Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Kamanda wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar. Alipofika Kujitambulisha.

Kamanda wa Brigedia Nyuki Zanzibar  Brigedia  Generali Fadhil Nondo kushoto akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baada ya kuteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo wa JWTZ upande wa Zanzibar.Brigedia Fadhil Nondo alikuwa akikaimu nafasi hiyo tokea Mwezi Januari Mwaka huu wa 2017    baada ya  aliyekuwa akishikilia wadhifa huo Brigedia General  Cyrill  Ivor Mhaiki kufariki Dunia Mapema mwaka huu.
(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla lazima iendelee kubakia salama muda wote ili kuwapa fursa Wananchi, Wageni wanaoingia Nchini pamoja  na Raia wake wafanye mambo yao ya kawaida bila ya bughdha yoyote.

Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Kamanda Mpya wa Brigedia Nyuki Zanzibar  Brigedia General Fadhil  Nondo aliyefika Ofisini kwake kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} hivi karibuni.

Brigedia General Fadhil Nondo alikuwa akikaimu nafasi hiyo tokea Mwezi Januari Mwaka huu wa 2017    baada ya  aliyekuwa akishikilia wadhifa huo Brigedia General  Cyrill  Ivor Mhaiki kufariki Dunia Mapema mwaka huu.

Balozi Seif  alisema Zanzibar  inapaswa kuwa katika ulinzi wa uhakika muda wote kulingana na mazingira yake yaliyozunguukwa na Bahari ambayo wakati kwengine hutoa nafasi kwa wahalifu kufanya vitendo vinavyosababisha hofu na shaka kwa Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Brigedia Kamanda huyo wa Nyuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Viongozi wake itakuwa tayari wakati wote kumpa ushirikiano wa karibu zaidi ili kuhakikisha anatekeleza vyema dhamana aliyokabidhiwa na Taifa.

Hata hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake Balozi Seif alimshauri Brigedia General Fadhil Nondo kushirikiana na Makamanda na walinzi wa Vikosi vyengine vilivyopo Zanzibar ili kazi yao ya ulinzi iende vyema bila ya kukaribisha vikwazo, mikwaruzo au migongano yoyote ile isiyokuwa na faida.

Balozi Seif alimtakia kheir na mafanikio katika uwajibikaji wake huo Mpya Kiongozi huyo Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ} kwa upande wa Visiwa vya Zanzibar.

Mapema  Brigedia General Fadhil Nondo alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atakuwa tayari kupokea maagizo yoyote atakayopewa kuyatekeleza katika nafasi yake hiyo mpya ya Uongozi.

Kamanda Nondo alisema kwa mujibu wa Mfumo na Taratibu za Jeshi la Wananchi wa Tanzania  nafasi yake ya kazi inawajibika kutekelezwa kwa kupokea maagizo na ushauri kutoka kwa Viongozi wa Juu wa eneo analofanyia Kazi.

Brigedia General Fadhil Nondo kabla ya uteuzi huo alikuwa Afisa Mafunzo na Operesheni wa Brigedia Nyuki pamoja na Mkuu wa Kambi la JWTZ iliyopo Bavuai Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.