Habari za Punde

Watendaji wa Afisi Kuu CCM Zanzibar Wapingwa Msasa.

Afisa Milki wa Chama cha Mapinduzi Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar, Mwenenzi Ndg Omar Said, (kulia) akimkakabidhi nyaraka za Kiutendaji Kaimu Mkuu wa Utawala wa CCM Afisi Kuu Zanzibar Ndg Mohammed Sijaamini kushoto hafla hiyo imefanyika katika ukumbi mdogo wa CCM kisiwandui Zanzibar
Baadhi ya Watendaji na Maofisa wa CCM Zanzibar na Wakuu wa Idara za Chama wakiitikia dua mara baada ya hafla ya makabidhiano ya Ofisi. 

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
WATENDAJI, Viongozi  na Maafisa Wakuu wa Idara  Mbali mbali za Afisi Kuu CCM Zanzibar  wametakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kunufaika na huduma bora zinazotolewa na taasisi hiyo ya kisiasa.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Utawala wa CCM Zanzibar , Nd. Mohamed Sijaamini  katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi hiyo huko Kisiwandui  Zanzibar.

Alisema mbali na CCM kuwa ni taasisi ya kisiasa bado ina majukumu ya msingi yakiwemo kusimamia vizuri utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 ili wananchi wote bila kujali itikadi zao za kidini na kisiasa wapate huduma bora za kijamii na kiuchumi.

Makabidhiano hayo yamefanyika kufuatia aliyekuwa Mkuu wa Utawala wa CCM Zanzibar, Nd. Salum Khatib Reja kuhamishiwa Makao Makuu ya Chama hicho Mjini Dodoma kwa ajili ya shughuli za kiutendaji ambapo baada ya uhamisho huo  nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Afisa Milki ya Chama hicho Afisi  Kuu Zanzibar.

Kaimu Mkuu huyo mpya wa  Utawala, alieleza kwamba utumishi uliotukuka, uadilifu, utendaji bora na ubunifu wa Maafisa hao ndiyo nyenzo pekee zitakazosaidia kuendelea kulinda heshima ya CCM katika nyanja za kitaifa na kimataifa.

Pia alisisitiza umuhimu wa watendaji hao kulinda na kusimamia vizuri taswira ya chama hicho kwa kupanga mikakati endelevu ya kuimarisha Utendaji  katika Idara za Chama na Jumuiya zake  ili kwenda sambamba na matakwa ya siasa za sasa katika Dunia ya Sayansi na Teknolojia.

“Pamoja na majukumu ya kiutendaji tuliyokuwa nayo kwa sasa ni lazima tutumie muda mwingi kufikria mipango mizuri ya kufanikisha Uchaguzi wa Chama chetu uliopo hivi sasa pamoja na kuhakikisha CCM inashinda kwa ngazi zote 2020, hapo ndio tutakuwa tumeenda   sambamba na matakwa ya muundo mpya wa Chama hicho.

Pia tunatakiwa kutumia nyenzo mbali mbali za kitaaluma tulizokuwa nazo kwa kubuni mikakati endelevu itakayosaidia chama kufikia malengo yake ya kisiasa na kiuchumi kwa ufanisi.”, alisema Sijaamini na kusisitiza ushirikiano kwa Watumishi hao.

Mapema akimtambulisha Kiongozi huyo, Afisa Milki wa CCM Zanzibar ambaye pia alikuwa akikaimu nafasi hiyo Nd.Mwenemzi Omar Said aliwataka  watumishi hao  pamoja na wanachama kwa ujumla kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Kaimu Mkuu wa Utawala huyo ili aweze kutekeleza shughuli za kiutendaji vizuri  kwa maslahi ya Chama na taifa kwa ujumla.

Aidha alisema CCM imeimarika  kisiasa na kiuchumi kutokana na kutekeleza mambo yake kwa misingi ya uwazi, weledi na umoja mfumo ambao haupo kwa vyama vingine vya kisiasa nchini.

Akitoa maneno ya Shukrani  Mkuu wa eneo la Idara ya Ogarnazesheni Zanzibar, Bi. Nadra Mohamed Juma  ameahidi kwamba watumishi hao watazifanyia kazi kwa vitendo nasaha na maagizo yaliyotolewa na kiongozi huyo mpya kwa lengo la kuhakikisha  shughuli zote za  kiutendaji na kisiasa zinaendelea kufanyika kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.