Habari za Punde

ZLSC walipoungana na mataifa mengine duniani kusherehekea siku ya haki za binadamu

Na Salmin Juma , Pemba

Kila ifikapo tarehe 10 ya mwezi  12 mataifa mengi duniani huadhimisha siku ya haki za binaadamu ikiwa ni ishara ya utetezi wa upatikanaji wa haki hizo , hatimae pia kituo cha huduma za sheria Zanzibar Legal Service Centrer  ( ZLSC ) afisi ya Pemba  wameungana na wenziwao wa mataifa tofauti kuadhimisha siku hiyo huku wakiitaka jamii kutofumbia macho vitendo au viashiria vyovyote vinavyoonyesha kuvuruga haki hizo ,wakisema kua  watu wote ni sawa mbele ya sheria.

Akifungua maadhimisho hayo katika ukumbi wa skuli ya Madungu chakechake Pemba mgeni rasmi ambae ni mrajis mkuu wa Jimbo kutoka Mahkama kuu Pemba  Mh Husein Makame Husein amesema kua haki za binaadamu zipo kisheria nchini  na zinastahiki kulindwa ili kudumisha usawa katika jamii ya watu.

Amesema kua ikiwa wao kama serikali wanazilinda haki hizo, hivyo ikitokea mtu amevunjiwa haki yake ya msingi anaweza kwenda moja kwa moja mahkama kuu huko ndipo kunapohusika na mas-ala hayo na haki itapatikana.

Akizungumzia changamoto zilizopo kisiwani Pemba katika utatuzi wa kesi za uvunjwaji wa haki za binaadamu Mrajis huyo amesema, tatizo kubwa ni kua mpaka sasa Mahkama kuu haijapata Jaji mkaazi hali  inayopelekea kesi kudorora, lakini pia amewatoa hofu wananchi kwa kusema kua changamoto hiyo ipo mbioni kutatuka hivi karibuni.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mratibu wa kituo cha huduma za sheria afisi ya Pemba Bi Fatma Khamis Hemed amesema kua kituo chao ni mdau mkuu wa kupigania haki za binaadamu pamoja na ushuri wa kisheria ambapo amewataka wananchi kujitokeza pindi tu watakapofikwa na shida ya kisheria.

Akiwasilisha mada ya HAKI ZA BINAADAMU Afisa mfawidhi  Kutoka tume ya haki za binaadamu na utawala bora Pemba Bw Suleiman Salim Ahmad amesema kua ibara ya 11 hadi ya 21  ya katiba ya Zanzibar inaeleza haki za mwanaadamu ambazo anastahiki kuzipata nchini ikiwamo Uhru wa faragha, Uhuru wa kutoa maoni na taarifa.

Akigusia njia za kihalali zinazoweza kutumiwa na jamii  iwapo wataona kuna haki imevunjwa  amesema, watu hao  wanaweza kufanya migomo na  maandamano  ya amani kufikisha ujumbe wao na mamlaka husika zitafikiwa na ujumbe huo.

Nae Afisa mipango wa kituo cha huduma za sheria afisi ya Pemba Bw:Khalfan Amour muhammed ameonyesha mafanikio yaliyofikiwa na kituo hicho mpaka muda huu ikiwa ni pamoja na kuendelea na harakati zake kama kawaida za ushauri wa kisheria na utetezi wa haki za binaadamu ambapo amesema hilo ni jambo la kujivunia kwakua zipo baadhi ya asasi zimeshindwa kuendelea na malengo yao na kusita katikaki ya safari.

Aidha amesema kua kituo kimekua na utaratibu kwa kutoa  matamko juu ya jambo linalotekea na ikiwa  kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Kimsingi haki za binaadamu ni tokea mtu anapozaliwa ikiwemo kupata elimu, haki ya kupiga kura, haki ya kutibiwa, haki ya kuishi na nyenginezo.

Maadhimisho ya siku ya haki za binaadamu yamewashirikisha watu wa makundi mbalimbali kama vile wanafunzi, PDD (afisi ya mkurugenzi wa mashtaka Pemba) Jeshi la Polisi, Jumuiya za watu wenye ulemavu na asasi mbalimbali za kiraia 

Pia washiriki walipata kuuliza maswali na kutoa michango yao juu ya haki za binaadamu  na  kauli mbiu ya mwaka huu ni "SIMAMA KWAAJILI YA HAKI YA MTU MWENGINE LEO"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.