Habari za Punde

Tatizo la ajira bado ni changamoto kwa vijana

Na Miza Kona Maelezo 

Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Ameir Ali Ameir amesema tatizo la ajira nchini bado ni changamoto kubwa kwa vijana kutokana vijana wengi kukosa sifa za  kuajiriwa na baadhi yao  kuchagua  kazi za kuajiriwa.

Hayo ameyasema leo katika Ukumbi wa Kidongochekundu wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Kuwajengea Uwezo wa Kamati za Ajira za Wilaya za Mjini na Magharibi.

Amesema vijana ndio nguvu kazi katika jamii hivyo wana nafasi kubwa katika kulitumika Taifa kwa  kufanya kazi lakini mtazamo wa vijana bado ni tatizo  na baadhi wamejenga tabia ya uvivu unaopelekea kuwepo kwa vijana wengi wanaomaliza masomo  wakiwa wazururaji wasio na ajira.

Mkurugenzi huyo amezitaka kamati za ajira kujipanga vizuri kuyafuatilia matatizo yanayowakabili vijana kupitia vigezo vyao, masheha, waajiri, mtazamo pamoja Utamaduni wao ili  kuwanusuru kujiingiza katika vikundi viovu.

“NI kazi ya kamati kupita kwa waajiri ili kuangalia Changamoto, mafanikio attitude na Utamaduni kwa vijana pia unaweza kufahamu matatizo ya vijana kupitia vigezo vyao pia wazee wana nafasi gani katika kuwasaidia vijana,” alifahamisha Mkurugenzi Ameir.

Aidha amezifahamisha kamati hizo kutafuta taarifa yakinifu kwa vijana  ili kupata kujua matatizo ya ajira yanayowakabili  na kuweza kuwasaidia na kuwaingiza katika soko la ajira.

Ameeleza kuwa  vijana wanahaki ya kupata kazi yenye heshima inayoendana na mazingira bora ambayo yatamjenga kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kumpatia kipato cha kujikimu kimaisha na kuondokana na utegemezi.


Akiwasilisha Mada ya Mpango Kazi wa Ajira kwa Vijana Afisa Ajira Kutoka Idara ya Ajira Mustafa Hassan Makame amesema serikali imeweka mikakati mbali mbali ili kuhakikisha inakabiliana na tatizo la ajira na kuona kwanba  tatizo hilo linapungua nchini.

“Ujasiri amali ni njia  ya kutatua tatizo  la ajira kwa vijana na sio ajira za serikali peke yake hivyo vijana wana nafasi kubwa ya kujiajiri wenyewe,” ameeleza afisa huyo.  
Nae Mtaalamu kutoka Shirika la Kazi Duniani Edmund Mushy amesema serikali pekee haiwezi kulitatua tatizo la ajira  kwa vijana  ni lazima pawepo  mashirikiano na wadau wengine ikiwemo sekta binafsi na  taasisi  nyngine kwani nao wana mchango mkubwa katika kukuza ajira nchini.

Wakichangia mada washiriki wa mafunzo hayo  wameiomba wizara kuweka mratibu wa ajira katika Wilaya  zote atakaeshughulia masuala ya ajira ili kuondosha usumbufu uliopo katika wilaya hizo na kamati ziweze kufanya kazi walizopangiwa kwa ufanisi.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.