Habari za Punde

ZSSF Kulikarabati upya Jengo la Chawal Building ( Jumba la Treni)

MFUKO WA HIFADHI YA JAMII ZANZIBAR (ZSSF)

Taarifa kwa umma

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inawajali wananchi 

wake kwa kuona wanaondokana na hali yeyote hatarishi 

ambayo itawasababishia madhara au vifo.

Moja ya hatua yake ni kuepusha majanga na ajali 

zinazoweza kuepukika.

Katika harakati zake hizo, ni muda mrefu imetoa tahadhari 

kwa wananchi wanaoishi katika nyumba kongwe za mji 

mkongwe ambazo zinaonekana kuwa katika hali mbaya kwa wakaazi wake na wapita njia.

‘Chawal Building’ maarufu jumba la treni lilioko darajani ni 

moja kati ya nyumba ambazo ni miaka zaidi ya miwili sasa 

Smz imewataka wanaoishi humo kuondoka kutokana na 

uchakavu wa jumba hilo lenye zaidi ya miaka 100!!!

Mbali ya wakaazi hao kutoondoka; kwa sasa serikali 

imeshatilia nguvu amri yake hiyo ili kuwanusuru wakaazi hao 

na janga lolote la kuanguka jumba hilo lakini pia hata wapita 

njia karibu na jengo hili. 

Kwa kuwa jumba hilo ni moja kati ya majengo yaliyoko 

katika urithi wa kimataifa chini ya unesco, na kusimamiwa na mamlaka ya hifadhi na uendelezaji wa mji mkongwe; Serikali kupitia ZSSF inadhamiria kulikarabati na baadae kuendelea kutumiwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kwa wafanyabiashara waliokuwemo kabla ya kukarabatiwa kwake.

Katika utekelezaji wa hilo tayari michoro imekamilika na 

hatua za kuiwasilisha Unesco zinaendelea ili kuelewa hatua 

hiyo na kupata baraka zao.

Hatua nyengine ya dharura ya kuepusha maafa kwa 

wananchi ni kulidhibiti eneo hilo kwa kulizunguushia uzio 

eneo lote ili kutotumika kabisa kwa shughuli zozote wakati 

matayarisho ya ujenzi yakiendelea.

Serikali ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa jumba la Chawal 

ilikaa mara nyingi na wafanyabiashara na wakazi wake 

kujadili hatma yao lakini pia ilitoa muda wa kutosha kwa 

wahusika hao kuhama ambapo muda wa mwisho ni tarehe 

05/06/2016.

Serikali na ZSSF inapenda kuchukua nafasi hii ya 

kuwashukuru wale walioanza kutekeleza agizo hilo lakini pia 

kupitia kwenu waandishi tunawakumbusha kuwa sasa muda 

umemalizika hivyo tunawaomba kutekeleza amri hiyo yenye 

faida kwa maisha yao na mali zao.


Tunawakumbusha wafanyabiashara waliokuwemo katika 

jumba hilo kuwa bado serikali haijabadilisha mtazamo wake 

kwao, kwa kuwapa kipaumbele kabisa cha kuwapangisha 

mara baada ya kukamilika ujenzi wake utaratibu muafaka.

Aidha katika kusaidia utekelezaji wa agizo la kuhama, zssf 

imetayarisha usafiri wa magari bila ya malipo wa kuwasaidia 

kuhamisha mali zao kwa kuzipeleka popote watakapo. hata 

hivyo usafiri huo ni kuanzia leo tarehe 03/06/2016 hadi 

tarehe 05/06/2016.

Tunaomba mashirikiano ya wakaazi, wafanyabishara 

pamoja na wananchi wote kwa ujumla ili kufanikisha ujenzi huo kwa faida yetu sote na urithi wa vizazi vijavyo.

Kwa pamoja tutaweza inshallah

IMETOLEWA NA
MKURUGENZI MWENDESHAJI
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII ZANZIBAR (ZSSF)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.