Na Bi Hekima
Leo nina ujumbe mzito wa
kutuma.
Nimeamua kufunguka na kutominya
maneno maana naona sasa mambo na maneno yanavuka mipaka ya kiasi, uungwana na
heshima kwani kuna waja wamelewa kibri, majigambo na majivuno, ubabe na ujinsi
kiasi cha kumgeuza Mwenyezi Mungu mshiriki wao katika tabia, kauli na mila
ambazo hakika haziakisi sifa wala utukufu wa Mwenyezi Mungu.
Kuna matukio matatu ambayo
nitayajengea kupambanua hoja yangu. Jana nlikua maeneno ya Amani dukani. Wakati
nataka kurudisha gari nyuma ntoke nilipopaki ilisadifu kuwa askari kazuia gari
ili wanafunzi wavuke.
Wakati narudi nyuma niingie
barabara kuu kuna vitoto vya kiume wa darasa la 2 mpaka la nne baadhi wakiwa
wamepanda baiskeli wanapita pia njia hiyo. Sijaamini maskio yangu niliposkia
kauli yao ya kunitaka ntoke njiani wakisema "huyu mwanamke si afanye
atoke! Huyu mwanamke atatuweka hapa!" Mtoto ninayemjukuu ananiita we
mwanamke?! Hawa watoto ndo wanaonekana
wanaenda skuli, chuoni na darsa kujifunza kuwa mwanamke hata wa size ya dada,
mama, shangazi au bibi yako ni "mwanamke tu!" Tena hukwita kama taka
taka fulani hivi.
Lakini inapaswa nisishangae
maana huu wa kuwadhalilisha, kuwapuuza na kuwadharau wanawake ni utamaduni
ulioenea hata kwa wanaojivunia kuwa "wacha mungu".
Wapo waja wanaamini kuwa
waliotukuzwa na wanaofaa ni wanaume tu. Si kwa sababu yoyote ila jinsi yao tu.
Hivyo kuna mja mmoja kuna siku tunaenda kusali ikasadifu wanaume wanasali juu
wanawake chini akatukejeli kwa kusema "huko ndio kwenu. Nyinyi daima watu
wa chini tu!" Narudia alikuwa naye anaenda kusali lakini roho yake ina
mawazo na mtizamo kuwa yeye "bora" kwa vile tu ni mwanamme.
Majuzi nlikua nimemtemblea
mtu nka paki gari sehemu nliokuta wengine wameweka. Ingawa nafasi ilikua
imebanwa kwa vile gari yangu ndogo ikaingia. Nimeacha njia ya kuweza kupita
mtu. Nikiacha mzigo tu mitaa ya ng'ambo hivyo nlikua sina ukaazi hapo baada ya
dakika nkatoka.
Kwa mshangao nkakuta kuna
mtu kaweka pikipiki yake mbele ya gari yangu. Nimesubiri mda kuona kama
miongoni mwa waliokaa vibarazani watasema chochote au kuja kuondoa. Kila mmoja
kabaki alipokuwa wana 'check' situation.
Baada mda akapita kijana
mmoja nkamuomba nsaidie kuiweka pembeni kidogo niweze kutoka. Mara akatoka
kijana na jiwe, mtoto ambaye namzaa kwa umri mkubwa tu, akitufurumushia matusi
ya "mwanaharamu wewe, ….nina …mamako ishike uone!!"....Hakika
sijamfahamu nini maana yake.
Hata hivyo akaja akaiondoa
pikipiki yake akilalama kuwa nilipoweka gari ni "njia kubwa". Mimi
sijaona njia. Nimeona uchochoro wa wapita kwa miguu. Hilo mmoja pili hakujakuwa
na namna ya kusema kuwa hapa kuna njia huwa tunatumia siku nyingine gari
jitahidi kuiweka vile! Inakuwaje mtoto mdogo kwa vile tu "mwanamme"
anadhani ni haki yake kuongea na wewe anavyotaka au hata kukuvunjia heshima?
"Ndio pepo iko chini ya miguu ya mama hiyo?" Ndivyo kumtukuza
mwanamke hivi?
Tena narudia kuwa sishangazwi
kwani wakuwafunza nao hawana busara, hawana malezi, hawana upeo na wala hawana
'humility'. Ukisikiliza yanayoitwa mawaidha ambayo yanarushwa masaa 24 katika
radio na kanda na hata katika cable basi asili mia 95 ya mawaidha hayo ni
kuhusu wanawake. Kati ya hayo 5% ni kuhusu utii wa wanawake kwa 'wanaume hasa
waume zao. Mawaidha yaliyobaki ni kuwakejeli, kuwa kebehi, kuwa laani, kuwa
umbua, kuwa kosoa alimradi kuwatoa kila walakini kuwanyima utukufu na utu wao.
Sijaona popote mwanamme
anahakikisha chochote au akitajwa kuwa BORA kwa vile tu yeye ni mwanamme. Wala sijaona popote ambapo
alichoharamishiwa mwanadamu kimeharimishwa kwa misingi ya ubaguzi. Wala
sijasoma popote ambapo Mwenyezi Mungu anahimiza binadamu wadhalilishane, au
wahujumiane au waumbuane au wakebehiane.
Sasa ubavu huu wa kibri kiliokithiri wanaume wanaojiita waislamu
wanaupata wapi? Watakaa katika majukwaa
wakibwabwaja maneno bila ya kujali aina ya hadhira iliyopo ila ya kuwa na kiasi au uchaguzi nini
wanasema na nani wanamwambia na kwa malengo yepi.
Ninalolitambua mimi ni kuwa
waja wa namna hii na 'siasa zao za jinsi au za dini' hazina malengo mema ya
kukuza upendo au heshima kati ya watu.
Nina hakika katika moyo
wangu kuwa Mwenyezi Mungu anayehubiriwa siye Mwenyezi Mungu aliyemjaalia kila
mwanadamu utukufu. Nina hakika kuwa kamwe kwa kuumba viumbe tofauti katika
dunia dhamira ya Jalali kamwe haikuhusu kunyima wengine utu na kuwafanya
wengine Bora wakuu wa kiburi na majivuno.
Nina hakika kuwa hakuna
utukufu katika tabia iliyomfakarisha sheitan na Muumba wake hivyo imani ya
namna hiyo haiwezi kuwa na tija. Na nina hakika silazimiki kuvumilia,
kukubaliana wala kuweka uzito katika matamshi, utamaduni na utashi unaojenga na
kupalilia tabia za kishetani.
KUBWA zaidi kama mwanamke Si
RADHI kwa matamshi, maneno ama kauli zenye lengo la kuudhalilsiha utu na
utukufu wangu. SI RADHI na watu wanaoneza utamaduni unaohimiza watu
kudharauliana, kubezana au kuumbuana.
Ijumaa hii namuomba mwenyezi
Mungu awazindue waja waliojisahau na kumfuata 'shaitan' kwa mawazo na majivuno
awazindue na watubie, la kama walizaliwa na mwanamke kama mimi, wakalelewa na
kukuzwa na mwanamke kama mimi na wakapata faraja na maliwazo kwa mwanamke kama
mimi wakaosa kumshkuru, kumheshimu na kumuenzi basi hujuma zao ziwarudi,
ziwasute na ziwafadhaishe kwa udhalimu wanaotufanyia na kwa upotofu
wanaosababisha hata kwa kizazi kinachoinukia. Ya Rabbal Alamin.
No comments:
Post a Comment