Habiba Zarali, Pemba
MKUU wa Wilaya ya
Mkoani kisiwani Pemba, Issa Juma Ali, amewataka viongozi wa Wilaya hiyo kufanya
kazi zao kwa uadilifu , kufuata sheria na mipaka inayowaongoza, ili waweze
kutimiza majukumu yao kikamilifu bila ya hitilafu yoyote kujitokeza.
Kauli hiyo aliitowa huko Ofisini kwake ,alipokuwa
akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo masheha na madiwani wa wilaya hiyo kwa lengo la
kuwatambulisha wajibu wao katika kuwatumikia wananchi.
Alisema
upatikanaji wa ufanisi katika kazi hutokana na
mashirikiano yaliyopo kati ya viongozi ambao ndio watoa
huduma na wananchi wanaopokea huduma hizo.
Alifahamisha kila mmoja ni vyema akafanya kazi zake
bila ya kumuingilia mwenzake ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana bila ya
chuki na uhasama ndani yake.
“Katika kazi kila mmoja ana majukumu yake ya kufanya
hivyo basi ni vyema mukawa na umoja na mashirikiano ili kazi zenu ziweze
kufanikiwa na kuleta tija”, alisema.
Aidha mkuu huyo wa wilaya, aliwataka
watendaji hao kuendelea kusimamia shughuli zote za
maendeleo na kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika kwa
kila linalotendeka.
Kwa upande wak,e Sheha wa Shehia ya Ng’ombeni , Subira
Iddi Mohamed, alisema pamoja na mashirikiano hayo ipo haja ya
kuongeza nguvu katika sekta ya elimu ili wanafunzi waweze
kuleta matokeo mazuri zaidi.
Alisema wapo baadhi ya wanafunzi wilayani
humo hushindwa kushuhulikia masomo yao na kujishughlisha
na mambo yasiyo wahusu ikiwa ni pamoja na
kuangalia Tv hadi saa sita za usiku
jambo ambalo linachangia kuleta matokeo mabaya.
Alieleza kutokana na umuhimu wa elimu ni vyema
yawepo mashirikiano ya pamoja kati ya wananchi na viongozi wao kwani muda
utakapowapita watoto hao bila ya kusoma hawatoweza kuipata tena elimu
waliyoikosa .
“Bila ya kuwaekea mikakati madhubuti ya
kujishughulisha na kusoma wanafunzi wataharibika na tutabakia na janga la
vijana wasio na muelekeo katika wilaya yetu na kuiwekea serikali mzigo
usiobebeka ”, alisema .
Nae Diwani wa
kuteuliwa wilaya ya Mkoani, Abdallah Ali Muhamed, alimpongeza
mkuu huyo wa wilaya na kusema kuwa watahakikisha wanaendeleza ushirikiano kati yao kwa lengo la
kuendeleza umoja utakaoleta maendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Hivyo viongozi hao waliahidi kutowa
ushirikiano kati yao na mkuu huyo ili kuhakikisha wilaya hiyo inasonga mbele
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment