Habari za Punde

Wanaowakosesha waandishi habari, wana ajenda gani?



NA HAJI NASSOR, PEMBA

‘KUPATA habari na kutoa habari ni haki ya kila mwananchi’ ni nukuu sehemu ndogo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Ambayo imetamka hivyo, kwa nia njema kabisa, na kwa lengo kubwa kwamba, wananchi wake wa Zanzibar basi wawe sawa na wa mataifa mengine, juu ya kupata na kutoa habari.

 Kama hivyo ndivyo, pia Rais wetu mpendwa wa Zanzibar wa awamu hii ya saba dk: Ali Mohamed Shein, ni hivi karibuni tu amekemea tabia ya baadhi watendaji wenye tabia ya kuwakimbia wandishi wa habari, kwa lengo la kuficha habari.

Kwa mwenye akili, hapo amefahamu kuwa kitendo cha kuficha habari sio kizuri, maana pamoja na kukiuka Katiba, pia huwakosesha mambo kadhaa wananchi ikiwa ni pamoja na kutofahamu nini kipo, nini kinakuja, nini wanatakiwa wafanye au wajihadhari.

Wananchi wetu, naamini wanategemea sana vyombo vyetu vya habari, kwa kupata taarifa mbali mbali, tena hasa za maendeleo iwe za kiafya, elimu, siasa, imani, utamaduni, michezo na hata juu ya mwenendo wa Serikali yao, walioamua kuiweka madarakani.

Kama hivyo ndivyo, mbona waandishi wa habari walioko Pemba, wamekuwa wakikoseshwa habari, na kisha kuekewa vikwazo kadhaa na baadhi ya watendaji wakuu tena hasa wa taasisi za Serikali na mashirika ya Umma.

Waandishi wa habari walioko Pemba, wawatafsiri vipi watendaji hawa, au ofisi ni milki yao, Katiba hawaifahamu, wanapuuza nukuu ya Rais wetu, hawajiamini kuzungumza na waandishi wa habari, au ndio hao wanaodumaza upatikanaji wa habari?

Zipo taasisi za umma Kisiwani Pemba, watedaji wake tunaowaamini, wamekuwa wakiwakwepa waandishi wa habari ,wakiwa na sababu zisizoingia akili mwa biaadamu, na hasa kama wao ambao wamekabidhiwa madaraka kuziongoza taasisi hizo kwa Pemba.

Kwa mfano kikosi cha KMKM ,JKU, wizara ya Afya, wizara inayosimamia wanawake na watoto unapotaka taarifa kwa mfano juu ya walikichokifanya au malengo yao kwa mwkaa ujao, hapo ni shughuli kubwa na mtendaji wake mkuu, huthubutu kusema kuwa hilo yeye halimuhusu.

Katika kuficha kwao habari, hapo mwandishi ataambiwa kuwa kuna agizo kutoka juu, habari zisitolewa na wala yeye sio msemaji, na kutakiwa mwandishi wa habari alieko Pemba aende Unguja kwenye makao makuu ya taasisi hiyo.

Sasa natujiulize, ni juu ipi kunakotoka agizo hilo, wakati kiongozi wetu mkuu dk: Shein amesema kuficha habari sio sahihi na naamini na yeye amenukuu sehemu ndogo tu ya katiba ya Zanzibar, kwa hilo hakukurupuka.

Inawezekana wakuu wa vikosi hivi na mashirika mengine au wizara hizo zinazoficha habari Pemba, sio lengo pengine ni hao wanaoitwa mabossi wakuu walioko Unguja ndio waliowawekea kizingiti.

Ingawa kwa hawa wanaoficha habari kwa mfano KMKM Pemba, hata ushirikiano hawana, maana tulitarajia walau atoe namba ya simu ya huyo anaeitwa bossi alieko Unguja, lakini hapo si hasa kukatiwa simu kabla ya kuhitimisha mazungumzo.

Naamini kwa hawa anaofanya ukiritimba wa kihabari Pemba, inawezekana kabisa wanajua tu kuwa habari ni kwa ajili ya chakula kwa mwandishi, kwamba akimkosesha atalala na njaa.

Laa…!! hasha mwandishi wala hali habari, bali anachokitafuta ni kutekeleza wajibu wake wa kuwahabarisha wananchi juu ya kazi na majukumu yaliofanya na taasisi husika.

Hivi sasa kwa mfano wizara ya Afya na ile inayosimamia wanawake na watoto, kila unachohitaji humtaka mwandishi wa habari, aombe habari kwa njia ya barua rasmi, ingawa wanasahau kuwa wao wanapowahitaji waandishi hao, hunyanyua simu na kuwataka wafike pahala fulani ili kwenda kazini.

