Habari za Punde

Waandishi wa Habari Watakiwa Kutumia Lugha Sahihi.

Na Mwashungi Tahir / Ali Issa -  Maelezo Zanzibar.                                                         
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa usahihi pale wanapoandika na  kutangaza habari ili kuepusha kupotosha lugha hiyo kwa jamii.

Hayo yameeelezwa leo huko Rahaleo na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar Muhammed Seif Khatibu wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa Habari na Watangazaji juu ya Matumizi sahihi ya Lugha ya Kiswahili katika uandishi wa habari.

Amesema kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa waandishi wa habari wakati wanapoandika habari hutumia maneno yasiyo sahihi jambo ambalo ni makosa.

Alisema lugha  ya kiswahili ni muhimu kutumia kwa mwandishi wa habari kwani ndio lugha inayotumika kwa jamii hivyo ni vyema kutumia maneno sanifu yanayofahamika ambayo yamekubalika kisheria.

“Kuandika lugha sahihi ya kiswahili, fasaha na sanifu ni jukumu lenu waandishi, haifai kuandika lugha isiyofahamika sio kuandika kama mnavyotaka wenyewe ni vyema kufuata utaratibu unaokubalika kisheria na kamusi la kiswahili,”alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha alisema uandishi wa habari ni taaluma kama ilivyo taluma nyengine ya ikiwemo ya udaktari,ualimu na ina  taratibu zake maadili sheria na kanuni,hizi lazima zifuatwe vyenginevyo itapelekea kupotosha jamii wakati  waandishi ni kioo kwa jamii.

Mwenyekiti huyo aliwaomba waandishi kuzipitia habari kwa usahihi mara baada ya kuziandika kwa lengo la kuepuka maneno yasiyokubalika pamoja na kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa walengwa bila ya makosa.

Alisema lugha ya Kiswahili tayari inatumika duniani kote ambapo inazungumzwa na baadhi ya radio zinazotangaza lugha hiyo kama vile radio ya China, deuchewelle ya Ujerumani na BBC ya London Sauti ya Kiswahili Marekani na Teheran.

“Mfano kutumia neno  onesha sio sahihi  sahihi onyesha , watoto pacha sahihi watoto mapacha sio sahihi, siku za mbele sahihi na siku za mbeleni sio sahihi, abiria wawili wameuwawa katika ajali ya gari sio sahihi ila abiria wawili wamekufa katika ajali ya gari ndio sahihi na baadhi ya maneno mengine”, alifahamisha Mwenyekiti huyo.

Akitoa mada ya Matatizo ya Matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika Vyombo vya Habari Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili (BAKIZA ) Mwanahija Ali Juma  alisema kuna baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitumia maneno yasiyo sahihi jambo ambalo ni upotoshaji wa matumizi ya lugha kwa jamii.

Aidha Katibu huyo alisema kuwa baraza hilo lengo la mafunzo hayo ni kukumbusha matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili  katika vyombo vya habari na kutoa habari zenye kufahamika na kueleweka kwa jamii.

Alisema Baraza la Kiswahili Zanzibar linapongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhamasisha lugha ya Kiswahili kwa kukikuza na kukiendeleza na kuweza kutumika Afrika Mashariki.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kutumia vyema matumizi ya lugha ya Kiswahili katika fani yao hiyo na kuhakikisha kwamba maneno yatakayotumika katika vyombo vya habari ni yenye kukubalika ambayo ni sahihi na yenye ufasaha.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.