Habari za Punde

Jamii yatakiwa kufahamu tatizo la kifua kikuu ili kukabiliana nalo

 Msaidizi Meneja kitengo shirikishi Ukimwi,Kifua kikuu na Ukoma Issa Abeid akizungumza machache na kumkaribisha Waziri wa afya Hamad Rashid Mohamed kuzungumza na waandishi wa habari  kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku hiyo hapo kesho Machi 24 – 2018.
  Meneja kitengo shirikishi Ukimwi,Kifua kikuu na Ukoma Farhat Khalid akitoa ufafanuzi namna ya kupunguza maambukizi ya Kifua Kikuu
 Waziri wa afya Zanzibar Hamad Rashid Mohammed akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hawapo pichani kuelekea  katika kilele cha maadhimisho  ya  siku ya Kifua Kikuu machi 24.
 Mwandishi wa habari wa ITV na Radio ONE Farouk Karim akiuliza maswali katika mkutano huo


Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akitoa shukurani kwa waandishi wa habari na wadau mbalimbali waliojitokeza katika mkutano huo.(Picha na Abdalla Omar Maelezo – Zanzibar).

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  23.03.2018

Jamii imetakiwa kulifahamu vyema tatizo la kifua kikuu na kushirikiana na Wizara ya afya kupitia Kitengo shirikishi cha UKIMWI, Homa Ya Inni, Kifua kikuu na Ukoma ili kukabialiana na tatizo hilo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed alipokuwa akizungumza na Wanahabari ofisini kwake Mnazimmoja mjini Zanzibar kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Kifua kikuu duniani.

Amesema Maradhi ya Kifua kikuu, ni moja kati ya maradhi ambayo Shirika la afya Duniani limeyapa kipaumbele ili kuweza kufanikisha mapambano dhidi yake.

Waziri Hamad amesema kila ifikapo Machi 24 ya kila mwaka ndiyo siku ya maadhimisho ya  Kifua Kikuu ulimwenguni ambapo hutumika kuikumbusha  na kuishajihisha jamii kuwa Kifua Kikuu bado ni janga kubwa katika jamii.

Aidha kupitia maadhimisho hayo Wizara ya afya ikishirikiana na Viongozi mbali mbali huitumia fursa hiyo kutathmini juu ya hali ya maradhi nchini na kuandaa mikakati madhubuti ya kupambana nayo.

Akielezea hali halisi ya Maradhi hayo kwa Zanzibar, Waziri Hamad amesema Zanzibar huwa na wastani wa wagonjwa wapatao 700 hadi 900 wanaogundulika na maradhi haya kila mwaka.

Waziri Hamad amesema Maadhimisho ya mwaka huu yameambatana na ujumbe usemao “tunahitaji viongozi mahiri wa kuongoza mapambano ya  kumaliza kifua kikuu ”

Akielezea kuhusu ujumbe wa Mwaka huu Waziri Hamad amesema Viongozi wa ngazi zote ikiwemo kiserikali, kisiasa na kijamii kuzungumzia Kifua kikuu kwenye vikao vyao na mikutano ya hadhara ili kufanikisha azma ya kupunguza maambukizi ya Kifua kikuu.

Amesema ni vyema pia kuwashajihisha wale wote wenye dalili za maradhi ya Kifua kikuu kufika mapema  hospitali na vituo vya afya  kwa ajili ya uchunguzi na  tiba sahihi ya Kifua kikuu.

Amefahamisha kwamba kuwahi mapema na kupatiwa tiba sahihi mapema ndiyo njia kubwa katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu kuenea katika jamii.

Awali Naibu Waziri wa Wizara hiyo Harus Said Suleiman alisema huduma za matibabu ya Kifua kikuu zimeimarishwa kwenye vituo vyote Mijini na mashamba.
Alisema huduma za uchunguzi na matibabu ya Kifua kikuu hutolewa bure bila ya malipo yoyote katika vituo vya afya au hospitali za Serikali, baadhi ya vituo vya mashirika ya dini na baadhi ya vituo na hospitali za watu binafsi.

Aidha elimu ya Afya pamoja ya namna ya dalili na namna  kujikinga  na maradhi haya hutolewa sehemu mbali mbali zikiwemo maskuli,  pamoja na sehemu nyengine mijini na vijijini pindi tu mgonjwa anapogundulika.

Kwa upande wake meneja Kitengo shirikishi cha UKIMWI, Homa Ya Inni, Kifua kikuu na Ukoma Zanzibar Farhat Khalid amezitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na Kukohoa kwa muda wa wiki mbili au zaidi, Kupata makohozi ambayo yamechanganyika na damu na Homa za hasa wakati wa jioni.
Dalili zingine ni pamoja na kutokwa na jasho jingi ambalo si la kawaida wakati usiku, kukosa hamu ya kula pamoja na kupungua uzito au kukonda.
Kilele cha maadhimisho hayo ni hapo kesho Machi 24 ambapo kutakuwa na maandamano yatakayoanzia Viwanja vya Jimkana na kumalizia kwa mkutano katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.