Habari za Punde

Eneo la Kijangwani soko la Mbao kugeuzwa kituo cha Daladala: Tuliliandika hili takrban miaka mitatu iliyopita

Tuliwahi kuliandika hili katika mtandao huu takriban miaka mitatu iliyopita Tujuikumbushe


http://www.zanzinews.com/2013/11/mbona-mimi-nipo-mnahangaika-nini.html

Na A K Khiari
Nipo Kijangwani, sehemu moja nzuri na ipo katikati. Nilipojengwa miaka dahari iliyopita nilikuwa kituo cha mabasi yaendayo mashamba.

Naam wakati Serikali yangu ilipokuwa na neema nilikuwa nikitoa huduma ya mabasi yanayokwenda mashamba kwa muda mrefu mpaka serikali sijui  kama ilinichoka au ikaniona sina umuhimu tena basi ikaniacha kama nilivyo haikuniuliza ndewe wala sikio.

Tokea Mabasi ya mara mwisho yalipokoma kutoa huduma sijui ni miaka mingapi sasa maana nimeshakuwa mtu mzima na kumbukumbu imenitoka sikuulizwa tena hali yangu nnafanya nini.

Sikusikitika sana maana naijua serikali yangu nikabaki nipo nipo tu kama vijana wa sasa wanavyotuambia. Mara mbele yangu wakaja vijana wakaanza kucheza mpira kwenye viwanja, mara baadae wakaja wauza mbao wakakaa mbele wakijitafutia rizki zao.Jirani yangu nikaletewa mjengo mzuri wa Posta nikawa nnauonea uchoyo kwa uzuri wake ulipojengwa miaka hiyo. Mara hata Idara ya habari na utangazaji pale studio, Rahaleo kijana wa zamani kama mimi au mtu mzima mwenzangu naye akapata mfadhili sijui kutoka China akamjenga naye kidogo akaniacha mimi vilevile kama nilivyo. Mara nikasikia Msikiti Mkuu wa Ijumaa Masjid Mushawwar umejengwa Mwembeshauri nikadhani labda na mimi nitakumbukwa, wapi!

Nilipokumbukwa nikaambiwa sasa nitakuwa sehemu ya kuoshea magari ( car wash), Mara nikaambiwa ile Sheli ya zamani ya mabasi sasa tutaigeuza Sheli kamili ya mafuta. Yote haya yanafanyika sijasikitika lakini nkaungulika maana mimi nilipojengwa nilikuwa kituo cha mabasi sikuwa hayo mengine ninayoletewa tu kwa sababu ya kuwepo kwangu hapo. Lakini nifanyeje na mimi pale nimewekwa tu maskini wa Mungu mie.

Hivi majuzi nimesikia shaghalabaghala ya kuhamishwa kituo kikuu cha Daladala Darajani na kuanzishwa vituo vidogo vidogo, Malindi, Donge na Mnazimmoja jirani na baraza la wawakilishi la zamani ndipo nikapata na mshangao mbona mimi nipo?

Nimenyamaza siku nyingi lakini sasa itanibidi niseme maana sijisifu lakini nnaamini ninazo sababu za kuwa kituo kikuu cha Daladala.

Nipo sehemu ya kiistrateji nzuri kwani barabara zote zinazoingia mjini zinaweza kunifikia hapo kiurahisi bila usumbufu wala msongamano tofauti na Darajani ambapo msongamano unakuwa mkubwa kwa kuwepo Barabara moja tu inayofikia stendi kuu.

Wa Bububu na wanaotokea nji hiyo watafikia wakitokea Kinazini. Wa Amani na wanaotokea njia hiyo akina wa Daraja Bovu watafika wakitokea  Mwembeladu. Wa Fuoni pamoja na wa Kwarara, Nyarugusu, Chuo watafikia wakitokea Posta. Wa Uwanja wa ndege, Chukwani na Kisauni na Jan’gombe watafikia wakitokea Miembeni. Na wanaotoka mjini watafikia wakitokea Rahaleo. Umenipata hapo? Niambie nani mwengine ana sifa kama zangu?

Kweli nnaweza kuwa na udhaifu wangu kwamba Hawa wanaotaka kwenda Hospitali nitawafanya nini nao ndio muhimu?. Ngoja niwaambie Nitawaomba wenye kupanga njia (Route) waniandalie Ruti mpya ya town tu itakayoanza Kijangwani, ipitie Mwembeladu, Kinazini, Mlandege, Malindi, Darajani, Hospitali, Michenzani na Kurudi Kijangwani (Problem solved). Ila mwananchi kidogo itambidi apande, wakati mwengine Daladala zaidi ya moja.

Pia kitu chengine nnachoringia ni kwamba miundo mbinu kwa ajili ya kazi hii tayari ninayo, nitahitaji kuboreshwa tu kidogo kwe kutolewa Barabara zitakazoniunganisha na Barabara kuu zilizopo. Nitaweza kuwa na sehemu kubwa ya kuegesha magari ya daladala na kukidhi mahitaji ya Magari yaliyopo kama nitapata mtaalamu mzuri wa kunishughulikia. Nnaringia bara ya Kinazini hadi Kariakoo ambayo ni njia nne (dual carriageway) ahsante Mzee wetu Karume alipoona mbali.

Pili Mji tayari umekuwa kwa kiasi kikubwa na wakaazi wengi hawaishi sehemu za mijini bali wako sehemu nje ya miji na hivyo huduma nyingi sasa zimeweza kusambazwa sehemu tofauti.

Hata hivyo itabidi wauza mbao pale wanisamehe kwa kuondoka na kutafuta sehemu nyengine (nitawaomba radhi kama nimewaudhi) kama nikipata dili ( deal) pamoja na kiwanja cha Komba wapya kama wataweza kunisaidia na kujiunga nami katika mkakati wangu huu wa kudai haki yangu ya asili ya kuwa ni kituo cha Mabasi au daladala basi tutaendelea kuwa pamoja. 

Ila sitokubali kirahisi kwamba nigeuzwe kituo tu bila ya kuletewa plan yenye kukidhi mahitajio yangu maana wakati mwengine kizuri hujiuza ati! Si unaona hapo juu kwenye picha ya hicho kinachoitwa kituo kipya cha Daladala kilivyo? Hata barabara hakina Je siku za mvua na magari ingia toka patakuwaje?

Nnasema hivi kwasababu pia, ingawa si vizuri kusema, lakini nnaona choyo kwamba jirani yangu pale mtoto wa juzi tu 1976, kiwanja cha kufurahisha watoto Kariakoo tayari kimepata mfadhili wa kukiboresha tena kuwa cha kisasa na kileo pamoja na maduka kadha wa kadha ( ZSSF). Je mimi wa mwaka 1947!? Hata hivyo  hapahajaribika kitu, nami nikiwepo karibu pale basi tutasaidiana yeye atafurahisha watoto na mimi nitawaleta karibu, kweli kufa kufaana. 

Na nikunon’goneze , nimesikia pale Michenzani nako pamajuzi juzi tu panataka kugeuzwa kuwa kituo cha kikuu cha biashara na kuna jimnara linajengwa kuadhimisha miaka 50 ya mapinduzi. Basi kama wangelinifikiria na mimi hasa kwa kuwepo karibu na kituo hicho nitawaletea wateja kede kede kutoka kila kona ya mji wetu.

Basi nnawakumbusha tu mbona bado nipo msihangaike  au hamjaijua thamani yangu bado? Kama mnatafuta muarubaini wa Stendi kuu ya Daladala njooni tuzungumze nnawaahidi sitowaangusha .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.