Habari za Punde

“Misiwafuge watoto waleeni”


NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAZAZI na walezi wilaya ya Chakechake kisiwani Pemba, wametakiwa kuacha kuwafuga watoto wao na badala yake wawalee, ili wakuwe katika malezi bora na makuzi, yenye kufuata nyenendo na tamaduni zenye tija.
Kauli hiyo imetolewa na Mwalimu Mkuu wa skuli ya Maandalizi ya star ya Kichungwani Chakechake, Moza Said wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi, wazazi na walezi kwenye siku ya wazazi na mahafali ya wanafunzi wao, hafla iliofanyika uwanja wa Tennis.

Alisema, mfumo wa kuwalea watoto kwa njia ya kuwafuga, na kuwapa kila watakacho na kuwaacha kufanya kila wajiskiavyo, kunaweza kuwasababishia kujikaribisha na udhalilishaji ulioshamiri katika siku za hivi karibuni.

Alisema, ni lazima wazazi na walezi hao, wakaze kamba kwenye kuwalea watoto wao, kwa mujibu wa tamaduni za kizanzibar zinavyoelekeza maadili na mwenendo mwema.

“Sisi walezi lazima tutofautishe baina ya kumlea mtoto na kumfuga, maana tukimfuga basi tutaharabikiwa hapo baadae, lazima tushirikiane kati malezi”,alisema.

Katika hatua nyengine Mwalimu Mkuu huyo wa skuli ya Maandalizi ya Star, aliwataka wazazi kuwendelea kushirikiana na uongozi wa skuli hiyo, ili wanafunzi wapate msukumo wa maisha yao ya kutafuta elimu.

Mapema aliewahi kuwa Mkuu wa wilaya ha Chakechake Hanuna Ibrahim Massoud, aliwataka wazazi na walezi, kujitahidi kuwalipia watoto wao ada, ili skuli hiyo isonge mbele.

Aidha alisema, uanzishwa wa skuli hiyo, ni kuitikia wito wa serikali wa kuwapatia elimu bora watoto wanaoanza skuli za Maandalizi, kabla ya kuingia msingi.

Hivyo, alisema kama wazazi wameamua kuwapeleka watoto wao kwenye skuli hiyo, lazima waelewa kuwa suala la kulipa ada halina mjadala.

“Mimi niwataka wazazi wale wazito wa kutoa ada, sasa wajikaze sana maana, mambo mazuri yalipo Star nasari, pia yanategemea ulipaji wa ada za watoto wenu”,alifafanua.

Akisoma risala ya Mwalimu, Hawa Abdalla Mohamed, alisema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na kukosa jengo la kuanzisha skuli ya Misingi.

Jengine, alimuomba mgeni rasmi, kushughulia uwezekano wa kuwekewa matuta kwenye barabara yao inayopita chini ya skuli yao, ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

“Karibu na skuli yetu, pana barabara inayoruhusu kupitishwa kwa vyombo vya moto tena kwa mwendo kasi, sasa kabla hapajatokezea ajali, lishughulikie”,alishauri.   


Awali wanafunzi hao katika skuli ya Maandalizi ya Star, iloanza zaidi ya miaka nane sasa, walionyesha umahiri wao katika nyimbo, sanaa, tamaduni, kucheza, michezo ya kuvuta kamba na kupasua mabofu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.