STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
12.08.2017

RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, ametoa pongezi kwa Bodi ya
Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na uongozi
wa Benki hiyo kwa mafanikio iliyoyapata na kuitaka kujiendesha kibiashara ili
ipate kuimarika zaidi.
Dk. Shein aliyasema hayo,
alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya
Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), pamoja na uongozi wa Bodi ya PBZ katika
vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.
Katika vikao vya leo, Dk.
Shein kwa nyakati tofauti alikutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango,
Bodi ya Wakurugenzi ya PBZ na uongozi wake pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika
la Bima na uongozi wake.
Aidha, Dk. Shein alieleza
kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza lakini Benki hiyo imeweza kupata
mafanikio makubwa na kusisitiza haja
ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja hatua ambayo itasaidia kuiendeleza Benki
hiyo.
Akitoa maelezo yake Dk.Shein
alisema kuwa wafanyakazi Benki hiyo ni lazima wafuate maadili, sheria na
taratibu za kazi na kuutaka uongozi kuwapongeza kwa wale wanaofanya vizuri.
Waziri wa Wizara ya Fedha
na Mipango Dk. Khalid Mohamed alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa miongozo
anayoitoa kwa Wizara hiyo na kupongeza hatua zilizofikiwa na PBZ kwa kumiliki
asilimia 41 ya mikopo kwa Soko la Mabenki hapa Zanzibar kwa mwaka 2016 hatua
inayoonesha jinsi Benki hiyo inavyoaminiwa.
Katibu Mkuu Kiongozi na
Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwa upande wake alitoa
pongezi kwa hatua kubwa iliyofikiwa na Benki hiyo sambamba na kusisitiza haja kwa
Benki hiyo kuwa Serikali ina matumaini makubwa na chombo hicho kwani ni chanzo
kimojawapo cha kuiongezea mapato yake.
Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar Said Hassan alieleza kufarajika kwake na maendeleo makubwa
yaliopatikana na PBZ na kueleza haja ya kuifuata na kuitekeleza Sheria iliyounda
Benki hiyo pamoja na zile zinazoenda sambamba na sheria hiyo.
Mapema Mwenyekiti wa PBZ Abdulrahman
Mwinyimbegu alieleza kuwa kuongezeka kwa
matawi kumesaidia kupata wateja wengi na hivyo amana za wateja zimeongezeka
kutoka TZS 33 bilioni mwaka 2001 hadi kufikia TSZ 427 bilioni mwaka 2016.
Alieleza kuwa hadi kufikia
mwezi Juni 2017 Mtaji halisi umefikia TZS 50 bilioni na PBZ inatarajia hadi
mwishoni mwa mwaka huu mtaji halisi utafikia TZS 58 bilioni.
Aliongeza kuwa Bodi ya Wakurugenzi
kwa kushirikiana na Uongozi wa PBZ katika mpango wake wa baadae imepanga
kutekeleza baadhi ya miradi katika kipindi kitakachomalizikia mwaka 2020
ikiwemo kuweka mtandao mpya wa kibenki, kuimarisha huduma za kimtandao.
Miradi mengine ni kuanzisha
mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali kwa njia ya kielektroniki, uanzishwaji wa
biashara ya kadi za Mastercard, kuongeza idadi ya matawi kwa kufungua matawi
huko Dodoma na Dar es Salaam pamoja na kujenga jengo la Makao Makuu Mazizini.
Mkurugenzi Mtendaji wa (PBZ)
Juma Ameir alieleza kuwa mapato ghafi ya benki yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi
mwaka kutoka TZS 16 bilioni katika mwaka 2011 hadi kufikia TZS 58 bilioni mwaka
2016 ambapo kiwango hiki ni zaidi ya makadirio ya TZS 55 bilioni kwa mwaka
2016.
Aliongeza kuwa amana za
wateja zimeongezeka kutoka TZS 140 bilioni mwaka 2011 hadi kufikia TZS 427
bilioni mwaka 2016 ambapo hata hivyo Benki inatarajia kuwa na amana za wateja
zenye kufikia thamani ya TSZ 478 bilioni ifikapo Disemba mwaka 2017 .
Wakati
huo huo,
Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bodi ya
Wakurugenzi ya Shirika la Bima na Uongozi wake na kumpongeza Waziri kwa
kulisimamia vyema Shirika hilo pamoja na mashirikiano makubwa yaliopo katika
Bodi na uongozi wa Shirika hilo ulipelekea kupata mafanikio makubwa.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuwepo Idara itakayoshughulikia suala zima la mafunzo kwa
wafanyakazi za Shirika hilo.
Katibu Mkuu Kiongozi na
Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja ya kutoa
elimu kwa jamii ili wapate uwelewa juu ya umuhimu mkubwa wa kuwa na Bima katika
mali zao kutokana na umuhimu wake.
Nae Mwenyekiti wa Shirika
la Bima Jumbe Said Ibrahim alieleza kuwa
mapato kwa kipindi cha miaka mitatu 2014 hadi 2016 yameongezeka kutoka TZS bilioni
17 hadi bilioni 19 mwaka 2016 ambapo alieleza kuwa licha ya kuongezeka kwa
mapato Shirika hilo limelipa TZS bilioni 6 kwa madai ya maumivu, vifo,
uharibifu wa mali, moto na mengineyo.
Mwenyekiti huyo alieleza
kuwa mbali ya huduma za Bima, Shirika hilo limekuwa likitoa huduma zake kwa
ukaribu na jamii pamoja na kutoa misaada mbali mbali katika sekta ya afya,
elimu na wananchi kwa jumla.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Bima Abdulnasir Ahmed Mohammed alieleza kuwa mtaji wa Bima kwa
mashirika ya Bima unaongezeka kila mwaka kwa mujibu wa Sheria namba 10 ya mwaka
2009.
Akitoa ushauri wa Shirika
hilo kwa taasisi nyengine Mkurugenzi huyo alisema kuwa kuna haja ya kuangalia
upya utoaji wa leseni za madereva hususan vijana, kuwa na sheria kali kwa wale wanaoendesha
vyombo kwa kasi na kwa wale wanaopakia mizigo na abiria wengi kupindukia,
kuwepo vifaa vya kuzimia moto maofisini.
Ushauri mwengine ni vyombo
vya baharini visiruhusiwe kubeba abiria mpaka vipate vibali maalum na viwe
vinafanyiwa uchunguzi kila mara, umri wa madereva wanaoendesha magari ya abiria
usipungue miaka 30 na kuendelea, iwapo ajali itatokea dereva mwenye gari
asiruhusiwe kuchukua gari yake mpaka jeshi la Polisi litakapofika kwa ukaguzi
wa gari pamoja na madereva wanaosababisha ajali mara kwa mara kunyanganywa
leseni ya udereva na kupewa adhabu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment