STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
22.09.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Ofisi ya Mufti pamoja
na viongozi wa misikiti ya kisasa inayojengwa hapa nchini kuwa na mikakati
mizuri ya uendeshaji na uangalizi kwani baadhi ya misikiti hiyo iliyojengwa kwa
gharama kubwa imekuwa ikipoteza haiba yake kutokana na uchakavu.
Alhaj Dk. Shein alisema
kuwa misikiti hiyo ya kisasa iliyojegwa kwa gharama kubwa imekuwa ikipoteza
haiba na kukumbwa na chamgamoto ya uchakavu wa miundombinu muhimu baada ya
kipindi kifupi tangu inapokabidhiwa kwa Kamati za Misikiti au wananchi wa
maeneo yanayohusika.
Hayo ameyasema leo
katika ufunguzi wa msikiti wa Jaamiu
Zinjibar ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi wa msikiti huo , Alhaj
Dk. Shein alisisitiza kuwa kila inapowezekana ni vyema Ofisi ya Mufti ikawa na
ufuatiliaji wa misikiti hiyo inayojengwa kwa gharama kubwa ili kuangalia
utunzaji na maendeleo yake.
Aliongeza kuwa miradi ya
ujenzi wa misikiti inayojengwa na ikatunzwa vizuri na kwa uadilifu, huwa
wanatiwa moyo wale wenye nia na ari ya kusaidia na kuzidi kufungua milango ya
kheri, neema na riziki kwa Waislamu wa maeneo mengine ambao bado hawajafaidika
na neema kama hiyo.
Alhaj Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Oman kwa kukubali kujenga
msikiti huo mkubwa, mzuri na wa kisasa hapa Zanzibar na kutoa shukurani kwa wananchi
wa Oman chini ya uongozi imara wa Sultan Qaboos Bin Said Bin Al Said.
Pia, Dk. Shein alimpongeza Balozi Mdogo wa Oman
aliyopo Zanzibar Dk. Ahmed Hamoud Al Habsi na wasaidizi wake kwa juhudi
walizochukua hadi mradi huo ukakamilika kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Alhaj Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuitumia misikiti ipasavyo na kujiepusha kufanya mambo
yanayoweza yakawa shirki sambamba na kujiepusha na mizozo pamoja na mifarakano
ambayo haina tija kwa Waislamu.
Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kwa bahati mbaya
katika miaka ya hivi karibuni, kuna baadhi ya Waislamu katika baadhi ya
misikiti walianza kugombania uongozi wa misikiti, walikuwepo waliotishia
kuiteka misikiti kwa kuwa katika himaya yao na baadhi yao walifanya uharibifu
wa vifaa na nyenzo.
Aliongeza kuwa wapo waliodiriki kuwafukuza waumini
wenzao na kugawana makundi ya waliokuwa na haki na wasiokuwa na haki ya
kuongoza na wengine walipoanzisha mizozo yao walidiriki hadi kupigana na
kuumizana kwani walighafilika juu ya umuhimu wa msikiti na mwenye msikiti.
Alieleza imani yake ni kwamba msikiti huo wa
Jaamiu Zinjibar utakuwa ni miongoni mwa kiungo muhimu cha kuwaunganisha
Waislamu wa Zanzibar kutokana na jina uliopewa na kuwa kitovu muhimu katika
kutekeleza ibada ya funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kukumbushana umuhimu
wakutekeleza Hijja.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwahimiza
wananchi na waumini wanapopata bahati ya kuwaleta wadhamini na wafadhili wa
ujenzi wa misikiti na madrasa na uchimbaji wa visima, wawafikishe wafadhili hao
katika sehemu za vijijini, Unguja na Pemba ili nao wazidi kupata neema hiyo
kwani misikiti na madrasa nyingi za kisasa bado zinajengwa katika maeneo ya
mjini ikilinganishwa na vijijini.
Pia, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu wote
washirikiane katika kujenga madrasa wao wenyewe badala ya kukaa na kusubiri
wafadhili katika kutekeleza ibada hiyo muhimu huku akiwataka wazazi kuwa na
moyo wa kushirikiana na walimu wa madrasa katika kusomesha na kuwalea watoto.
Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali Mmanga Mjengo Mjawiri alitoa pongezi kwa Serikali ya Falme ya Oman na
hasa Sultan Qaboos kwa msaada wa TZS
Bilioni 17.9 ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia eneo la
ujenzi, msamaha wa kodi wa vifaa vyote vya ujenzi vilivyotoka nje ya nchi na
msamaha wa malipo ya mkandarasi sawa na TZS Bilioni 3.1.
Mkataba wa ujenzi wa Msikiti huo ulitiwa saini
tarehe 6 Januari mwaka 2014 baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
iliyowakilishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Serikali ya Falme ya
Oman iliyowakilishwa na Ofisi ya Diwan of Royal Cort ambapo ujenzi umefanywa na
Kampuni ya Esteem Construction ya Dar-es-Salaam na kusimamiwa na Wahandisi wa
Ofisi ya Diwan of Royal Cort ya Oman.
Msikiti huo mkubwa una nafasi ya kusaliwa na
Waislamu zaidi ya 4,000 na una sehemu ya kusali wanaume na wanawake, vyumba
sita vya madarasa, maktaba, maabara ya lugha na kompyuta, ukumbi wa mihadhara
ya shughuli za kidini pamoja na maegesho ya gari.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo msikiti huo wa
kisasa ambao unatarajiwa kuendesha ibada na pia kutoa mafunzo mbali mbali ya
Dini ya Kiislamu na lugha mbali mbali ikiwemo lugha ya kiarabu.
Mapema Mwakilishi wa Serikali ya Oman na Katibu
Mkuu wa Kituo Kikuu cha Sayansi na Utamaduni cha Sultan Qaboos, Habib bin
Mohammed Al Riyami alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ni njia moya wapo ya
kujenga uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Zanzibar na Oman na
kuahidi kuwa Oman chini ya uongozi wa Mfalme Qaboos itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo elimu pamoja na
kuiimarisha dini ya Kiislamu.
Mufti Mkuu wa Zanzibar Saleh Omar Kabi alieleza
fadhila za kujenga msikiti pamoja na kuendeleza elimu ya dini ya Kiislamu na
kusisitiza kuwa wananchi wa Oman wakiongozwa na Sultan Qaboos wameendelea
kuonesha udugu wa damu kati yao na wananchi wa Zanzibar kama ilivyokuwa kwa Aus
na Hazraj wakati wa Mtume Mohammad (SAW).
Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Serikali ya Oman, Masheikh pamoja na wananchi walihudhuria katika
ufunguzi wa msikiti huo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Balozi Mdogo wa Oman Dk.
Ahmed Hamoud Al Habsi na viongozi wengineo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment