Habari za Punde

Waandishi wa Habari na Watangazaji Watakiwa Kutumia Kiswahili Fasaha.

Mkuu wa kitengo cha Tehama kutoka Radio Times Fm Bw. Dickson George Zuri (wapili kulia) akimuonyesha Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) moja ya mtambo unaotumika kurushia matangazo katika studio za Times Fm alipofanya ziara katika radio hiyo leo Jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akizungumza na watumishi wa Radio Times Fm (hawapo pichani) alipofanya ziara katika radio hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kushuto ni Mkurugenzi wa vipindi kutoka Times Fm Bw. Amani Missana
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wananchi moja kwa moja kupitia Studio za Times Fm alipofanya ziara katika radio hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akimsikiliza Mchambuzi Mkaazi kutoka Radio Times Fm Dkt. Bravious Kahyoza (kushoto) alipofanya ziara katika radio hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa vipindi kutoka Times Fm Bw. Amani Missana
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kushoto) katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Radio Times Fm baada ya kufanya ziara katika radio hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kushuto ni Mkurugenzi wa vipindi kutoka Times Fm Bw. Amani Missana.Picha na: Genofeva Matemu - WHUSM


Na Shamimu Nyaki - WHUSM.
Serikali imewataka waandishi wa Habari na Watangazaji kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha wanapofikisha ujumbe kwa hadhira na kuzingatia kuwa Kiswahili ndio lugha inayotambulisha Taifa letu hivyo wanapaswa kutumia lugha hiyo kwa usahihi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe alipotembelea kituo cha redio cha Times Fm ambapo amewataka waandishi na watangazaji kuzingatia Utamaduni wa nchi yetu hasa matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili ili kukitangaza na kukiendeleza kama adhma ya Serikali inavyosema.

“Nyie ni mabalozi wa lugha yetu ya Kiswahili kwa kuwa mnakitumia kila siku katika kufikisha ujumbe kwa hadhira yenu hivyo mnapaswa kukitumia kwa ufasaha kuleta maana ambayo mmeikusudia”. Alisema Mhe. Mwakyembe.

Aidha amewataka waandishi na watangazaji ambao bado hawakizi vigezo vya kuwa katika tasnia  hiyo kwenda shule kuongeza elimu na ujuzi unaotakiwa katika fani hiyo kabla muda wa ukomo uliotolewa kumalizika kulingana  na Sheria ya Habari ya mwaka 2016 inavyosema.

Akizungumzia Sekta ya Sanaa na Utamaduni Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuandaa Sera nzuri itakayoleta matokeo chanya kwa wasanii kupitia kazi zao hususani suala la wizi wa kazi hizo pamoja na kuwa na Hati Miliki ya kazi zao kwa kushirikiana na COSOTA.

Kwa upande wake Meneja wa Vipindi wa redio hiyo Bw. Amani Missana amesema kuwa redio hiyo inashiriki kwa ukamilifu katika kuhamasisha Watanzania kuunga mkono Sera ya Tanzania ya viwanda kupitia vipindi mbalimbali ikiwemo kipindi cha “Hatua Tatu” kinachorushwa kila siku za wiki asubuhi.


Hata hivyo ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapatia katika kutekeleza wajibu wao wa kuwaelimisha na kuwaburudisha wananchi na kuahidi kuendelea kufanya hivyo kwa uzalendo bila kuvunja Sheria ya kanuni za utangazaji na uandaaji wa vipindi vyenye kutoa mtazamo chanya kwa  wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.