Au sasa na waandishi wa habari nao wawafungie vioo, na mkiwataka walioko Pemba, muende Ungua kwa wakuu wao kazi, mndhani hapo ndio itakuwa tunawaweka wapi wananchi tunaowatumikia?

Jamani tunakwenda wapi, huu ndio utendaji wa kazi wa uwazi na ukweli au ni sahihi mwandishi alieko Pemba kuvuuka maji hadi Unguja, ili apate habari ambayo Pemba yupo mtendaji ambae tunaamini anaweza kutoa habari.

Tena kwa sasa hata vile vituo vya mkono kwa mkono kwa mfano cha Chakechake ambacho kilikuwa na urafiki mkubwa na waandishi wa habari, sasa kimeshatiwa sumu kwamba ukihitaji baraua uende Wete kwa Afisa Mdhamini kutaka ruhusa.

Taasisi kama hizi zipo nyingi Kisiwani Pemba ambazo hudai kuwa zimepewa maagizo ya maandishi kutoka kwa mabosi wao walioko Unguja, kwamba wasithubutu kuzungumza na waandishi wa habari hata kwa lolote.

Jamani tuwahurumie wananchi wetu wa Zanzibar hasa walioko Pemba, ili wapate taarifa sahihi zilizomo kwenye taasisi zilizioko Pemba, au ndio waendelee kuvipenda vyombo vya habari vya nje ya Zanzibar kwa kutoa habari nzuri.

Watendaji wakuu waliopo Kisiwani Pemba ni vyema wakapewa ‘dozi’ washirikiane kikamilifu na vyombo vya habari na waandishi wa habari walioko Kisiwani humo, maana naamini migomo ya waandishi wa habari haina tija, lakini je na sisi tukiamua kuwagomea maendeleo yatapatikana?

Mbona bado kwa baadhi ya taasisi Kisiwani Pemba zinaendelea ukiritimba wa kutoa habari kwa waandishi wa habari, tuseme hawa wako kwenye dunia gani, au wakorofi ni wakuu wao waliopo makao makuu Unguja? siamani.

Inawezekana wao hawa alioko Pemba wanataka kushirikiana na vyombo vya habari, lakini kutokana na nidhamu ya waoga kwa mabosi wao, ndio maana sisi wa mrengu wa habari, pengine tunawatupia lawama wao kwa kutokujua.

Lakini mbona zipo taasisi hata Idara ndogo zinashirikiana vyema na vyombo vya habari kwa mfano Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, TRA, Shirika la Utalii, Wizara ya Biashara, Katiba na Sheria, Ofisi ya Makamu wa Pili na vitengo vyake na hata ZFA Pemba .

Hizi naamini zote ni taasisi za Umma, na zina wakuu wake Unguja, sasa tuseme kuzungumza na waandishi wa habari zinakikuka maadili, zinakikuka maagizo ya mabosi wao, haziogopi waandishi wa habari, au ndo zinazofahamu wajibu wao, jawabu ni kweli.

Hadi lini taaisis hizi zitaendelea kuwa bubu kwa waandishi wa habari, na kukosa taarifa sahihi za kuwapasha wananchi wetu, au ndio zinataka waandishi wa habari waandike wapendavyo kisha iwe ni kunyosheena vidole, hili sio jambo jema.

Mabosi wa taasisi mbali mbali walioko Unguja wakati umefika sasa, kuwaamini watendaji wenu wakuu walioko Pemba, na hasa kwa kile kinachohusu Pemba, kwa nini wasikizungumze ili wananchi wakifahamu kupitia vyombo vya habari.

Hili la kukalia habari sasa limesharithishwa hata wa baadhi masheha wa shehia, nao huuwaambia waandishi wa habari, kwamba wamekatazwa kuzungumza chochote na vyombo vya hyabari hata kwa zile changamoto zinazowakabili, wakidai kuwa hadi mwandishi apate ruhusa kutoka Wilayani.

Lakini hili ka kuwafunga midomo watendaji wasizungumze na waandishi wa habari, athari yake kamwe haishii hapo bali kama ikiachiwa basi kuna siku hata wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaweza kuzuiwa wasizungumze na vyombo vya habari.


Sote kwa pamoja, tunaweza pindi tukiamua kufanya shughuli na wajibu wetu kwa kushirikiana na tena bila ya kusimamiwa, na mjenga nchi mwananchi mwenyewe, ambao ni mimi na wewe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.