Habari za Punde

Jamii yaaswa kusajili ardhi na kupatiwa hati milki

Na Salmin Juma, Pemba

Jamii kisiwani Pemba imetakiwa  kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa na idara ya ardhi kwa kuzisajili  ardhi zao na   kupatiwa hati miliki zinazotambulika ambayo itamuepusha na  migogoro ya ardhi.

Kauli hiyo imetolewa na  afisa  mtambuzi wa ardhi,  Moh'd Salim  kutoka Idara ya Ardhi  Pemba alipokuwa  akizungumza  na  maafisa wa wilaya  pamoja wajasiriamali  kutoka  katika mikoa yote miwili.

Amesema kuwa  imeonekana  kwamba  wajasiriamali   wengi  wanakosa  fursa  za kumiliki raslimali   ardhi  pamoja  na  mambo  mengine  ambayo  yanawahusu  katika   jamii.

Aidha ameitaka jamii  kutotumia ardhi kwa shughuli zisizoeleweka  bali waitumie kwa  maendeleo  ya kijamii  na kuhakikisha kwamba  hawauzi  kiholela ardhi zao bila ya kufuata utaratibu wa kisheria  ili kuondokana na migogoro hiyo.

Nae  mratibu kutoka jumuiya ya  NGENEREKO, Mohd Nassor amesema lengo kuu ni kusaidiana  na serikali kwa kupunguza migogoro ya ardhi kwani serikali ina nia njema na kuitaka jamii kutumia raslimali zao vizuri.

Hata hivyo amesema  kuwa elimu bado ni ndogo  kwa jamii  hivyo amesema kupitia mradi huo watashirikiana na widhara husika ili kuhakikisha wanatoa elimu kwa  jamii.

Akitoa  wito  kwa niaba ya wenzake, Maryam Mohd Muhene amesema watahakikisha wanachukua juhudi katika kutoa  elimu katika vikundi vyao ili kuona kwamba wanachama wote wanakuwa na uwelewa wa kutosha juu ya hati miliki ya ardhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.