Habari za Punde

Mshambuliaji wa Serengeti Boys Aiokoa Timu ya Mjini Unguja

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Mshambuliaji wa Klabu ya Miembeni City, Ibrahim Abdallah “Imu Mkoko” jana aliikoa timu yake ya Kombain ya Mjini Unguja baada ya kufunga bao la kusawasisha katika dakika ya 69 na kufanya matokeo kuwa 2-2 dhidi ya Dulla Boys katika mchezo wa kirafiki uliopigwa majira ya saa 3 usiku katika Uwanja wa Amaan.

Katika mchezo huo Mjini ndio wa mwanzo kupata bao katika dakika ya 24 kupitia Yakoub Amour kisha Dulla Boys wakajibu mapigo katika dakika ya 33 kupitia Ali Haji na kwenda mbele 2-1 katika dakika ya 44 baada ya Simai Ali kufunga bao hilo la pili ndipo dakika ya 69 Mkoko akaikoa timu yake na kuufanya mchezo umalizike 2-2.

Mkoko alijumuishwa katika kombain hiyo punde tu aliporejea Visiwani Zanzibar mwezi uliopita akitokea mjini Gentil, Gabon katika michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya AFCON akiitumikia timu ya Taifa ya Tanzania “Serengeti Boys” baada ya kutolewa kwa kufungwa 1-0 na Niger katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Uwanja wa Port Gentil mjini Gentil, nchini Gabon.

Tayari Mkoko, amekuwa tegemeo katika kikosi cha timu hiyo na wamekuwa wakimtumia kuwa mshambuliaji wa kati tegemeo na wenyewe Mjini Unguja wanatarajia kufanya vyema kwenye Mashindano ya Vijana ya Rolling Stone ambayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake kuanzia June 29, 2017 na kumalizika July 9, 2017 huko Mbulu, Manyara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.