Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza Balozi wa Uturuki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Ali Davutaglu alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo wakati wa mazungumzo yao .[Picha na Ikulu.] 27/032018
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameihakikishia
Uturuki kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande
mbili hizo na kusisitiza ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya Zanzibar na
mji wa kitalii wa Antalya uliopo nchini humo.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Ali Davutaglu aliyefika
Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kufanya mazungumzo
na Rais wa Zanzibar.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea
kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii hivyo ni vyema mashirikiano yakaimarika zaidi
kwa watalii wanaofika eneo la kitalii la Antalya nchini Uturuki wakafika na
Zanzibar.
Alieleza kuwa mji wa
kitalii wa Antalya nchini Uturuki lumebarikiwa kuwa na vivutio vingi sambamba
na hali ya hewa nzuri ambapo sifa zote hizo zinafanana na Zanzibar, hivyo ni
vyema ukawepo ushirikiano kati ya pande mbili hizo katika kuwaleta watalii
wanaofika Antalya kuja kutembelea na Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa changamoto ya usafiri wa moja kwa moja kati ya Uturuki na
Zanzibar iliyokuwepo hapo siku za nyuma hivi sasa haipo kutokana na kuwepo kwa
usafiri wa ndege ya Kampuni ya “Turkish Airline” inayofanya safari zake kati ya
Istanbul na Zanzibar.
Rais Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo wa Uturuki fursa iliyotolewa na
Zanzibar kwa kuikaribisha nchi hiyo kuweka ubalozi wake mdogo hapa Zanzibar
kama ilivyo kwa baadhi ya nchi kama vile, China, India, Msumbiji na Misri.
Dk. Shein alimueleza
Balozi huyo kuwa iwapo hilo litafanikiwa litasaidia kwa kiasi kikubwa
kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo katika kuendeleza sekta
kadhaa ikiwemo biashara kati ya wananchi wa pande mbili hizo.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein aliipongeza Uturuki kwa kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar
huku akisisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano katika sekta ya elimu,afya,
uwekezaji na sekta nyenginezo ambapo katika sekta ya elimu alieleza haja ya
kuwepo mashirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo
Kikuu cha Ankara nchini Uturuki.
Rais Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo wa Uturuki kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya pande
mbili hizo uliimarika zaidi pale Rais aliyemaliza muda wake Rais Abdullah Gul
alipompa muwaliko kutembelea nchini humo na kufanya ziara mnamo mwaka 2011
hatua ambayo iliendeleza matembeleano kati ya viongozi wa Tanzania na Uturuki.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliipongeza Serikali ya Uturuki chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip
Erdogan kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya
maendeleo ikiwemo sekta ya elimu kwa kuendelea kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi
wa Zanzibar.
Nae Balozi wa Uturuki
nchini Tanzania Ali Davutaglu alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Uturuki itaendeleza
uhusiano na ushirikiano wake kati yake na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuunga
mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.
Katika mazungumzo
hayo, Balozi Davutaglu alimueleza Dk. Shein kuwa Uturuki itaendelea kutoa
ushirikiano wake kwa Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwemo sekta
ya elimu na kuahidi kuwa mashirikiano katika sekta ya utalii hasa kati ya mji
wa kitalii wa Antalya na Zanzibar kuwa nchi yake italifanyia kazi.
Wakati huo huo, Rais
Dk. Shein alifanya mazungumzo na ujumbe wa Kampuni ya Mawasiliano ya HUAWEI
kutoka China chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Kampuni hiyo tawi la
Tanzania Gao Mengdong, Ikulu mjini
Zanzibar.
Dk. Shein aliipongeza Kampuni
ya HUAWEI kwa kuendeleza mawasiliano ya kisasa kwa kuanzisha simu zenye mfumo
wa kisasa wa 5G pamoja na kueleza maendeleo ya miradi yao kwa Zanzibar pamoja
na mchakato wa mradi wa umeme wa kutumia jua.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment