { MZF } mwishoni mwa mwaka 2015 tayari limeshasaidia kukamilisha ujenzi wa Skuli Mpya ya Msingi ya Mahuduthi iliyomo ndani ya shehia ya Mkungu Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kuisni Pemba.

Ujenzi wa skuli hiyo umegharimu jumla ya shilingi Milioni 300,000,000/- ambapo kati ya hizo shilingi Milioni 14,000,000/- ni nguvu za Wananchi na zilizobaki zimebebwa na Uongozi wa shirika hilo la Milele Zanzibar Foundation.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.