Habari za Punde

ZFA Yajivua Majukumu ya Kamati ya Kocha Msoma.

Na Mwandishi Wetu.

Katika kuhakikisha inapunguza majukumu na kuyatoa kwa wahusika, Kamati Tendaji ya Chama cha Mpira wa miguu Zanzibar, (ZFA) leo imekutana na kamati yake ya Ufundi kujadili maendeleo ya mchezo huo kwa msimu mpya wa ligi ulioanza Oktoba pili mwaka huu.

Kikao hicho cha leo ambacho pia kimehudhuriwa na viongozi wa Kamati ya Waamuzi kilikua chini ya Mwenyekiti wake Rais wa ZFA, Ndg.Ravia Idarous Faina majira ya saa nne asubuhi uwanja wa Amaan.
Masuala mengi ya michezo yalizungumzwa ikiwemo suala la ushirikiano kati ya kamati ya waamuzi na ile ya makocha ili kusiwepo mvutano hususan upande mmoja unapoonekana kwenda kinyume na majukumu yake.

Katika hali ya kufurahisha na isiyotarajiwa rais wa ZFA, aliamua kuwapa jukumu makocha hao la kuteuwa makocha wote watakaosimamia timu za taifa za Zanzibar kuanzia leo hii.

"Kuanzia leo hii jukumu la kuteuwa makocha wa timu zetu za taifa litakuwa juu yenu" alisema rais huyo.
Awali Kamati Tendaji ya ZFA ndiyo iliyokuwa ikipendekeza jina la mwalimu mkuu wa timu ya taifa pasipo hata kushirikisha kamati hiyo ya ufundi.

Kufuatia kauli hiyo kocha wa Black Sailor, Juma Awadhi Mohammed ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo alipongeza juhudi zinazofanywa na ZFA za kuhakikisha inajipunguzia majukumu na kuyatoa kwa wengine.

Mchakato huo wa Makocha utaanza kwa kuteuwa kocha atakayesimamia timu ya taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 sambamba na ile ya taifa ya Zanzibar Heroes zinazotarajia kushiriki mashindano ya Cecafa mwaka huu.

Kamati ya Makocha Zanzibar inasimamiwa na mwenyekiti wake Abdulghan Msoma anayefundisha klabu ya KVZ ambao ni makamu bingwa wa ligi kuu ya soka visiwani hapa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.