Habari za Punde

Banka aingia katika kinyanganyiro cha mchezaji bora wa mwezi mara mbili mfululizo Ligi Kuu Bara


Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.

Leo beki wa Singida United, Shafik Batambuze amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/2018.

Batambuze anayecheza nafasi ya ulinzi wa pembeni, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Ibrahim Hajib wa Yanga na kiungo Mohammed Issa (Banka) wa Mtibwa Sugar, alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam.


Uchambuzi huo kwa mujibu wa utaratibu hufanywa na kikao cha Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.

 
Lakini mimi leo nitamzungumzia Mzanzibari kiungo wa timu ya Mtibwa Sugar Mohammed Issa “Banka” ambae ameingia katika kinyanganyiro hicho mara mbili mfululizo, yani mwezi wa Agost na Septemba.

Mwezi Agost Banka alishindwa na Mshambuliaji wa Simba ya Dar es Salaam, Emmanuel Okwi ambae alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Agosti wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018, lakini na leo tena Banka akashindwa na beki wa Singida United, Shafik Batambuze ambae amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/2018.

Ninachokiona mimi ni mafanikio makubwa kuingia katika ushindani kama huo ndani ya miezi miwili mfululizo kwenye ligi ngumu katika soka la hapa Afrika, naamini mwezi wa Oktoba atafanikiwa yeye kuwa mchezaji bora na Mungu atamsaidia.

Ndoto za kiungo huyo wa zamani wa klabu ya Chuoni ya Zanzibar zinaonekana kuzidi kukuwa kwani msimu uliopita Banka aliingia katika ushindani wa kuwania mchezaji bora chipukizi wa ligi kuu soka ya Tanzania bara, sasa haya yote ni mafanikio makubwa sana kwa Mzanzibar huyu.

Hivi karibuni kocha wa timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) Salum Mayanga alimchagua Banka kwenye kikosi chake kilichokaa kambi na kucheza na timu ya Malawi Jumamosi iliyopita ya Oktoba 7, 2017 kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa ulofanyika katika Uwanja wa Uhuru na kutoka sare ya kufungana 1-1.

Ushauri wangu kwake azidi kujituma na kujielewa kuwa yeye ni nani na anafanya nini kwani utajiri mkubwa unakuja kwake kwasababu mpaka sasa vilabu vikubwa wa soka Tanzania bara wanahitaji huduma ya kiungo huyo ambae kwasasa amekuwa gumzo katika soka la Tanzania.

Kila la kheir Banka piga kazi mdogo wangu utafanikiwa na kutimiza ndoto zako za kufika mbali katika maisha yako ya soka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.