Habari za Punde

Mtanzania Atua Academy ya PSG Nchini Ufaransa.

Uongozi wa mabingwa watetezi wa Ligi ya Ufaransa, PSG umeamua kumvuta katika akademi ya klabu hio mshambuliaji chipukizi wa Tanzania, Haytham Saadun Hamoud.

Haytham mwenye umri wa miaka 17 amezaliwa na kukulia Tanzania katika jiji la Dar es Salaam. Anatumia pasi ya kusafiria ya Tanzania. Anaongea kwa kujiamini kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Safari yake ya soka ilianzia katika mpango wa kuzalisha vipaji wa klabu ya Mtibwa Sugar, baada ya hapo alielekea Oman ndipo wasaka vipaji wa PSG walipomuona

Ameiambia Soka360 kuwa alipata fursa ya kuonekana na makocha wa PSG kwenye mashindano maalum yaliyofanyika nchini Dubai.

” Wasaka vipaji wa PSG walivutiwa na uwezo wangu kwenye mashindano maalum nchini Dubai. Mimi pamoja na wenzangu wanne kutoka mataifa mbalimbali duniani tulichaguliwa kwenda kufanya majaribio. ”

“kwa kutambua umuhimu wa fursa hii adimu, na hasa walikuwa wakitaka mtu mmoja tu, nilipambana na hatimaye kufuzu moja kwa moja kujiunga na akademi ya PSG katika kundi la chipukizi walio chini ya umri wa miaka 18. ” Anasimulia Haytham.

Haytham anaongezea kuwa wakati wa majaribio kocha wa akademi ya PSG, Andy Gill, raia wa Uingereza alivutiwa mno na uwezo wake na kumtabiria kufika mbali kama akiendelea na bidii na umakini alionao.

” Kocha Gill aliniambia haoni sababu ya mimi kutofika mbali kutokana na kile alichokiona katika miguu yangu wakati wa majaribio. ”

Anafuatilia soka la Tanzania na kwenye upande wa wachezaji wanaocheza nchini, uwezo wa kiungo Salum Abubakar ‘ Sure Boy’ unamvutia sana.

” kuna wachezaji wengi tu wazuri wanaocheza nchini lakini binafsi navutiwa na Sure Boy, ni fundi na ninamuombea dua yeye pamoja na wenzake wafanikishe malengo yao.”

Licha ya kuwa na ndoto za kufanikiwa kucheza angalau moja ya ligi tano bora zaidi duniani, Haytham anasema anatamani kuja kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania siku za usoni.

” Najiendeleza niweze kufika mbali zaidi na kuweza kuja kulitumikia taifa langu. Naomba sana Mungu anilinde na mitihani ya dunia ilinifanikishe yaliyopo moyoni mwangu. ”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.